Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema, Mama Dunia ni Injili ya Kazi ya Uumbaji, mwaliko wa kuamsha na kupyaisha Injili ya Kazi ya Uumbaji katika ulimwengu mamboleo! Papa Francisko anasema, Mama Dunia ni Injili ya Kazi ya Uumbaji, mwaliko wa kuamsha na kupyaisha Injili ya Kazi ya Uumbaji katika ulimwengu mamboleo!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Jubilei ya Miaka 50 ya Maadhimisho ya Mama Dunia

Kwa Wakristo anasema Baba Mtakatifu, Mama Dunia ni Injili ya Kazi ya Uumbaji inayodhihirisha nguvu ya uumbaji katika mchakato wa kumuumba mwanadamu na viumbe vyote hai, ili kuenzi maisha ya binadamu. Maandiko Matakatifu yanahitimisha kazi ya Uumbaji kwa kusema “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana”. Mwa. 1:31! Kulinda na kutunza mazingira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 22 Aprili 1970, miaka 50 iliyopita, wananchi wa Marekani walipofanya maandamano makubwa kudai sera makini za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Jumuiya ya Kimataifa ikatambua umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote! Utunzaji bora wa mzingira ni sehemu ya utekelezaji wa kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemdhaminisha mwanadamu tangu kuumbwa kwa Bustani ya Edeni ili ailime na kuitunza. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano, tarehe 22 Aprili 2020 ameungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia. Hii ni fursa ya kupyaisha tena upendo katika mchakato wa utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kwa kutoa kipaumbele kwa watu wanyonge ndani ya familia kubwa ya binadamu! Huu ni muda wa kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo kama ambavyo inajidhihirisha katika mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. 

Baba Mtakatifu Francisko, katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” unabeba dhamana kubwa ya utunzaji wa mazingira kwani ni suala linalomwathiri binadamu moja kwa moja kwa sababu lina uhusiano na maana halisi ya safari ya maisha yake hapa duniani! Maandiko Matakatifu yanasema, Mwenyezi Mungu alimfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. Kumbe, watu wanaishi katika mazingira nyumba ya wote kama familia ya binadamu katika utofauti wao wa kibaiolojia na viumbe wengine. Binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, “Imago Dei”, kumbe, wanahimizwa kutunza na kuheshimu viumbe vyote hai; sanjari na kurutubisha huruma na upendo kwa jirani zao ambao ni wanyonge zaidi, kama sehemu ya mwitikio wa upendo wa Mungu kwa binadamu uliofunuliwa na Mwanae wa pekee Kristo Yesu. Kutokana na ubinafsi wa kupindukia, watu wamepunguza uwajibikaji wao kama walinzi na watunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Inatosha kuona kuwa mazingira yanaingia kwenye uharibifu mkubwa.

Shughuli mbali mbali za binadamu zimepelekea uchafuzi mkubwa wa mazingira, hali inayohatarisha maisha ya binadamu. Ni kutokana na muktadha huu, kumekuwepo na makundi makubwa ya wanaharakati wa mazingira, kitaifa na kimataifa ili kuamsha tena dhamiri nyofu juu ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaunga mkono jitihada zote hizi na kwamba, kuna haja kwa vijana wa kizazi kipya kujitosa tena barabarani ili kuwafundisha walimwengu yale mambo msingi, kwa kutambua kwamba, kesho ya binadamu iko mashakani, ikiwa kama ataendelea kuharibu mazingira yanayompatia jeuri ya kuishi ulimwenguni! Binadamu ameshindwa kutunza mazingira, bustani nyumba ya wote pamoja na kuwatunza jirani zake. Kwa hakika binadamu ametenda dhambi dhidi ya mazingira nyumba ya wote, dhidi ya jirani zake na zaidi sana dhidi ya Muumbaji, Baba Mwema anayemwangalia kila mtu na anayetaka watu waishi kwa umoja ili wapate ustawi na maendeleo. Kumbe, kuna haja ya kurejesha tena mahusiano kwa kuangalia kwa dhati kabisa mazingira, nyumba ya wote. Kamwe mazingira si hifadhi ya rasilimali ya dunia inayoweza kutumika kadiri watu wanavyotaka.

