Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Mzunguko Mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Mzunguko Mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala 

Papa Francisko: Mzungumko Mpya wa Katekesi: Fumbo la Sala!

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 6 Mei 2020 ameanza mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Timayo, Bartimayo, yule kipofu ni kati ya watu wenye mvuto wa pekee sana katika fumbo la sala! Kristo anasikiliza na kujibu kilio cha waja wake. SALA!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sehemu ya Injili ya Marko inayomwonesha Timayo, Bartimayo, yule kipofu mwombaji aliyekuwa anaketi kando ya njia jinsi alivyopaaza sauti yake kuomba rehema aliposikia kwamba Yesu Mnazareti alikuwa anapita pale! Kilio chake kikasikika na watu wakamtia shime, akapata nafasi ya kuonana na kuzungumza na Kristo Yesu, aliyemponya kutokana na imani yake thabiti, na hatimaye, akaanza kumfuata njiani ndicho kilichokuwa kiini cha Fumbo la Sala. Rej. Mk. 10:46-52. Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 6 Mei 2020 ameanza mzungumko mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala, chemchemi ya imani na kilio kinachobubujika kutoka katika undani wa mwamini kwa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Timayo, Bartimayo, yule kipofu ni kati ya watu wenye mvuto wa pekee sana katika fumbo la sala!

Kama ilivyokuwa kwa akina Zakayo Mtoza ushuru, Mwana wa Timayo, Bartimayo aliposikia kwamba Yesu Mnazareti anapita karibu yake, alipiga kelele na kusema, “Mwana wa Daudi, Yesu, Unirehemu”. Sauti hii, iliwachefua baadhi ya watu, wakataka kumnyamazisha na kumshikisha adabu, lakini Bartimayo, akazidi kupaaza sauti akisema “Mwana wa Daudi, Yesu, Unirehemu”. Hiki ni kielelezo cha mwamini anayeomba rehema kutoka kwa Mwenyezi Mungu bila kuchoka. Bartimayo, kipofu anamtambua Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Daudi, yaani Masiha. Hii ni kiri ya imani kutoka kwa mtu ambaye alidharauriwa na watu wote pale njiani. Kristo Yesu, akakisikiliza kilio chake, kwa sababu aligusa sakafu ya moyo wake, kiasi hata cha kuwa tayari kumfungulia malango ya wokovu! Yule waliyetaka kumshikisha adabu, sasa “amepewa jeuri” anaitwa na Kristo Yesu ambaye anamuulizia kile alichotoka kutoka kwake!

Bartimayo anasema kwa uhakika kabisa “Mwalimu wangu, nataka nipate kuona”. Yesu anamponya kwa sababu ya imani yake thabiti. Katekisimu ya Kanisa Katoliki inasema, unyenyekevu ndio msingi wa sala na hali inayotakiwa kupokea kwa wingi paji la sala. Mwanadamu ni mwombaji mbele ya Mwenyezi Mungu ambaye huwa ni wa kwanza kuwatafuta waja wake na kuwaomba maji ya kunywa. Hii ni kwa sababu Mwenyezi Mungu anawaonea watu wake kiu, ili hata wao waweze kumwonea kiu zaidi. Imani anasema Baba Mtakatifu ni kilio cha ndani kama ilivyokuwa kwa Bartimayo, kipofu na kamwe hakiwezi kufumbwa mdomo na kunyamazishwa. Imani ni matumaini ya kuweza kuokolewa kutokana na shida zinazomwandama mwamini. Kamwe mwamini asikubali kuendelea kukaa katika mazoea, lazima apaaze sauti yake ya imani kumwelekea Mwenyezi Mungu.

Bartimayo kipofu ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa kwa udumifu katika sala na hatimaye, Kristo Yesu, akamsikiliza na kumponya upofu wake. Kutoka katika sakafu ya moyo wa mwanadamu kuna sauti inayolia kila kukicha! Hii ni sauti inayouliza maswali kuhusu maisha ya mwanadamu hapa ulimwenguni na hasa zaidi, pale mwanadamu anapoanza kutembea katika giza la maisha. Huu ndio mwanzo wa kupiga kelele na kusema, “Mwana wa Daudi, Yesu, Unirehemu”. Hiki ni kielelezo cha sala ya hali ya juu kabisa inayokimbilia na kuambata fumbo la huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Wakristo katika sala na maombi yao, wanaungana pia na waamini wa dini mbali mbali duniani. Mtakatifu Paulo anapowaandikia Warumi anasema, “Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa” Rum. 8: 22. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mzungumzo mpya wa Katekesi Kuhusu Fumbo la Sala kwa kusema, wasanii wamefanikiwa sana kumwonesha mwanadamu kuwa mwombaji mbele ya Mungu. Hii ni tafsiri nzuri sana ya maana ya binadamu yaani mwombaji mbele ya Mwenyezi Mungu.

Papa: Fumbo la Sala

 

06 May 2020, 14:34