Tafuta

Vatican News
Kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Mei Mosi, 2020: Papa Francisko anawakabidhi wafanyakazi wote chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, ili awaombee! Kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Mei Mosi, 2020: Papa Francisko anawakabidhi wafanyakazi wote chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, ili awaombee!  (AFP or licensors)

Kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, Mei Mosi 2020!

Mei Mosi, 2020 ni Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani sanjari na Kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi. Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wafanyakazi wote chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, ili aweze kuwaombea huruma ya Mungu, wale wote walioguswa na kutikishwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Hii ni kumbukumbu ya mauaji ya halaiki yaliyotokea kunako mwaka 1886 katika viwanja vya Haymarket j Chicago, nchini Marekani. Polisi walikuwa wakitawanya mkusanyiko wa wafanyakazi wakati wa mgomo wa kupinga masaa nane ya kazi ambapo mtu asiyejulikana aliwarushia askari bomu. Polisi waliwalirushia risasi wafanyakazi hao na kuwaua wanne. Kanisa kwa upande wake linaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi. Kanisa linatambua na kuthamini umuhimu wa kazi kama wajibu na utimilifu wa maisha ya mwanadamu sanjari na ushiriki wa mwanadamu katika kuitiisha dunia, ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Huu ni mwendelezo wa ushiriki wa mwanadamu katika kazi ya uumbaji na mchango katika kazi ya ukombozi. Kutokana na ugumu wa dhambi ya asili, Kristo Yesu alitoa mwelekeo mpya wa kazi, kuwa ni kielelezo cha ukombozi. Kielelezo cha kazi na utume huu, ni mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu!

Mama Kanisa katika huruma na upendo wake usiokuwa na kifani, ili apate kuwalinda na kuwatuliza wafanyakazi, Papa Pio XII kunako mwaka 1955 akamteua Mtakatifu Yosefu, kuwa tegemeo, mfano na mwombezi wa wafanyakazi wote duniani. Mkazo kwa waamini ni kuhakikisha kwamba, wanafanya kazi kwa juhudi na maarifa, ili kuweza kujipatia: mali na mapato halali; watambue na kuheshimu kazi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanatumia rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Mtakatifu Yosefu, Mfanyakazi, awasaidie waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwaelekeza watu kwa Kristo Yesu. Awalinde na kuwasaidia wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, awaombee wale wote ambao wamepoteza fursa za ajira na kazi au ambao bado wanachakarika kutafuta fursa za kazi!

Wafanyakazi waendelee kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Yosefu, aliyesimama kidete kuitunza na kuitegemeza Familia Takatifu ya Nazareti hasa katika nyakati hizi ngumu za Janga kubwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano, tarehe 29 Aprili 2020, amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Mei Mosi, 2020 ni Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani sanjari na Kumbukumbu ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi. Baba Mtakatifu amewaweka wote chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi, ili aweze kuwaombea huruma ya Mungu, wale wote walioguswa na kutikishwa na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Awaombee wale wote waliopoteza fursa za ajira kutokana na ugonjwa huu. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, awaangalie watoto wake wote wanaomkimbilia wakiomba msaada, watu wote wahamasishwe na wawe na moyo wa kuwasaidia watu wote wanaoteseka kutokana na ukosefu wa fursa za ajira.

Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi
30 April 2020, 12:30