Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Mei 2020, amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa wanamichezo mjini Vatican na kuwapongeza kwa kuchangia dhidi ya COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Mei 2020, amekutana na kuzungumza na wawakilishi wa wanamichezo mjini Vatican na kuwapongeza kwa kuchangia dhidi ya COVID-19.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Wanamichezo Wachangia Vita Dhidi ya COVID-19!

Papa Francisko: Michezo inapaswa kuchangia: ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao kama ambavyo walivyofanya kwa kukusanya fedha zitakazopelekwa kwenye Hospitali ya Papa Giovanni XXIII iliyoko huko Bergamo na kiasi kingine, utapewa Mfuko wa Hospitali Brescia, maeneo ambayo hivi karibuni, yalikuwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, michezo inayo nafasi muhimu sana katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Michezo ni nyenzo msingi katika kusimamia na kudumisha haki msingi za binadamu; ni njia ya mchakato wa utakatifu; ni mahali muafaka pa kuonja uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji, umoja, udugu na mshikamano wa kweli unaovunjilia mbali ubinafsi kwa kukazia umoja katika ukweli wake! Baba Mtakatifu, Jumatano tarehe 20 Mei 2020 mara baada ya Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala, Mintarafu kazi ya Uumbaji amekutana na kuzungumza na wanamichezo waliokuwa wanajiandaa kushiriki katika michezo iliyokuwa inayongozwa na kauli mbiu “Tunakimbia kwa pamoja” “We run together, Simul Currebant”. Kimsingi wanamichezo wanapaswa kuwa ni madaraja yanayowaunganisha watu mbali mbali katika jamii.

Michezo hii ilikuwa imeandaliwa na Kardinali Gianfranco Ravasi Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni akishirikiana na wadau mbali mbali wa michezo nchini Italia. Lengo ni kuhamasisha utamaduni wa amani, upendo na mshikamano unaomwilishwa katika michezo. Na kwa njia ya michezo, wadau mbali mbali waweze kuimarisha utamaduni wa watu kukutana, kushirikiana na kushikamana kama sehemu ya mchakato wa majadiliano katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amewakumbusha wanamichezo kwamba, wao ni chemchemi ya furaha na amani ya ndani kwa watu wengi wanaokutana nao katika hija ya maisha yao. Michezo inapaswa kuchangia: ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao kama ambavyo walivyofanya kwa kukusanya fedha zitakazopelekwa kwenye Hospitali ya Papa Giovanni XXIII iliyoko huko Bergamo na kiasi kingine, utapewa Mfuko wa Hospitali Brescia, maeneo ambayo hivi karibuni, yalikuwa na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Fedha hii itawasaidia madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa ni mashujaa walioko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, kiasi hata cha kuhatarisha usalama na maisha yao katika ujumla wake. Kristo Yesu alisema hakuna upendo mkubwa zaidi kuliko wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Makada katika sekta ya afya wamekuwa ni mashuhuda wa hali ya juu katika utekelezaji wa majukumu yao, ambayo wanaendelea kuyafanya kwa weledi, uadilifu mkubwa na uwajibikaji katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu anaendelea kusema, kwamba, michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo.

Lakini, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuandika ukurasa mpya wa michezo katika ulimwengu mamboleo kwa kujikita katika: ushirikishwaji; ukweli, uwazi na uaminifu pamoja kuwa na upendeleo kwa maskini. Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha! Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo.

Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, yamemekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Papa: Michezo

 

22 May 2020, 14:25