Tafuta

Vatican News
Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Aprili 2020: Mchakato wa kujinasua kutoka kwenye mtandao wa matumizi haramu ya dawa za kulevya! Nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Aprili 2020: Mchakato wa kujinasua kutoka kwenye mtandao wa matumizi haramu ya dawa za kulevya!  (AFP or licensors)

Nia za Baba Mtakatifu Mwezi Aprili 2020: Athari za Dawa za Kulevya!

Papa Francisko anawaalika watu wa Mungu kujiwekea mikakati ya kujikwamua kutoka katika matumizi haramu ya dawa za kulevya. Mchakato huu wa kuwakomboa wale waliozamishwa kwenye matumizi haramu ya dawa za kulevya usimikwe kwenye Injili ya huruma ya Mungu. Anasali ili waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya waweze kusaidiwa na kusindikizwa vyema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Takwimu zinaonesha kwamba, waathirika wakuu wa matumizi haramu ya dawa za kulevya ni watoto na vijana wenye umri kuanzia miaka 15-35 na kwamba, madhara yake ni makubwa sana kiafya kwani yanachangia kuenea kwa magonjwa kama Ukimwi na Kifua kiuu na hivyo kudidimiza nguvu kazi ya taifa. Vijana wengi wamekuwa ni mzigo mkubwa kwa familia, jamii na taifa katika ujumla wake, kutokana na vitendo vya kihalifu na hivyo kupelekea kuchafua sifa njema ya familia na jamii zao. Vijana na watoto wadogo wamekuwa wakitumiwa kama wakala katika mchakato wa kukuza na kudumisha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani. Kuna baadhi ya Serikali duniani zinataka kuhalalisha matumizi ya baadhi ya dawa za kulevya kama njia ya kupambana na biashara haramu ya dawa hizi. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Aprili 2020 zinazosambazwa kwa njia ya video na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiwekea sera na mikakati ya kujikwamua kutoka katika matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Mchakato huu wa kuwakomboa wale waliozamishwa kwenye matumizi haramu ya dawa za kulevya usimikwe kwenye Injili ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasali ili kwamba, waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya waweze kusaidiwa na kusindikizwa vyema, ili hatimaye, waweze kujikwamua kutoka katika utumwa huu, unaodhalilisha utu na heshima yao. Baba Mtakatifu anasema, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile: kazi za suluba kwa watoto wadogo, biashara ya ngono na picha za utupu, biashara haramu ya viungo vya binadamu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni uhalifu dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kamari na upatu ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha ya watu na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu na hivyo kuwa ni chachu ya rushwa, ufisadi na kizingiti kikubwa, katika mchakato mzima wa maendeleo fungamani ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Lengo kuu zaidi ni kuendeleza mchakato wa kuwekeza katika elimu, kuzuia, kutibu na pale inapowezekana kufuta kabisa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya na utumwa mamboleo, badala ya kuendelea na mtindo wa sasa wa kuwatia pingu wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya!

Yote hii ni minyororo inayoweza kumtumbukiza mtu katika mahangaiko makubwa kiasi hata cha kuweza kumzamisha katika ugonjwa wa sonona na hatimaye, kuteteleka kwa afya ya akili! Matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake ni kikwazo kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Matumizi haramu ya dawa za kulevya, michezo ya kamari na upatu, ni mambo ambayo yanapekenyua uhuru na utu wa binadamu, kikwazo kikuu cha uhuru wa kweli, maendeleo endelevu na fungamani. Hizi ni dalili za utepetevu katika mchakato wa malezi, makuzi na ukomavu wa mtu! Janga la matumizi haramu ya dawa za kulevya linachagizwa na wafanyabiashara wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka, kiasi cha kushindwa kuona madhara yake katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Hiki ni kielelezo cha hali ya juu sana cha ubinafsi katika ulimwengu mamboleo. Matumizi haramu ya dawa za kulevya ni donda wazi katika jamii nyingi na madhara yake yanajionesha hata kwenye familia na jamii husika!

Wadau mbali mbali wa huduma kwa watu wanapaswa kuunganisha nguvu ili kufanya upembuzi yakinifu kuhusu janga la matumizi haramu ya dawa za kulevya, ili kuibua mbinu mkakati wa kupambana nalo, kwa njia ya kinga na tiba, ili kulinda na kudumisha: utu na heshima ya binadamu! Vijana wanapaswa kutambua kwamba, dhamana ya maisha, utu na heshima yao viko viganjani mwao, kumbe, wanawajibika kulinda na kudumisha maisha yao. Wimbi kubwa la matumizi haramu ya dawa za kulevya kimataifa linatishia amani, usalama, ustawi na maendeleo fungamani ya watu wa Mungu. Matumizi haramu ya mitandao ya kijamii yana madhara yake pia kwa mwanadamu kama ilivyo michezo ya kamari, upatu na ukahaba. Changamoto zote hizi zimejadiliwa mintarafu mitazamo ya kitaalimungu, sayansi ya binadamu, kanuni maadili na utu wema pamoja na kubainisha mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, ili kuwakomboa waathirika kutoka katika “jangwa la utupu kimaadili na kisaikolojia” na upweke hasi unaoweza kuwatumbukiza watu katika ugonjwa wa sonona! Elimu na malezi makini yanaweza kuwasaidia waathirika kurejea tena katika maisha yao ya kawaida, ikiwa kama watafanya kazi ya ziada!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican akichangia katika mada hii amesikitika kusema kwamba, madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa miaka mingi hayakupewa msisitizo wa pekee na hivyo kuonekana kuwa ni jambo la mpito! Lakini madhara yake kwa sasa ni makubwa kiasi cha kutishia maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Mwanzoni kabisa, mambo haya yanaonekana kuwa kama ni jambo la kawaida! Si ajabu kuona watu wakicheza kamari na upatu; wakitumia interneti na mitandao ya kijamii; wakifanya manunuzi makubwa hata bila sababu msingi; watu kutumbukia katika ukahaba na picha za utupu na hata pengine kuwa na matumizi haramu ya simu za viganjani! Mambo haya badala ya kuwa ni sababu ya furaha na uhuru wa binadamu, yanageuka kuwa ni kero, ugonjwa na utumwa. Kanisa linataka kuwasaidia watu wote hawa, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kwa kuhimiza kinga, elimu, malezi na makuzi bora. Kwa kuwahakikishia vijana usalama wa maisha yao; umuhimu wa michezo kwa vijana; maisha bora na fursa za ajira ni kati ya mambo ambayo ni muhimu sana na yanayoweza kuchangia mchakato wa kuwazuia vijana kutumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya!

Kardinali Pietro Parolin pamoja na mambo mengine, anakazia umuhimu wa ujenzi wa utamaduni wa mshikamano unaoongozwa na kanuni auni; umuhimu wa kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; ujenzi wa sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana wa kizazi kipya pamoja na kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kanisa ni mtaalam aliyebobea katika utu na heshima ya binadamu anataka kusaidia mchakato wa kuelimisha, kutibu na kumsaidia mtu, daima kwa kulenga mafungamano ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kumwezesha kukua na kukomaa: kiroho, kimwili na kiakili, ili kuwajibika barabara katika maisha na matamanio yake halali. Mama Kanisa anatambua athari za kiafya zinazotokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya, kumbe, kuna haja ya kuendelea kuwaelimisha watu kutambua madhara yake na kuwasaidia kuondokana na utegemezi huu ambao ni hatari kwa maisha yao.

Papa: Nia Aprili 2020
18 April 2020, 12:28