Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kushikamana katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kushikamana katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.  (AFP or licensors)

Papa: Miaka 70 ya Tamko la Schuman: Vita Dhidi ya COVID-19

Baba Mtakatifu Francisko amerejea kuhusu kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman lilipotolewa. Changamoto kwa viongozi wa Jumuiya ya Ulaya kwa sasa ni kushikamana na kushirikiana katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa sababu madhara yake ni makubwa katika medani mbali mbali ya maisha ya watu! Ubinafsi, Uchoyo na Utaifa hauna nafasi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya tarehe 9 Mei 2020 imeadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman, Waziri Mkuu wa Ufaransa lilipotolewa kunako tarehe 9 Mei 1950. Tamko hili ni chimbuko la Umoja wa Ulaya, baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.  Tamko lilipania kuhakikisha kwamba, Bara la Ulaya linasitisha chuki, uhasama na kinzani na hivyo kuanza kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani, umoja, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Ulaya. Amani Duniani itaweza kulindwa na kudumishwa kwa kujikita katika umoja na mshikamano, kwa kukusanya nguvu na rasilimali kwa ajili ya kupambana na mambo yale ambayo yanatishia: utulivu, amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Sala ya Malkia wa Mbingu, tarehe 10 Mei 2020 amerejea kuhusu kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Tamko la Robert Schuman lilipotolewa. Changamoto kwa viongozi wa Jumuiya ya Ulaya kwa sasa ni kushikamana na kuendelea kushirikiana kwa dhati katika mapambano dhidi ya janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa sababu madhara yake ni makubwa katika medani mbali mbali ya maisha ya watu!

Kwa upande wake, Kardinali Jean-Claude Hollerich, Rais wa Tume ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Jumuiya ya Ulaya, COMECE, katika mahojiano maalum na Vatican News anasema makubaliano ya Schengen yaliyotiwa mkwaju kunako mwaka 1985, ulikuwa ni mwanzo wa kufungua mipaka miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, ili kuimarisha: Umoja, mshikamano, amani na maendeleo fungamani ya binadamu. Leo hii Umoja wa Ulaya unakabiliwa na changamoto ya mapambano dhidi ya la Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Anasema, huu ni wakati wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu; kwa kuendelea kukazia mchakato wa upatanisho, haki na amani kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu Francisko, daima amekazia mshikamano unaovuka mipaka ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kuna watu wanaopoteza maisha nje ya mipaka ya Jumuiya ya Ulaya kwa: Vita, Umaskini, Njaa, Maradhi pamoja na Majanga asilia.

Katika muktadha huu, Jumuiya ya Umoja wa Ulaya haiwezi kamwe kuwageuzia kisogo wale wanaohitaji msaada wa hali na mali kwani hii ni sehemu ya utimilifu wa utu na udugu wa kibinadamu. Kwa sababu watu wanategemeana na kukamilishana na wala hakuna mtu anayeweza kuishi peke peke kama kisiwa! Kardinali Jean-Claude Hollerich, Rais wa Tume ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Jumuiya ya Ulaya, COMECE anakaza kusema, changamoto mamboleo zinahitaji watu wa Mungu kujizatiti katika ujenzi wa umoja na mshikamano; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mshikamano, umoja na udugu ni msingi wa amani ya kudumu. Huu ni wakati wa kushuhudia kwamba, Jumuiya ya binadamu inaweza kushikamana kupambana na majanga mbali mbali katika maisha kama ilivyo kwa wakati huu wa janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Ni muda wa kupambana na virusi vya uchoyo, ubinafsi na utaifa usiokuwa na mashiko wala mvuto!

COMECE: Tamko Miaka 70 Schuman.
11 May 2020, 12:14