Kwa Wakristo anasema Baba Mtakatifu, Mama Dunia ni Injili ya Kazi ya Uumbaji inayodhihirisha nguvu ya uumbaji katika mchakato wa kumuumba mwanadamu na viumbe vyote hai, ili kuenzi maisha ya binadamu. Maandiko Matakatifu yanahitimisha kazi ya Uumbaji kwa kusema “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana”. Mwa. 1:31. Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia, Jumuiya ya Kimataifa inapewa changamoto ya kugundua tena utakatifu wa kazi ya uumbaji, ili kuweza kuheshimu mazingira, nyumba ya wote na pia ni nyumba ya Mwenyezi Mungu. Hii iwe ni changamoto ya kuwasukuma wananchi kutambua kwamba, wanaishi kwenye nchi takatifu. Ni fursa makini kwa mwanadamu kuamsha tena ndani mwake tafakari ya uzuri ambao Mwenyezi Mungu amemwekea ndani mwake.

Unabii wa tafakari hii ni ushuhuda unaopata chimbuko lake kutoka kwa watu mahalia, wanaoendelea kuwafundisha walimwengu kwamba, ili kutunza mazingira nyumba ya wote, kuna haja ya kulinda, kupenda na kuyaheshimu! Mwelekeo huu wa maisha unahitaji wongofu wa kiekolojia unayomwilishwa katika matendo halisi. Kama familia moja inayotegemeana, inahitaji sera na mikakati ya pamoja ili kudhibiti mambo yanayo sababisha uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Kutegemeana kunawalazimu watu kuwa na mtazamo wa ulimwengu mmoja wenye mpango wa pamoja.Jumuiya ya Kimataifa inatambua na kuthamini umuhimu wa kushirikiana kama Jumuiya ili kulinda mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwataka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika mchakato utakaowaelekeza katika matukio makuu mawili. Moja ni Mkutano wa Baianuai (biodiversity) unaoratajiwa kuadhimishwa huko Kunming, China pamoja na Mkutano wa 26 wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP26 huko Glasgow, nchini Uingereza.

Kwa sasa Umoja wa Mataifa umetangaza kuahirishwa kwa Mkutano wa 26 wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP26 uliokuwa ufanyike baadaye mwaka huu kutokana na janga la kimataifa la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kipaumbele cha kwanza kwa sasa ni kulinda uhai wa binadamu. Baba Mtakatifu anapenda kutumia fursa hii tena kuwahamasisha wanaharakati na watetezi wa mazingira nyumba ya wote, kuandaa matukio muhimu katika ngazi ya watu mahalia, kitaifa na kimataifa, yatakayowahusisha watu mbali mbali kwa sababu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia yamepata chimbuko lake kutoka kwa watu wa kawaida. Kila mtu kadiri ya uwezo na nafasi yake, anaweza kuchangia katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mwelekeo huu ni nafasi ya kuondokana na mawazo mgando kwamba, jitihada zote hizi haziendi kuubadilisha ulimwengu. Lakini zinainufaisha jamii pasi ya watu wenyewe kutambua kwani zinahitaji wema ambao japo hauonekani huzidi kuenea.

Baba Mtakatifu amehitimisha katekesi yake ambayo imekita ujumbe wake katika Jubilei ya Miaka 50 tangu Jumuiya ya Kimataifa ilipoanzisha Siku ya Kimataifa ya Mama Dunia, kwa kuwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema, katika kipindi cha Pasaka kuendelea kujizatiti katika mchakato wa kupyaisha upendo kwa zawadi kubwa ya Mama Dunia, nyumba ya wote, kwa kuwahudumia watu wote wa familia kubwa ya binadamu. Wote kwa pamoja kama ndugu, wamwombe Mwenyezi Mungu ili aweze kuwashushia Roho wake Mtakatifu ili aweze kuufanya upya uso wa nchi.

Papa: Mama Dunia 50 Yrs.

 

22 April 2020, 13:34