Tafuta

Papa Francisko, Jumatano, tarehe 8 Aprili 2020 ametafakari kuhusu Fumbo la Mateso katika maisha ya mwanadamu na kuwataka waamini kutafakari mateso ya Kristo katika maisha yao. Papa Francisko, Jumatano, tarehe 8 Aprili 2020 ametafakari kuhusu Fumbo la Mateso katika maisha ya mwanadamu na kuwataka waamini kutafakari mateso ya Kristo katika maisha yao. 

Papa Francisko: Fumbo la Mateso katika maisha ya mwanadamu!

Maadhimisho ya Juma Kuu ni fursa kwa waamini kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao! Iwe ni fursa kutafakari Fumbo la Msalaba, kama kielelezo cha maadhimisho ya Liturujia ya familia, Kanisa dogo la nyumbani. Waamini wakite maisha yao katika sala kwa kutambua kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu na kamwe hawezi kuwaacha pweke!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia Simulizi la Mateso ya Kristo Yesu kuwa ni kiini cha Katekesi yake, Jumatano, tarehe 8 Aprili 2020, wakati huu ambapo watu wengi wanajiuliza maswali mazito yasiyokuwa na majibu ya mkato. Je, kwanini Mwenyezi Mungu hawezi kuingilia kati na kusitisha janga hili la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mwenyezi Mungu mbona amekaa kimya, wala hayaangalii mateso ya watu wake? Simulizi la Mateso ya Kristo Yesu liwasaidie waamini kuzama zaidi katika imani wanapofanya tafakari katika maadhimisho ya Juma Kuu. Jumapili ya Matawi, Kristo Yesu aliingia mjini Yerusalemu kwa shangwe na wengi baadaye wakajiuliza na kusema kwamba, walitumaini kwamba, Kristo Yesu ndiye atakayewakomboa Israeli na adui zake. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, watu hawa walikuwa wanamsubiri Masiha mwenye makuu, nguvu na upanga mkali mikononi mwake. Lakini kwa bahati mbaya, wakashangaa kumwona Masiha ambaye alikuwa ni mpole na mnyenyekevu wa moyo, aliyewaita watu kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuonja huruma na upendo wake wa daima. Lakini ni watu hawa hawa waliokuwa wamepiga kelele wakisema, “Asulubishwe!

Wafuasi wa Kristo Yesu, wakaogopa, wakachanganyikiwa na kumwacha peke yake! Walifikiri mioyoni mwao, ikiwa kama hatima ya Kristo Yesu ni mateso na kifo Msalabani, haiwezekani akawa ni Masiha na Mpakwa wa Bwana kwa sababu Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu na mshindi wa yote! Katika Simulizi la Mateso ya Yesu, Akida aliyesimama hapo akimwelekea Yesu, alipoona kuwa amekata roho jinsi hii, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu”. Mk. 15:39. Huyu alikuwa ni Askari na wala si Myahudi, lakini akaguswa ndani mwake na upendo wa Kristo uliokuwa unabubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba! Hapo akaona uwepo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, leo hii mwanadamu anataka kuona ufunuo wa Uso wa Mungu ambaye ni mwenye nguvu, mwenye mafanikio makubwa na anayetenda haki kadiri ya viwango vya binadamu na hata pengine, kadiri ya vionjo vya watu binafsi. Lakini, Injili inamwonesha Mwenyezi Mungu aliyejinyenyekesha na kuwa karibu pamoja na watu wake kama jirani mwema na Fumbo la Pasaka, likawa ni kielelezo cha juu kabisa cha ufunuo wake.

Juu ya Msalaba, Yesu akaonesha kimya kikuu, akafungua mikono yake ili kuwakaribisha wote waliokimbilia huruma na upendo wake wa daima! Akaufunua utukufu wa Mungu, kwa kuonesha kwamba, kwa hakika alikuwa anapenda si kwa maneno, bali kwa vitendo. Akaonesha ule upendo unaofumbatwa katika kimya kikuu, ili kuwakirimia waja wake maisha; hawalazimishi watu kumfuata, bali anawaachia uhuru unaowawajibisha! Hawatendei waja wake kama “watu wa kuja”, “wageni”, “mnyamahanga” au “vyasaka” bali rafiki na kujitwika udhaifu na dhambi za binadamu, ili kuweza kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Baba Mtakatifu anasema, katika kipindi hiki kigumu, ambacho watu wengi wanalazimika kukaa ndani ya familia zao kwa sababu ya karantini, wajitahidi kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kuuangalia Msalaba kama sehemu ya ushiriki wao katika Liturujia ya Kanisa wakati huu wa maadhimisho ya Juma Kuu. Mambo makuu mawili: Biblia Takatifu na Msalaba! Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu walipokuwa na njaa, walimkimbilia Yesu akawalisha na kuwashibisha, kiasi hata cha kutaka kumkamata na kumfanya kuwa Mfalme wao, lakini Yesu akatoweka na kuondoka zake.

Pale ambapo Shetani, Ibilisi alitaka kufunua Umungu wake, “akashikisha adabu” na kumwambia anyamaze kwa sababu alitaka kufunua huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na makuu. Kristo Yesu, ni Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu, lakini hakutenda dhambi! Akida katika Injili anatangaza kwa ushupavu mkubwa kwamba, kwa hakika mtu huyu alikuwa ni Mwana wa Mungu! Hapa aliona ukuu na nguvu ya Mungu inayofumbatwa katika upendo kwa sababu Mungu ni upendo! Bila shaka waamini wengi wangependa kumwona Mwenyezi Mungu ambaye anajifunua kwa nguvu na vitisho vingi. Lakini ikumbukwe kwamba, upendo wake mkuu unafumbata udhaifu na mapungufu ya binadamu na kuyapatia mwelekeo mpya. Katika Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ameganga na kuponya dhambi za binadamu; akamhurumia na hatimaye, kumkirimia maisha mapya. Kristo Yesu amegeuza hofu na mashaka ya binadamu kuwa ni chemchemi ya imani na matumaini. Pasaka ni ufunuo wa mapenzi mema ya Mungu kwa binadamu! Hii ni kwa sababu mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni tukio la kihistoria na wala “si mambo ya kufikirika wala Hekaya za Abunuwasi”. Ndiyo maana baada ya ufufuko wa Kristo Yesu, waamini wanaambiwa “Msiogope”!

Kristo Mfufuka ni msingi thabiti wa maisha ya wafuasi wake na kamwe hawawezi kuzama na kupotea kutoka katika uso wa dunia! Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Kristo Yesu amekuwa karibu na kati ya watu wake, ameshinda dhambi na mauti. Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaowafikia na kuwaambata watu wote. Mwanadamu anaweza kubadili historia ya maisha yake kwa kumkaribia Mwenyezi Mungu na kupokea wokovu wake. Maadhimisho ya Juma Kuu, iwe ni fursa kwa waamini kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao! Iwe ni fursa kutafakari Fumbo la Msalaba, kama kielelezo cha maadhimisho ya Liturujia ya familia, Kanisa dogo la nyumbani. Waamini wakite maisha yao katika sala kwa kutambua kwamba, wanapendwa na Mwenyezi Mungu na kamwe hawezi kuwaacha pweke! Na kwa tafakari hii ya kina, Baba Mtakatifu amewatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema maadhimisho mema ya Juma Kuu na hatimaye, Pasaka Njema!

Papa: Fumbo la Mateso
08 April 2020, 14:03