Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ameadhimisha kumbukizi la Miaka 93 ya kuzaliwa kwa kuwakumbuka na kuwaombea wagonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI ameadhimisha kumbukizi la Miaka 93 ya kuzaliwa kwa kuwakumbuka na kuwaombea wagonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona.  (AFP or licensors)

Papa Mstaafu Benedikto XVI Miaka 93: Sala kwa Wagonjwa wa Corona

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI: Miaka 93 ya Kuzaliwa: Amepokea salam na matashi mema kwa njia ya simu, kadi na e mail. Amekuwa akijulishwa mwenendo mzima wa maambukizi ya Virusi vya Corona. Ameguswa sana na idadi kubwa ya mapadre, watawa, madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya ambao wamepoteza maisha yao wakati wakiwa wanatoa huduma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, Alhamisi, tarehe 16 Aprili 2020, ameadhimisha kumbukumbu ya miaka 93 ya kuzaliwa kwake kwa Ibada ya Misa Takatifu, akiwa kwenye Monasteri ya “Mater Ecclesiae” iliyoko mjini Vatican pasi na shamrashamra zozote na wala bila kupokea wageni kama ilivyozoeleka kwa miaka mingine iliyopita. Lakini ni tukio ambalo limepambwa kwa sala, sadaka na matashi mema kutoka kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amewakumbuka na kuwaombea kwa namna ya pekee wagonjwa na waathirika wa maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hayo yamebainishwa na Askofu mkuu Georg Gänswein, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI. Ni siku ambayo Baba Mtakatifu Mstaafu amepokea salam na matashi mema kwa njia ya simu, kadi na e mail. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI amekuwa akijulishwa mwenendo mzima wa maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 na kwamba, anafuatilia matukio yote haya kwa hofu na wasi wasi mkubwa kutokana na madhara yake kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Ameguswa na kusikitishwa sana na idadi kubwa ya mapadre, watawa, madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya ambao wamepoteza maisha yao wakati wakiwa wanatoa huduma kwa waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19.  Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI anasema pamoja na ukubwa wa janga hili, lakini watu wa Mungu wasikubali hata mara moja kupokwa imani na matumaini yao! Kwa wakati huu, anautumia muda wake mwingi kwa kusali, kutafakari, kujisomea, kupiga kinanda na kusikiliza muziki kutoka nchini mwake. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, katika kumbukumbu ya miaka 93 tangu kuzaliwa kwake, amepokea Kitabu cha Wasifu wake kilichoandikwa na Bwana Peter Seewald, kitakacho anza kuuzwa madukani mwazoni mwa Mwezi Mei, 2020. Kitabu hiki ni muhtasari wa maisha na utume wake na kimechapishwa na Droemer Knaur. Mwandishi huyu ni gwiji katika taaluma yake na vitabu vyake vimekuwa vikipendwa sana!

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI: Kumbukizi la Miaka 93 ya Kuzaliwa kwake. Historia ya maisha yake kwa ufupi kabisa: Joseph Aloisius Ratzinger, alizaliwa tarehe 16 Aprili 1927. Akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 29 Juni 1951. Akabahatika kufundisha vyuo kadhaa vya taalimungu nchini Ujerumani. Tarehe 28 Mei 1977, akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Munich na Freising na tarehe 27 Juni 1977 akateuliwa kuwa Kardinali. Tarehe 19 Aprili 2005 akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Utume ambao aliutekeleza kwa unyenyekevu, imani, matumaini na mapendo makuu. Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, (1858) sanjari na Kumbu kumbu ya Mkataba wa Lateran (1929), Papa Benedikto XVI alipoamua kwa hiyari yake mwenyewe, kung’atuka kutoka madarakani. Sababu kuu ni kutokana na uzee pamoja na kuanza kuzorota kwa afya yake. Alipenda kutoa nafasi kwa kiongozi mwingine, kuendeleza dhamana na wajibu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Yaliyojiri Kumbukizi la Miaka 93 B16.

 

17 April 2020, 12:41