Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Msaidizi Eusebius Alfred Nzigilwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mpanda nchini Tanzania, kuanzia tarehe 13 Mei 2020. Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Msaidizi Eusebius Alfred Nzigilwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mpanda nchini Tanzania, kuanzia tarehe 13 Mei 2020. 

Askofu Eusebius Nzigilwa, Jimbo Katoliki la Mpanda, Tanzania

Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki Mpanda, alizaliwa tarehe 14 Agosti, 1966. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 23 Juni 1995. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, tarehe 28 Januari 2010 akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuwekwa wakfu tarehe 19 Machi 2010. Jimbo la Mpanda limekuwa wazi tangu tarehe 21 Desemba 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Askofu Msaidizi Eusebius Alfred Nzigilwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Mpanda, nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu Askofu Nzigilwa alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Saalam. Itakumbukwa kwamba, Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki Mpanda, alizaliwa tarehe 14 Agosti, 1966, Jijini Mwanza nchini Tanzania. Alipata masomo yake ya sekondari Seminari Ndogo ya Mtakatifu Petro, Jimbo Katoliki la Morogoro. Mnamo mwaka 1988 alishiriki katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria na baadaye, alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi, kwa masomo ya Falsafa na yale ya Taalimungu katika Seminari kuu ya Kipalapala, Jimbo kuu la Tabora.

Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 23 Juni, 1995 kama Padre wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kwa hakika mwaka 2020 anatarajia kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre. Kuanzia mwaka 1995-1996 alikuwa ni Padre mlezi, nyumba ya malezi, Jimbo kuu la Dar es Salaam, iliyoko Parokia ya Mtongani, Kunduchi. Aliwahi pia kuwa ni Mkurugenzi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu kuanzia Mwaka 1996 hadi Mwaka 1997. Baadaye Kardinali Polycarp Pengo alimteuwa kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Visiga, Jimbo kuu la Dar es Salaam kuanzia mwaka 1997-1999. Baadaye akaendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikojipatia shahada ya kwanza ya elimu.

Baada ya masomo, aliteuliwa kwa mara nyingine tena na Kardinali Pengo kuwa Gambera wa Seminari Ndogo ya Visiga, kuanzia 2003 hadi 2008 alipolazimika kwa mara nyingine tena kurudi Chuo kikuu cha Dar es Salaam kumalizia masomo yake katika Sayansi ya Elimu na hivyo kujipatia Shahada ya uzamili. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI tarehe 28 Januari 2010 akamteuwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kuwekwa wakfu tarehe 19 Machi 2010 wakati wa Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria na Msimamizi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam. Askofu Nzigilwa amekwisha hudumia watu wa Mungu akiwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza kama Askofu kwa muda wa miaka 10, yaani hadi raha!

Jimbo Katoliki la Mpanda, Tanzania limekuwa wazi kuanzia tarehe 21 Desemba 2018 baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuunda Jimbo kuu Jipya la Mbeya linalojumuisha: Jimbo Katoliki la Mbeya, Jimbo Katoliki la Iringa na Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu akamteua Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga kuwa Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Mbeya nchini Tanzania. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Nyaisonga ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, alikuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda. Mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania unasonga mbele!

Askofu Nzigilwa, Jimbo Katoliki Mpanda
13 May 2020, 11:58