Tafuta

Vatican News
Jumapili tarehe 19 Aprili 2020 Kanisa linaadhimisha Jumapili ya Huruma ya Mungu "Divina Misericordia". Miaka 2020 tangu kuanzishwa kwake na Miaka 20 ya Utakatifu wa Sr. Maria Faustina Jumapili tarehe 19 Aprili 2020 Kanisa linaadhimisha Jumapili ya Huruma ya Mungu "Divina Misericordia". Miaka 2020 tangu kuanzishwa kwake na Miaka 20 ya Utakatifu wa Sr. Maria Faustina 

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Chemchemi: Upendo, Huruma na Msamaha

Adhimisho la Jumapili ya huruma ya Mungu, linapata chimbuko lake wakati wa adhimisho la Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Huruma ya Mungu inakita mizizi yake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jumapili ya Huruma ya Mungu mwaka Mwaka 2020 ni sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya miaka ishirini tangu kuanzishwa kwa Jumapili ya Huruma ya Mungu na miaka ishirini tangu Maria Faustina Kowalska alipotangazwa kuwa Mtakatifu na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 30 Aprili 2000. Huruma na upendo wa Mungu unabubujika kutoka katika Madonda yake Matakatifu, ambamo mwamini anapoyagusa kutoka katika undani wa maisha yake, anaweza kukiri kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Tomaso, Bwana wangu na Mungu wangu! Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa kitume “Dives in misericordia” yaani “Tajiri wa huruma” anakazia mambo makuu matatu: upendo wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu; huduma makini kwa maskini, wadhambi na wale wote wanaoteseka: kiroho na kimwili.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya haki inayofikia utimilifu wake katika msamaha kwa kutambua kwamba, upendo wa Mungu una nguvu zaidi kushinda dhambi na ubaya wa moyo unaoendelea kumwandama mwanadamu katika historia na maisha yake. Kimsingi Fumbo zima la Pasaka ni chemchemi ya huruma ya Mungu. Adhimisho la Jumapili ya huruma ya Mungu, linapata chimbuko lake wakati wa adhimisho la Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo. Huruma ya Mungu inakita mizizi yake katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo! Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kinga na kimbilio la maskini na wadhambi. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili waweze kupata msamaha wa dhambi. Huruma ya Mungu inazidi uelewa, maarifa na ufahamu wa akili ya binadamu

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume “Misericordia vultus” yaani “Uso wa huruma” anasema, Kristo Yesu ni ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu, muhtasari wa imani ya Kanisa ambayo imefunuliwa na Kristo Yesu kwa njia ya: mafundisho, matendo na nafsi yake. Fumbo la huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, utulivu na amani ya ndani. Huruma ni ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Kusamehe makosa ni kielelezo dhahiri cha upendo wenye huruma. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa mwanadamu. Anajisikia kuwajibika, kwani Mwenyezi Mungu anataka kuwaona watoto wake wakiwa wamesheheni furaha na amani tele.

Maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu kwa mwaka 2020 yana mwelekeo wa pekee kabisa katika maisha ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia! Hiki ni kipindi cha simanzi na majonzi; watu wengi wamekata tamaa kwani hawajui hatima ya maisha yao kwa siku za usoni kutokana na athari kubwa zinazoendelea kujitokeza kutokana na homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Viongozi na wakuu wa Makanisa katika Nchi Takatifu wanasema, Fumbo la Ufufuko ni kiini cha imani na matumaini ya Kanisa. Hili ni tukio ambalo linapaswa kutangazwa na kushuhudiwa katika uhalisia wa maisha kama kielelezo cha imani tendaji! Viongozi wa Makanisa wanawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini.

Ni wakati muafaka kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupambana na mifumo yote ya ukandamizaji, nyanyaso na vurugu; ubaguzi pamoja na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Huu ni wakati wa kukuza na kudumisha: huruma, upendo na mshikamano wa dhati; kwa kuwahudumia na kuwafariji, wale wote wanao omboleza vifo vya ndugu, jamaa na marafiki zao. Ni muda muafaka wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa faraja kutoka kwa Kristo Yesu. Dhamana na utume wa Wakristo katika kipeo hiki cha maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni kuwa ni vyombo na mashuhuda wa sala, faraja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu, kielelezo makini cha nguvu ya Mungu inayookoa!

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, licha ya changamoto kubwa zinazoendelea kujitokeza nchini Italia kutokana na athari za maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limeamua kuchangia Euro milioni 6 ili kusaidia Makanisa mahalia Barani Afrika na Amerika ya Kusini katika mapambano yake dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Fedha hii inalenga kusaidia mafunzo kazini kwa ajili ya madaktari na manesi wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Fedha hii pia itatumika kwa ajili ya kununulia vifaa tiba vinavyohitajika kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ibada ya Upatanisho ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia huruma, upendo na amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, waamini wanakirimiwa tena maisha mapya baada ya kuanguka dhambini na kupoteza ile neema ya utakaso waliyopokea wakati walipokuwa wanapokea Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya upatanisho, Kanisa linazidi kukua na kupanuka, kwa kumfuasa Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu asiyekuwa na mawaa. Huu ni mwaliko wa kujitakasa kwa kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu kuzungumza kutoka katika undani wa maisha ya watu, ili kweli wakleri waendelee kuwa ni vyombo vya huruma na upatanisho kati ya Mungu na watu wake. Katika maisha na utume wa kipadre, Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza! Mtakatifu Toma kwa kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, akatubu, akaongoka na kuwa Shuhuda wa Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma ya Mungu.

Fumbo la Huruma ya Mungu limekaziwa sana na Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Francisko akaliwekea mikakati ya kichungaji, kwa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji pamoja na kuanzisha Siku ya Maskini Duniani, inayoadhimishwa, Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa! Katika kipindi hiki cha kipeo cha homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Kanisa linaendelea kukazia umuhimu wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Ni wakati muafaka wa kugundua tena: Ukuu, ukweli, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kwa kudumisha mafungano, ili kweli mahusiano ya wanandoa yaendelee kuziimarisha familia, Kanisa dogo la nyumbani.

Baba Mtakatifu anasema, Kristo Bwana, huwajia wanandoa Wakristo katika Sakramenti ya Ndoa na kubaki nao, katika tafakari ya Neno la Mungu, Sala na katika hali zote za maisha. Familia zijijengee fadhila ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati; kwa kusamehe na kusahau, vingine, familia zitageuka kuwa ni uwanja wa masumbwi na hii imeanza kujitokeza kwenye baadhi ya familia! Kipindi hiki cha ukame wa maisha ya kiroho, kuna haja ya kuibua sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayokita mizizi yake katika kipaji cha ubunifu! Kwa upande mwingine, watawa wanapaswa kuyaangalia ya mbeleni kwa imani na matumaini; kwa kuendelea kujikita pia katika kipaji cha ubunifu, kwani Kristo Mfufuka ni chemchemi ya faraja na matumaini kwa waja wake. Hii ni nafasi ya kudumisha upendo kwa Mungu na jirani; kwa kujisasaka kwa ajili ya huduma kwa wazee, wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Huruma ya Mungu
18 April 2020, 12:55