Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2020 yanaadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo! Lakini kwa Mwaka huu, maadhimisho haya yanakabiliwa na changamoto kubwa! Maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2020 yanaadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo! Lakini kwa Mwaka huu, maadhimisho haya yanakabiliwa na changamoto kubwa!  (AFP or licensors)

Maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni, Ngazi ya Kijimbo kwa Mwaka 2020

Mwaka 2020 Siku ya Vijana Ulimwenguni inaadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo, Jumapili ya Matawi, mwanzo wa maadhimisho ya Juma kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya: Mateso, kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Maadhimisho ya Siku ya XXXVII Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2022 yatafanyika Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno! Vijana na Imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni yamekuwa ni alama ya kinabii katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana wa kizazi kipya wanaendeleza hija ya maadhimisho haya ambayo ni amana na urithi mkubwa uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, kama jibu muafaka la kukabiliana na changamoto katika maisha na utume wa vijana wa kizazi kipya;  ili kuwapatia matumaini yanayofumbatwa katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Hii ni alama ya ukaribu unaofumbatwa katika majadiliano na urafiki wa kweli ili vijana waweze kuwa ni alama ya matumaini na chachu ya mabadiliko katika ulimwengu mamboleo. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ni tukio ambalo linaendelea kupyaisha maisha na utume wa Kanisa, kwa kuona tena ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya vijana wa kizazi kipya. Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2020 Siku ya Vijana Ulimwenguni inaadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo, Jumapili ya Matawi, mwanzo wa maadhimisho ya Juma kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya: Mateso, kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Maadhimisho ya Siku ya XXXVII Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2022 yatafanyika Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mariamu akaondoka akaenda kwa haraka”

Kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa Mwaka 2020 ni “Kijana, nakuambia: Inuka!” Lk. 7:14. Baba Mtakatifu aliweka mkwaju kwenye ujumbe huu, hapo tarehe 11 Februari 2020 wakati wa Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Huu ni mwanzo wa tafakari ya miaka mitatu kuanzia mwaka 2019 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni huko nchini Panama hadi mwaka 2022, panapo majaliwa, vijana “watakapotia timu” Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno. “Inuka” ndilo neno linalobeba uzito wa juu kabisa katika ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa sababu huu ni mwaliko wa: kufufuka, kuamka na kupyaisha maisha katika mwanga wa Injili. Vijana wanahamasishwa kujitaabisha kusoma sehemu hii ya Injili inayomwonesha Kristo Yesu akimfufua yule kijana wa Naini, yaani sehemu ya Injili ya Lk. 7:11-17. Tafakari hii iwasaidie vijana kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, ili kumfuasa Kristo Yesu.

Injili haitaji jina la yule kijana aliyefufuliwa na Yesu pale mjini Naini na hapo kila kijana anapaswa kujiweka katika nafasi hii, ili kuweza kuupokea wito na mwaliko huu. Kuteleza na kuanguka ni jambo la kawaida katika maisha ya binadamu; kusimama na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu ni mwanzo wa toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anatoa mwaliko huu kwa kila mtu kusimama tena na kuanza kupyaisha safari ya maisha yake, kama kielelezo cha kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anasema, hatua ya kwanza ni kukubali kusimama. Wosia wa kitume kutoka kwa Baba Francisko “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”, unawakumbusha vijana kwamba, Kristo Yesu anaishi na ni matumaini na uzuri wa ujana katika ulimwengu mamboleo. Yale yote yanayoguswa na Kristo Yesu yanapyaishwa na kupata uzima mpya! Ujumbe mahususi kwa vijana ni kwamba, “Kristo anaishi! Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwahamasisha vijana kuwa ni wadau wakuu katika mchakato wa utekelezaji wa sera na mikakati ya utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.

Kuna uhusiano wa pekee kati ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana na Maadhimisho ya Siku za Vijana Ulimwenguni. Lengo ni kutaka kuhakikisha kwamba, vijana wanajitahidi katika maisha yao, kumwilisha Wosia wa kitume “Christus vivit” yaani “Kristo anaishi”. Msalaba wa Siku ya Vijana Ulimwenguni: Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, tarehe 22 Aprili 1984 mara tu baada ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Ukombozi, yaani kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, aliwakabidhi vijana Msalaba Mtakatifu, alama ya Mwaka Mtakatifu, lakini zaidi kama kielelezo cha upendo wenye huruma unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Ni kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo ameukomboa ulimwengu. Msalaba huu umezungushwa na vijana sehemu mbali mbali za dunia katika kipindi cha Miaka XXXV iliyopita.

Msalaba wa Vijana tangu Mwaka 1984 unahifadhiwa kwenye Kituo cha Vijana Kimataifa cha San Lorenzo, kilichoko mjini Roma. Msalaba huu umetembezwa sehemu mbali mbali za dunia sanjari na Sanamu ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, iliyounganishwa kwenye hija ya Msalaba wa Vijana kwa mara ya kwanza kunako Mwaka 2003. Msalaba wa Vijana umekuwa ni kielelezo cha sala, dhamana ya uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni kielelezo cha majadiliano ya kidini na kiekumene kuhusu imani ya Kanisa Katoliki miongoni mwa vijana wa kizazi kipya na watu wenye mapenzi mema. Msalaba umekuwa ni amana ya imani na ushuhuda wa vijana kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; ni kielelezo cha imani, matumaini na mapendo kwa wale waliokata tamaa.

Siku ya Vijana 2020

 

02 April 2020, 07:18