Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema, Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya faraja, furaha, imani na matumaini hasa katika nyakati za wasi wasi na hofu kubwa! Papa Francisko anasema, Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya faraja, furaha, imani na matumaini hasa katika nyakati za wasi wasi na hofu kubwa!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Fumbo la Pasaka: Faraja, Furaha na Matumaini!

Kristo Yesu katika maisha na utume wake, ameweza kugeuza ubaya kuwa ni chemchemi ya historia ya wokovu kwa watu. Upendo wa Mungu unaendelea kububujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa na kubaki wazi, kama faraja kwa watu waliokata tamaa na kuteseka, hasa nyakati hizi za shida na mahangaiko makubwa kutokana na maafa yanayosababishwa na Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Katekesi yake kuhusu Fumbo la Mateso ya Kristo Yesu yaletayo maisha na uzima wa milele, Jumatano, tarehe 8 Aprili 2020, ameyaelekeza mawazo yake kwa makundi mbali mbali ambayo tayari yalikuwa yamejipanga kuhudhuria Katekesi hii, lakini kutokana na itifaki inayozuia maambukizi makubwa ya Virusi vua Corona, COVID-19 hawakuweza kuhudhuria. Katika kipindi hiki, kuna wanafunzi wengi kutoka vyuo vikuu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, UNIV. 2020 wanaendelea kukutana kwa njia ya kimtandao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, watu wengi zaidi wataweza kutumia maadhimisho ya Juma Kuu, ili kuimarisha mahusiano na mafungamano yao ya dhati na Kristo Yesu, kwa njia ya Imani kwake Yeye aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Hii ni chemchemi ya imani, matumaini, mapendo na faraja wakati wa majaribu mbali mbali. Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi kuu ni siku muhimu sana zinazounda Juma Kuu, kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu amewatakia waamini wote Pasaka Njema, inayosheheni furaha, faraja na hasa zaidi matumaini kwa kutambua fika kwamba, ufufuko wa Kristo ni ushindi pia wa waamini wake. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, ameweza kugeuza ubaya kuwa ni chemchemi ya historia ya wokovu kwa watu wa Mataifa. Upendo wa Mungu unaendelea kububujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa na kubaki wazi, kama faraja kwa watu waliokata tamaa na kuteseka, hasa nyakati hizi za shida na mahangaiko makubwa kutokana na maafa yanayoendelea kusababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Katika shida na mahangiko mbali mbali, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuungana na kushibana na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Maadhimisho ya Juma Kuu, yawasaidie waamini kutubu na kumwongokea Mungu ili hatimaye, waweze kuadhimisha Fumbo la Pasaka wakiwa na nyoyo zilizotakaswa kwa neema na nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu. Waamini wamwombe Kristo Yesu, ili aweze kuifungua miyo yao, ili hatimaye, waweze kuonja: huruma na upendo aliouonesha kwa njia ya mateso na kifo chake Msalabani, ili kuweza kuwakirimia maisha mapya. Kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, ni wakati muafaka wa kujikabidhi kwa Kristo Yesu, Bwana wa uzima, chemchemi ya amani na matumaini. Fumbo la Pasaka ya Kristo Yesu limebadili mwelekeo mzima wa historia ya maisha ya mwanadamu kwa kuigeuza kuwa ni historia ya wokovu. Watu wa Mungu watambue kwamba, kwa hakika Mungu anawapenda na kuwajali sana.

Upendo wa Mungu usiokuwa na kifani unaendelea kuwasindikiza, kwa kuwa ndani pamoja nao! Watu wawe na ujasiri wa kumwekea Mwenyezi Mungu shida na mahangaiko yao ya ndani, kwani Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma atayageuza mateso na mahangaiko yao, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao! Hakuna sababu ya kutaharuki kwa woga!

Papa: Injili ya Matumaini
08 April 2020, 13:49