Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 18 Mei 2020 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 18 Mei 2020 ameadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II.  (AFP or licensors)

Mtakatifu Yohane Paulo II: Sala, Uwepo, Huruma na Haki ya Mungu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mtakatifu Yohane Paulo II alibahatika kuwa ni kiongozi na mfano bora wa kuigwa. Kwa hakika alikuwa ni mchungaji mwema aliyekita maisha yake katika sala; ukaribu kwa watu wa Mungu; akawaonesha upendo wa dhati; akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Alikuwa kweli ni shuhuda wa huruma na haki ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 18 Mei 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Altare ya Mtakatifu Yohane Paulo II kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II. Ibada hii imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka ndani na nje ya Vatican, waliokuwa na uhusiano wa pekee kabisa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kwa Ibada hii, Baba Mtakatifu Francisko anafunga rasmi maadhimisho ya Ibada za Misa Takatifu zilizokuwa zinarushwa moja kwa moja kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, ili kusaidia kuboresha maisha ya watu wa Mungu waliokuwa wanapambana na changamoto za maisha ya kiroho, baada ya Makanisa sehemu mbali mbali za dunia kufungwa kama sehemu ya protokali ya kudhibiti kuenea kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, waamini watapyaisha tena mahusiano na mafungamano yao ya maisha ya kiroho kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Sakramenti na Ibada mbali mbali zinazoendeshwa na Mama Kanisa. Katika utangulizi wa Ibada ya Misa Takatifu, Papa Francisko amemshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aliyemteua Mtakatifu Yohane Paulo II ili kuliongoza Kanisa la Kristo Yesu. Sasa awakirimie waja wake nguvu ya kuweza kuyaishi mafundisho yake kwa ari na moyo mkuu; asaidie kufungua nyoyo za waamini wake, ili ziweze kujazwa neema ya Kristo Yesu, Mkombozi pekee wa binadamu. Watu waokolewe kwa neema hii! Mtakatifu Yohane Paulo II alibahatika kuwa ni kiongozi na mfano bora wa kuigwa. Kwa hakika alikuwa ni mchungaji mwema aliyekita maisha yake katika sala; ukaribu kwa watu wa Mungu; akawaonesha upendo wa dhati; akasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu.

Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu amefafanua kwamba, Katika Agano la Kale, Mwenyezi Mungu ili kuonesha huruma na upendo kwa waja wake, alikuwa anawatumia Nabii, aliyefahamika kuwa ni Mtu wa Mungu. Kwa njia hii, Mwenyezi Mungu alikuwa anawatembelea waja wake. Katika Ibada ya Misa Takatifu anasema Baba Mtakatifu Francisko, familia ya Mungu imekutana, ili kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye katika huruma na upendo wake wa dhati, miaka mia moja iliyopita alimtuma, mtu mmoja, ambaye alimwandaa kwa Daraja ya Upadre na Uaskofu ili kuliongoza Kanisa lake, kwa sababu Mwenyezi Mungu anawapenda waja wake, amewatembelea na kuwapelekea Mchungaji mwema. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni Mtu wa Mungu, aliyekita maisha yake katika sala, licha ya dhamana na majukumu yake ya: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Alitambua kwamba, dhamana na wajibu wa kwanza wa Askofu ni kusali; na inapofika jioni, kuchunguza dhamiri yake, ili kuangalia ni muda gani ameweza kuutumia kwa ajili ya kusali.

Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mtu wa watu, aliyeonesha uwepo wake wa karibu kwa watu wote. Ni kiongozi aliyesadaka maisha yake kwa kutembelea sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwatafuta watu wa Mungu ili aweze kuwashuhudia na kuwatangazia furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kwa hakika, akawa ni kielelezo cha uwepo wa Mungu kati pamoja na waja wake katika hija ya maisha yao hapa duniani. Mtakatifu Yohane Paulo II, amekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa uwepo kati pamoja na waja wake. Ni kiongozi aliyekuwa na upendo wa dhati kwa watu wa Mungu, akajipambanua kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Alikazia Mafundisho Jamii ya Kanisa. Alikuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na haki ya Mungu kwa waja wake. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma na haki ni sawa na chanda na pete, kwani ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha ya mwanadamu.

Kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, amejitahidi kuwafunulia watu, huruma na upendo wa Mungu, kama Kristo Yesu alivyomfunulia Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kowalska wa Shirika la Masista wa Mama wa Mungu wa Huruma. Tangu sasa, Mtakatifu Faustina, atakuwa anaadhimishwa katika Kumbukumbu ya Hiyari na Kanisa zima, kila mwaka ifikapo tarehe 5 Oktoba. Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaomba waamini, lakini zaidi, viongozi wa Kanisa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba neema ya kuwa ni watu wa sala, ukaribu na watu wa Mungu pamoja na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki na huruma ya Mungu kwa waja wake. Amewaombea waamini waweze kuwaka moto wa mapendo, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Moto huu uliwaka ndani mwake, kiasi cha kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake!

Papa: Jubilei 100 Yrs

 

 

18 May 2020, 14:00