Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asema: Wosia wa Kristo Yesu kwa wafuasi wake: Amri Mpya ya Upendo na Ahadi ya Roho Mtakatifu Mfariji, Msaidizi mwingine! Baba Mtakatifu Francisko asema: Wosia wa Kristo Yesu kwa wafuasi wake: Amri Mpya ya Upendo na Ahadi ya Roho Mtakatifu Mfariji, Msaidizi mwingine! 

Papa Francisko: Wosia wa Kristo: Upendo na Roho Mtakatifu Mfariji

Wosia wa Kristo: Mosi ni kushika Amri Kuu ya Upendo na pili ni Ujio wa Roho Mtakatifu mfariji ambaye ni Msaidizi mwingine. Katika muktadha huu, Kristo Yesu anaunganisha upendo unaopaswa kunafsishwa kwa kushika Amri zake. “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Tafakari ya Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Pasaka, tarehe 17 Mei 2020 amekazia mambo makuu mawili yanayofumbatwa katika Injili kama ilivyoandikwa na Yohane 14: 15-21. Mosi ni kushika Amri Kuu ya Upendo na pili ni Ujio wa Roho Mtakatifu mfariji ambaye ni Msaidizi mwingine. Katika muktadha huu, Kristo Yesu anaunganisha upendo unaopaswa kunafsishwa kwa kushika Amri zake. Hii ni sehemu ya hotuba ya wosia ambao Kristo Yesu alikuwa anawapatia wafuasi wake akisema, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu”. Anaendelea kusema, “Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake”.

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwamba, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake kumpenda kwa kujikita katika mchakato unaowataka kufuata njia itakayowawezesha kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Huu ndio muhtasari wa Amri Mpya ya Mapendo: “Kama nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Watu watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” Yn. 13:34. Mkazo unaotolewa na Kristo Yesu ni wanafunzi wapendane wao kwa wao kama vile alivyowapenda mwenyewe upeo! Upendo huu usiokuwa na masharti unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kama kielelezo cha utashi wake. Kristo Yesu ili kuwasaidia wafuasi wake kujikita katika njia hii anawaahidi kwamba, atamwomba Baba yake wa mbinguni naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nao hata milele.

Huyu ndiye yule Roho wa kweli, Roho Mtakatifu Mfariji, atakayewajalia akili ya kusikiliza na ujasiri wa kutekeleza maneno yake. Huyu ndiye Roho Mtakatifu, Paji na Upendo wa Baba wa Mbinguni anayemiminwa kwenye sakafu ya kila moyo wa Mkristo. Baada ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu anasema Baba Mtakatifu Francisko, upendo wa Kristo Yesu umetolewa kwa wale wote wanaomwamini na waliobatizwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani: Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu Mfariji, anawaongoza, anawaangaza na kuwaimarisha, ili kila mmoja wao aweze kutembea katika hija ya maisha bila wasi wasi na mashaka hata pale anapokumbana na adui pamoja na vikwazo; wakati wa raha na machungu, daima akiwa imara na thabiti katika njia ya Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu anasema, yote haya yanawezekana ikiwa kama Wakristo wataonesha fadhila ya unyenyekevu kwa Roho Mtakatifu, ili kwa njia uwepo wake tendaji, aweze kuwafariji na kuigeuza mioyo yao ili kukumbatia na kuambata ukweli na upendo. Kutokana na udhaifu wa binadamu unaowatumbukiza katika kutenda ubaya na dhambi, Roho Mtakatifu anawasaidia waamini kutekeleza amri za Kristo. Waamini wamepewa Amri ya Upendo kama kioo kinachowawezesha kuona udhaifu wao wa kibinadamu na pale wanapoteleza na kuanguka. Waamini wamepewa Neno la Mungu kama Neno la Uhai linaloleta mabadiliko katika maisha ya mwamini; Neno linalopyaisha na kutakasa, ili hatimaye, kuweza kumjalia mwamini huruma na msamaha wa Mungu usiokuwa na kikomo! Hivi ndivyo ulivyo msamaha wa Mungu. Neno la Mungu ni taa inayoangazia miguu ya waja wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, yote hii ni kazi ya Roho Mtakatifu, Paji la Baba wa Milele, ambaye ni Mungu mwenyewe anayewasaidia waamini kuwa watu huru, wanaopenda na kutambua maana ya kupenda! Hawa ni watu ambao wamefahamu kwamba, maisha ni utume unaowataka kutangaza na kushuhudia matendo makuu ya Mungu yanayoyotekelezwa na wale wote wanaojiaminisha kwake. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko amemgeukia Bikira Maria, Mfano wa Kanisa, ambaye alibahatika kuwa ni msikivu mzuri wa Neno la Mungu na akawa tayari kupokea Paji la Roho Mtakatifu, awasaidie waamini kuiishi Injili kwa furaha kwa kutambua kwamba, wamempokea Roho Mtakatifu, Moto wa Mungu unaopasha joto nyoyo zao na kuyaangazia mapito ya waamini wake!

Papa: Roho Mtakatifu Mfariji

 

 

17 May 2020, 13:42