Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, tarehe 20 Mei 2020 ametafakari kuhusu Kazi ya Uumbaji! Baba Mtakatifu Francisko katika Mzunguko wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, tarehe 20 Mei 2020 ametafakari kuhusu Kazi ya Uumbaji!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Katekesi: Fumbo la Sala: Kazi ya Uumbaji

Uhusiano na mafungamano kati ya Mungu na mwanadamu ni kielelezo cha ukuu wa Mungu aliyewaita katika utupu na kuwaumba, kumbe, binadamu ni kiumbe. Katika shida na mahangaiko ya ndani, mwanadamu anaweza kupoteza zawadi ya sala. Kumbe, Mwanadamu anapaswa kukuza na kudumisha kipaji cha kumshukuru na kumtukuza Mungu, kila anapoona Kazi ya Uumbaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, katika mzunguko mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu, Jumatano, tarehe 20 Mei 2020 ametafakari kuhusu Fumbo la Kazi ya Uumbaji! Mzaburi katika Kitabu cha Zaburi Sura ya 8: 4-5 anakiri ukuu wa Mungu Muumbaji kwani anapozingalia mbingu ni kazi ya vidole vyake, mwezi na nyota alizoziratibisha. Mtu ni kitu gani hata amkumbuke, na binadamu hata amwangalie. Amemfanya mdogo punde kuliko Mungu na kumvika taji ya utukufu na heshima! Baba Mtakatifu anakiri kwamba, sehemu ya kwanza ya Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Mwanzo inafanana kama wimbo wa shukrani unaodhirisha wema na uzuri unaobubujika kutoka kwa viumbe hai.

Mwenyezi Mungu kwa neno lake akaumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kwa neno lake akatenganisha nuru na giza. Nuru ikawa Mchana na giza akaliita Usiku. Akatenganisha majira, akaumba mimea ya aina mbali mbali. Mwenyezi Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Kumbe, Kazi ya Uumbaji ni muhtasari wa uzuri na wema wa Munu. Baba Mtakatifu anasema kwa uumbaji Mwenyezi Mungu anakiita kila kiumbe kutoka si kitu na kukipa uwepo. Viumbe vimevikwa taji la utukufu na heshima kama ambavyo anakiri Mzaburi katika Zaburi ya 8. Huu ni ufunuo wa utukufu na upendo wa Mungu. Mwanadamu hata baada ya kupoteza ufanano wa Mungu kwa dhambi zake bado anabaki kuwa ni sura na mfano wa Mungu. Mwanadamu anatambua fika uzuri na utukufu wa Mungu ulioko ndani mwake. Rej. KKK. 2566.

Baba Mtakatifu anasema, sala ya binadamu kwa namna ya pekee kabisa, inakita mizizi yake katika kipaji cha kushangaa. Ukuu na uweza wake katika medani mbali mbali za maisha, lakini yote haya si mali kitu! Katika sala mwanadamu anahisi ndani mwake huruma ya Mungu na kwamba, kila kiumbe ni sehemu ya mpango wa Mungu katika Kazi ya Uumbaji! Hakuna kitu ambacho kimeumbwa kwa bahati mbaya tu! Uhusiano na mafungamano kati ya Mungu na mwanadamu ni kielelezo cha ukuu wa Mungu aliyewaita katika utupu na kuwaumba, kumbe, binadamu ni kiumbe wa Mwenyezi Mungu. Katika shida na mahangaiko ya ndani, mwanadamu anaweza kujikuta akiteleza na kuanguka kwa kukosa kuona umuhimu wa zawadi ya Fumbo la Sala katika maisha yake. Mwanadamu anapaswa kukuza na kudumisha kipaji cha kumshukuru na kumtukuza Mungu, kila anapoona Kazi ya Uumbaji.

Uzoefu na mng’amuzi haya ndio msingi wa Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Mwanzo. Waisraeli katika hija ya maisha yao, walikumbana na matatizo na changamoto za maisha; wakakutana na adui, wakatekwa nyara na kupelekwa utumwani. Huko wakajikuta wakiwa ugenini mbali na nchi yao wenyewe, hawakuwa na Hekalu wala mahali pa sala; maisha yao ya kijamii na kidini “yakaingia mchanga”. Kumbe, Kazi ya Uumbaji kama inavyosimuliwa na Kitabu cha Mwanzo, ni sababu tosha kabisa kwa mwanadamu kupata kiu ya sala kwa ajili ya kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuishi. Sala ni nguvu ya kwanza inayomtia mtu matumaini. Kwa njia ya sala matumaini yanaendelea kukua na kuongezeka; kwa kulinda na kutunza ukweli wa mambo msingi. Watu wa sala, kimsingi ni mfano bora wa kuigwa, licha ya shida, magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha.

Watu wa sala, wanapaswa kuheshimiwa, kulindwa na kuendelezwa. Watu wa sala wanatambua fika kwamba, sala ina nguvu zaidi kuliko hali ya kukata tamaa. Hawa ni watu wanao amini kwamba, sala ina nguvu zaidi kuliko kifo na kwamba, iko siku, wataweza kushamiri kama “mtende wa Lebanon” hata kama hawajui saa wala siku. Watu wa sala, wanang’aa hata gizani, kwa sababu sala inakuwa ni taa ya kuangazia mapito yao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa sala inayosimikwa katika furaha, amani na utulivu wa ndani. Waamini wawe ni wasambazaji na mashuhuda wa Habari Njema, kwa kutambua kwamba, wao ni zawadi ya upendo wa Mungu. Uzuri wa Kazi ya Uumbaji, uwasaidie waamini kubeba vyema Misalaba ya mateso na mahangaiko yao, ha hii iwe ni sababu ya kumshukuru na kumtukuza Mwenyezi Mungu kwa ukuu na utakatifu wa Kazi ya Uumbaji. Binadamu ni watoto wa Mungu Muumbaji, wana uwezo wa kusoma chapa ya Kazi ya Uumbaji!

Kwa bahati mbaya sana, kwamba, Kazi ya Uumbaji inayoonesha: upendo, ukuu na utakatifu wa Mungu, mwanadamu amekuwa ni chanzo cha uharibifu wake. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Katekesi yake kuhusu Fumbo la Sala, Kazi ya Uumbaji kwa kuwataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni watu wa shukrani kwani shukrani ni sala nzuri sana mbele ya Mwenyezi Mungu!

Papa: Kazi ya Uumbaji
20 May 2020, 13:55