Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Mfuko wa Dharura ili kusaidia juhudu za Makanisa mahalia kupambana na athari za Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Mfuko wa Dharura ili kusaidia juhudu za Makanisa mahalia kupambana na athari za Virusi vya Corona, COVID-19. 

Papa Francisko Ameanzisha Mfuko wa Dharura Dhidi ya Virusi vya COVID-19

Papa amechangia kiasi cha dola 750, 000 kama kianzio na anawaalika watu wa Mungu kuchangia katika Mfuko wa Dharura kupitia kwenye Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa katika nchi zao. Hiki ni kielelezo cha huruma na ukarimu unaojenga na kudumisha umoja na mshikamano na Makanisa mahalia katika kipindi hiki kigumu na chenye changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Mfuko wa Dharura unaosimamiwa na kuratibiwa na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa ajili ya kuwasaidia watu wa Mungu, ambao wameathirika sana kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Msaada huu utatolewa kwa Makanisa mahalia kupitia miundo mbinu pamoja na taasisi mbali mbali za Kanisa. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuanzisha Mfuko huu wa dharura kama sehemu ya vinasaba vya Kanisa katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu miongoni mwa watu wa Mataifa. Mama Kanisa, daima amekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa watu wa Mungu wanapokabiliwa na changamoto mbali mbali za maisha.

Takwimu zinaonesha kwamba, Barani Afrika kuna watawa zaidi ya 74, 000 na Mapadre ni 46, 000 wanaotekeleza dhamana na utume wao kati ya wagonjwa wanaohudumiwa kwenye Hospitali 7, 274, Zahanati 2, 346, bila kusahau nyumba za kutunzia wazee pamoja na vituo vya watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi. Kanisa Barani Afrika limeendelea kuwa mstari wa mbele kwa kuchangia kikamilifu katika sekta ya elimu inayotolewa kwa wanafunzi zaidi ya milioni 19, huku kukiwa na shule za msingi 45, 000. Kanisa limeendelea kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika huduma ya elimu na afya hususan katika maeneo ya vijijini, hata kama kwa sasa huduma hii inatolewa pia mijini kwa kusoma alama za nyakati.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso ya watu wanaoathirika kutokana na maambukizi makubwa vya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID, ili kuchangia kwa hali na mali katika Mfuko huu wa dharura, ili kukabiliana na changamoto zilizoko mbele ya Kanisa kwa sasa. Baba Mtakatifu amechangia kiasi cha dola 750, 000 kama kianzio na kuyaalika Makanisa, Taasisi na Watu binafsi kuchangia katika Mfuko wa Dharura kupitia kwenye Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa katika nchi zao. Hiki ni kielelezo makini cha huruma na ukarimu unaojenga na kudumisha umoja na mshikamano na Makanisa mahalia katika kipindi hiki kigumu na chenye changamoto pevu katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, anasema, Mfuko wa Dharura, pamoja na mambo mengine, unalenga kuyasaidia Makanisa mahalia kupambana na changamoto ambazo zimesababishwa na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kanisa kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kwa kutumia mtandao wake wa Injili ya upendo na huduma kwa watu wa Mungu, linapenda kuwahakikishia watu wote kwamba, liko pamoja na wale wote wanaopambana dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Kanisa linao mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hili ndilo lengo kuu la Baba Mtakatifu Francisko kuanzisha Mfuko wa Dharura ili kusaidia Makanisa mahalia ambayo yameguswa na kutikiswa sana na Virusi vya Corona, COVID-19. Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ni chombo madhubuti cha huduma kwa Majimbo 1, 110 yaliyoenea Barani Afrika, Asia, Oceania na Amerika ya Kusini.

Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa yametakiwa kujipanga vyema ili kuhakikisha kwamba, watu walioguswa na kutikiswa na Virusi vya Corona katika nchi zao wanapata msaada wa hali na mali kama njia ya kuunga mkono jitihada zinazoendelea kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki cha janga la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mchango kutoka kwa watu binafsi na taasisi mbali mbali unaweza kutumwa kwenye akaunti ifuatayo:

 

IT84F0200805075000102456047 (SWIFT UNCRITMM) for: Amministrazione Pontificie Opere Missionarie, indicating: Fund Corona-Virus.

Papa: Mfuko wa Dharura
07 April 2020, 12:58