Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua waamini wote duniani kuelezea umuhimu wa Ibada kwa Bikira Maria wakati wa Mwezi wa Mei, uliotengwa na Kanisa kwa ajili yake. Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua waamini wote duniani kuelezea umuhimu wa Ibada kwa Bikira Maria wakati wa Mwezi wa Mei, uliotengwa na Kanisa kwa ajili yake. 

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Waamini Wote Duniani, 2020

Mwezi Mei, waamini kwa namna ya pekee kabisa wanaonesha upendo na ibada yao kwa Bikira Maria. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Kipindi hiki cha Mwezi Mei waamini wamejenga utamaduni wa kusali Rozari Takatifu katika familia zao. Huu ni wakati muafaka wa kukazia dhana ya familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Janga la Corona, limewasaidia waamini kuimarisha tunu msingi za kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika kipindi hiki cha Janga kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, kiasi cha kuzua taharuki, hofu na wasi wasi kubwa miongoni mwa watu wa Mungu, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia waamini wote Barua kwa ajili ya Mwezi Mei, 2020 ambao kadiri ya Mapokeo ya Kanisa umetengwa maalum kwa ajili ya Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, Mwezi Mei, waamini kwa namna ya pekee kabisa wanaonesha upendo na ibada yao kwa Bikira Maria. Ni Mapokeo ya Kanisa kwamba, Kipindi hiki cha Mwezi Mei waamini wamejenga utamaduni wa kusali Rozari Takatifu katika familia zao. Huu ni wakati muafaka wa kukazia dhana ya familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limewalazimisha hata waamini kuimarisha zaidi tunu msingi za maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu Francisko anasema katika muktadha huu, ameona ni jambo jema sana, kwa waamini kugundua tena uzuri na umuhimu wa kusali Rozari Takatifu majumbani mwao wakati wa Mwezi Mei, 2020. Anawaalika waamini kusali Rozari kama mtu binafsi au kama familia kadiri ya hali na mazingira ya watu husika. Mapendekezo yote mawili yanaweza kutumiwa kwa kusoma alama za nyakati. Baba Mtakatifu anasema, siri kubwa ni urahisi wa kuweza kupata utaratibu mzuri wa kuweza kufuata na kusali Rozari Takatifu. Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia waamini na watu wote wenye mapenzi mema Sala mbili kwa Bikira Maria, ambazo hata yeye mwenyewe atazitumia wakati wa kusali Rozari Takatifu, Mwezi Mei 2020, akiwa ameungana moja kwa moja kiroho na waamini wote.

Sala hizi zimeambatanishwa kwenye Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Waamini Wote Kipindi cha Mwezi Mei, 2020, ili ziweze kuwekwa hadharani kwa ajili ya matumizi ya watu wote wa Mungu! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa pamoja Uso wa Kristo, wakiwa wamehifadhiwa kwenye Moyo Mtakatifu wa Bikira Maria, Mama wa Kanisa, anayewawezesha kuungana kwa pamoja kiroho kama familia na atawasaidia kuvuka salama katika majaribu haya mazito yanayomwandama mwanadamu kwa wakati huu. Baba Mtakatifu anasema, atawakumbuka na kuwaombea na kwa namna ya pekee kabisa, anawakumbuka wale wote wanaoteseka! Anawaalika hata wao pia kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mwishoni, anawashukuru waamini wote na kuwapatia baraka zake za Kitume!

Barua Mwezi Mei 2020
25 April 2020, 14:14