Tafuta

Vatican News
Papa Francisko: Ibada ya Misa Takatifu: Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu na Sr. Faustina kutangazwa kuwa Mtakatifu. Papa Francisko: Ibada ya Misa Takatifu: Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu na Sr. Faustina kutangazwa kuwa Mtakatifu.  (Evaldas Lasys)

Papa: Kumbu kumbu ya Miaka 20 ya Jumapili ya Huruma ya Mungu:

Papa Francisko Jumapili tarehe 19 Aprili 2020 ataadhimisha Ibada ya Misa kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Maria Faustina Kowalska alipotangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. Mama Kanisa anaadhimisha pia kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu, chemchemi ya neema na baraka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Huruma ya Mungu ni tema ambayo ni kielelezo cha maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huruma na msamaha ni tunu msingi ambazo Baba Mtakatifu anapenda kuona zikimwilishwa katika maisha ya watu wa Mungu. Huruma ya Mungu ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu na kwamba, daima binadamu wanapaswa kuhurumiana na kusameheana! Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu, hapo tarehe 19 Aprili 2020 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la “Santo Spirito in Sassia”, lililoko mjini Roma, hatua chache kutoka Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kanisa ambalo lina Ibada ya pekee kwa Huruma ya Mungu. Ibada hii itaadhimishwa kwa faragha na baada ya maadhimisho, Baba Mtakatifu atawaongoza waamini kusali Sala ya Malkia wa Mbingu “Regina Coeli” inayotumiwa na Mama Kanisa katika Kipindi hiki cha Sherehe ya Pasaka.

Ibada hii ya Misa Takatifu inatarajiwa kuanza rasmi saa 5:00 kwa saa za Ulaya sawa na Saa 6:00 mchana kwa Saa za Afrika Mashariki. Ibada itarushwa moja kwa moja na vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican na kutakuwepo na tafsiri mubashara katika lugha ya: Kiitalia, Kifaransa, Kiingereza, Kijerumani, Kihispania, Kireno na Kiarabu. Maadhimisho haya ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 20 tangu Mtakatifu Maria Faustina Kowalska alipotangazwa kuwa Mtakatifu na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 30 Aprili 2000. Mama Kanisa anaadhimisha pia Kumbu kumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu inayojulikana pia kama "Domenica in albis". Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watakatifu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kinga na kimbilio la maskini na wadhambi. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili waweze kupata msamaha wa dhambi. Huruma ya Mungu inazidi uelewa, maarifa na ufahamu wa akili ya binadamu.

Ilikuwa ni tarehe 23 Aprili 1995, Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea na kusali kwenye Kanisa la “Santo Spirito in Sassia”. Hapa ni mahali ambapo mwaka 1994 Kardinali Camillo Ruini, Makamu wa Askofu Jimbo kuu la Roma, wakati ule alikuwa ameanzisha Kituo cha Tasaufi ya Huruma ya Mungu. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Mtakatifu Yohane Paulo II akabariki Picha ya Huruma ya Mungu inayoheshimiwa Kanisani humo. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II tangu ujana wake, alikuwa na Ibada ya Huruma ya Mungu na hatima ya Ibada hii ni hapo tarehe 2 Aprili 2005, alipofariki dunia. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI hapo Mei Mosi, 2011 akamtangaza kuwa Mwenyeheri na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Aprili 2014 akamtangaza kuwa Mtakatifu pamoja na Papa Yohane wa XXIII.

Kanisa la “Santo Spirito in Sassia” limeungana na Hospitali ya “Santo Spirito in Sassia” ambayo imeendelea kujipambanua kuwa ni Kituo Kikuu cha Injili ya Upendo kwa wakimbizi, wahamiaji, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hapa ni mahali ambapo “watu wasiokuwa na utambulisho” wanapata huduma ya tiba. Kwa wale wanaoishiriki Ibada ya Huruma ya Mungu kwa moyo wa ibada na uchaji wa Mungu wanaweza kupata rehema kamili inayotolewa katika amana na utajiri wa maisha na utume wa Mama Kanisa. Mafundisho ya imani na ibada ya rehema katika Kanisa yameunganika kabisa na matunda ya Sakramenti ya Upatanisho. Kanisa linafundisha kwamba, Rehema kamili ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu za muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata baada ya kutimiza mashari yaliyotolewa na Mama Kanisa, kwa tendo la Kanisa ambalo likiwa ni mgawaji wa ukombozi hutumia kwa mamlaka yake hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya watakatifu wake.

Rehema imegawanyika katika sehemu kuu mbili: Rehema Kamili au Rehema ya Muda ni kutokana kwamba inaondoa au sehemu au adhabu yote kabisa ya muda inayotakiwa kwa sababu ya dhambi. Kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu wake kama atatimiza yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa. Pili, apokee Sakramenti ya Upatanisho. Tatu, apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili. Nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu. Mwishoni atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema Kamili.

Papa: Miaka 20 Jumapili Huruma ya Mungu
16 April 2020, 14:03