Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Alhamisi Kuu 2020 amegusia kuhusu: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na Huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, Alhamisi Kuu 2020 amegusia kuhusu: Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na Huduma ya upendo kwa watu wa Mungu.  (Vatican Media)

Papa Francisko Alhamisi Kuu 2020: Ekaristi! Daraja: Huduma!

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amegusia mambo makuu matatu: Fumbo la Ekaristi Takatifu; Huduma ya upendo kama kibali cha kuingilia mbinguni pamoja na Sakramenti ya Daraja Takatifu. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu kama kielelezo cha upendo wake mkuu kwa waja wake, aliamua kubaki kati yao kwa njia ya uwepo wake katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Asante Mapadre!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mama Kanisa, Alhamisi Kuu ameadhimisha Karamu ya Mwisho, Kristo Yesu, usiku ule alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili na Damu yake Azizi, kama Sakramenti ya upendo, umoja, kifungo cha mapendo, Karamu ya Pasaka ambamo Kristo huliwa na roho hujazwa neema, na ambamo waamini wanapewa amana ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni muhtasari wa imani ya Kanisa katika kufikiri na kutenda! Alhamisi kuu Mama Kanisa anakumbuka pia siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja ambayo ina ngazi tatu: Ushemasi, Upadre na Uaskofu. Huu ni ukuhani wa huduma ambao hutofautiana kiasili na ukuhani wa waamini wote. Alhamisi kuu, Mapadre hushikamana na Maaskofu wao mahalia kwa kurudia tena ahadi za utii. Na katika Ibada hii, Askofu Jimbo anatumia fursa hii kubariki Mafuta Matakatifu.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi Kuu, Jioni, tarehe 9 Aprili 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, huku Ibada hii ikihudhuriwa na idadi ndogo sana ya waamini kuwahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa itifaki ya kuzuia maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID. Hakukuwepo pia na Ibada ya kuwaosha miguu waamini walioteuliwa kama alama ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu inayopaswa kutekelezwa kwa unyenyekevu mkubwa! Baba Mtakatifu katika mahubiri yake, amegusia mambo makuu matatu: Fumbo la Ekaristi Takatifu; Huduma ya upendo kama kibali cha kuingilia mbinguni pamoja na Sakramenti ya Daraja Takatifu. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Yesu kama kielelezo cha upendo wake mkuu kwa waja wake, aliamua kubaki kati yao kwa njia ya uwepo wake katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kwa kushiriki kikamilifu, Mwili na Damu yake Azizi, waamini wanapata chakula kinachowapatia nguvu ya kwenda mbinguni. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha uwepo wa Kristo kati pamoja na wafuasi wake.

Baba Mtakatifu anasema, huduma ya upendo inayotolewa kwa unyenyekevu ni kibali cha kuingilia mbinguni. Katika mahojiano kati ya Kristo Yesu na Mtakatifu Petro, Mtume, Yesu anawakumbusha waja wake kwamba, hawana budi kumpatia nafasi ya kuwahudumia kwanza, kwani Kristo Yesu amejitambulisha kuwa ni Mtumishi mwaminifu wa Mungu anayependa pia kuwahudumia wanadamu. Dhana hii ya huduma inayofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu si rahisi sana kuweza kueleweka, lakini hili ni sharti muhimu la kuweza kuingia katika Ufalme wa mbinguni. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wakleri wote, tangu yule mdogo kabisa ambaye amepewa Daraja Takatifu hivi karibuni hadi Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mapadre wamepakwa mafuta ili kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu na kuwahudumia watu wa Mungu kwa unyenyekevu!

Majimbo mengi hayakuweza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Kubariki Mafuta Matakatifu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Ibada hii inaweza kuadhimishwa kabla ya Sherehe ya Pentekoste, vinginevyo, itahirishwa hadi hapo mwakani. Wakleri ni watu wanaoendelea kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; wamekuwa ni wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa, lakini zaidi, wahudumu wa watu wa Mungu. Takwimu zinaonesha kwamba, tangu kuibuka kwa maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, kuna zaidi ya Mapadre 100 tayari wamekwisha kufariki dunia. Hawa ni Mapadre waliokuwa wanawahudumia wagonjwa. Mapadre, watawa, madaktari, wauguzi na wafanyakazi katika sekta ya afya ni kati ya watu ambao wako kwenye hatari kubwa ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 na kwa hakika wengi wao tayari wamekwisha kufariki dunia!

Kuna baadhi ya Mapadre wanaowahudumia wafungwa magerezani. Huu ni utume tete sana unaohitaji fadhila ya unyenyekevu na udumifu. Ni watu wanaojisadaka kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, lakini hata wao, wanakumbwa na mauti huko huko kwenye huduma! Kuna maelfu ya wamisionari vijana waliotoka kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, wakafia huko huko ugenini kutokana na maradhi mbali mbali na wengi wao hadi leo hii makaburi yao hayana majina! Ni mapadre wanaowafahamu watu wao fika, kielelezo cha uwepo wao wa karibu kwa watu wa Mungu. Wote hawa wamekumbukwa na kuombewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu. Kuna Mapadre ambao wanashutumiwa kwa uwongo! Kashfa ya nyanyaso za kijinsia kwa watoto wadogo imechafua maisha na utume wa Kanisa, kiasi kwamba, hata leo hii kuna Mapadre hawathubutu hata kidogo kuvaa mavazi yao rasmi kwa kuogopa “maneno ya watu”.

Katika hali ya dhambi na ulegevu wa moyo, Wakleri wawe na ujasiri wa kufanya toba na kuomba msamaha; hata wao wakiwa tayari pia kusamehe. Mapadre waombe na kutoa msamaha, tayari kuanza kuandika kurasa mpya za maisha na utume wao. Jambo la msingi kutoka kwa Baba Mtakatifu ni kuwataka Mapadre wasiwe na shingo ngumu kama alivyokuwa Mtakatifu Petro, kwa sababu Kristo Yesu anataka kuwahudumia, kwani yuko karibu sana na maisha pamoja na utume wao, ili aweze kuwajalia nguvu pamoja na kuwaosha miguu yao. Kwa njia hii pia, wataweza kusamehe na kusahau, kwa kuonesha wema, ukarimu na msamaha; kipimo muhimu sana atakachotumia Mwenyezi Mungu kuwahukumu! Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuwa na ujasiri wa kusamehe na kusahau; waendelee kuwafariji watu wa Mungu hata kama wanaweza kuhatarisha maisha yao! Wawe na huruma kwa kuwapatia wakleri wenzao msamaha na upatanisho wa dhambi kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho. Inaposhindikana, wajitahidi kuacha mlango wazi, ili siku moja, aweze kurejea tena. Baba Mtakatifu amehitimisha mahubiri yake kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema na zawadi ya Makleri. Watambue kwamba, kwa hakika Kristo Yesu anawapenda upeo, lakini anawataka kumwachia nafasi ili aweze kuwaosha miguu yao!

Papa: Alhamisi Kuu 2020
10 April 2020, 16:54