Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote unapaswa kuwashirikisha watu wote kwa sababu madhara yake yanagusa na kuwatikisha wote pia! Baba Mtakatifu Francisko anasema, mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote unapaswa kuwashirikisha watu wote kwa sababu madhara yake yanagusa na kuwatikisha wote pia!  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Juma la Laudato si: Majadiliano ya kina na wote!

Papa Francisko anapenda kutoa mwaliko wa kupyaisha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuangalia ni jinsi gani mwanadamu anavyojenga maisha yake kwa siku za mbeleni. Ni majadiliano ambayo yanapaswa kuwashirikisha watu wote kwa sababu changamoto na athari za mabadiliko ya tabianchi zinachangiwa pia na kazi za binadamu, kumbe hata madhara yake yanawagusa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 24 Mei, 2020 kuadhimisha Juma la “Laudato si” kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya miaka mitano, tangu alipochapisha Waraka huu wa kitume ambao umekuwa ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anapenda kutoa wito na mwaliko wa kupyaisha majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuangalia ni jinsi gani mwanadamu anavyojenga maisha yake kwa siku za mbeleni. Ni majadiliano ambayo yanapaswa kuwashirikisha watu wote. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, changamoto na athari za mabadiliko ya tabianchi zinachangiwa pia na kazi za binadamu, kumbe, watu wote wanapaswa kujihusisha kwani madhara yake pia yanawagusa na kuwatikisa watu wote bila ubaguzi.

Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” uliozinduliwa hapo tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Kichwa cha Waraka huu kinapata chimbuko lake kutoka katika wimbo wa Mtakatifu Francisko wa Assisi kwa ajili ya viumbe na unaweza kutafsiriwa kuwa ni “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Baba Mtakatifu wakati wa Sala ya Malkia wa Mbingu, Jumapili tarehe 17 Mei 2020 amesema, maadhimisho haya yatakamilika Jumapili tarehe 24 Mei 2020, wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni. Katika kipindi hiki cha janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni wakati muafaka kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kujizatiti kikamilifu katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, tafakari pamoja na utekelezaji wa itifaki na maazimio yaliyofikiwa katika ngazi mbali mbali yatasaidia kujenga na kuimarisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Kumbukizi la Miaka 5 tangu Baba Mtakatifu alipochapisha Waraka wa “Laudato si” limegubikwa na hitilafu kubwa kutokana na maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 anasema Padre Benedict Ayodi, Meneja wa Mtandao wa Wanaharakati wa Kikatoliki Katika Utetezi wa Mazingira, “Global Catholic Climate Movement, GCCM. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote unakwenda sanjari na utekelezaji wa haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja ya kufanya wongofu wa kiekolojia mintarafu mtindo wa maisha, uzalishaji na ulaji ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Maadhimisho haya iwe ni nafasi ya kufanya rejea tena kwenye Mafundisho Jamii ya Kanisa pamoja na kuendelea kujikita katika fadhila za Kikristo yaani: Imani, Matumaini na Mapendo.

Ni wakati wa kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano wa Kitaifa na Kimataifa unaoongozwa na kauni auni. Maadhimisho haya iwe ni nafasi ya kupanda miti, kusafisha na kutunza mazingira. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka huu, anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote. Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa makini, Je, ni ulimwengu gani wanaopenda kuwaachia watoto wao kama urithi kwa siku za usoni?

Baba Mtakatifu kwa moyo wa unyenyekevu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Juma la “Laudato si” kama sehemu ya kumbu kumbu ya kimataifa ya Miaka mitano tangu kuchapishwa kwa Waraka huu wa kitume unaolenga utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Lengo ni kuweza kujibu kwa vitendo kipeo cha kiekolojia. Kamwe kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini hakiwezi kuendelea bila kusikilizwa!  Ni wakati wa kujizatiti zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa moyo shukrani, Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusherehekea kwa pamoja Juma la “Laudato si”. Katika kipindi cha miaka mitano tangu kuchapishwa kwa Waraka huu wa Kitume, Jumuiya na watu mbali mbali wameendelea kumwilisha waraka huu katika uhalisia wa maisha wakiwa na mwono wa ekolojia fungamani. Jambo la kusitikisha ni kuona kwamba, kasi ya uharibifu wa mazingira kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa sana, kiasi kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa vitendo ushauri unaotolewa na wanasayansi. Waraka huu wa kitume ni jibu makini linalotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ili kupambana na uchafuzi pamoja na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia kuchukua hatua madhubuti na endelevu katika maadhimisho ya Juma la “Laudato si” kuanzia tarehe 16 hadi tarehe 24 Mei, 2020. Huu ni muda muafaka wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, uliopitishwa Jijini Paris, nchini Ufaransa, Desemba 2015. Nchi nyingi duniani ziliahidi kudhibiti viwango vya ongezeko la joto duniani na kuhakikisha hakizidi nyuzi joto mbili kwa kipimo cha Selsiasi, na kuendeleza msukumo unaolenga kufikia nyuzi joto moja na nusu kwenye kipimo hicho. Utekelezaji wa Mkataba huu unafanyika katika ngazi ya kitaifa na kimataifa, kwa ajili ya ustawi na maendeleo mapana zaidi ya Jumuiya ya Kimataifa.

Waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wajitahidi kufanya tafakari ya kina katika mwanga wa ukweli na uwazi kuhusu vitendo vyao, tayari kujichimbia katika mchakato wa wongofu wa kiekolojia kwa kuchukua hatua madhubuti, ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika majanga na umaskini wa hali ya juu. Hii ni fursa pia kwa watu binafsi na Jumuiya mbali mbali kushirikisha maamuzi na hatua walizofikia kama sehemu ya mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Itakumbukwa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kutafuta njia zitakazosaidia kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Serikali mbali mbali katika Kipindi cha Mwaka 2020 zinatakiwa kuonesha sera na mbinu mkakati wa kupambana na mabadiliko ya tabianchi, kwa kuutekeleza kwa makini.

Laudato si

 

 

18 May 2020, 13:08