Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo na mshikamano wa dhati na wale wote walioathirika kwa virusi vya Corona-COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo na mshikamano wa dhati na wale wote walioathirika kwa virusi vya Corona-COVID-19.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Upendo na Ukarimu kwa waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19

Katika mahojiano maalum na Gazeti “La Repubblica” linalo chapishwa na kusambazwa nchini Italia, Baba Mtakatifu amefafanua kwamba, amemwomba Mwenyezi Mungu katika sala yake ili kwa mkono wake wenye nguvu na maajabu, aweze kusitisha ugonjwa huu wa hatari. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo na ukarimu kwa waathirika wa Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 15 Machi 2020 majira ya Saa 10: 00 za jioni alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Mkuu, lililoko Jimbo kuu la Roma, ili kuomba ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, “Salus popoli Romani” katika kipindi hiki kigumu cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19, sehemu mbali mbali za dunia. Baadaye, Baba Mtakatifu akatembea kwa miguu kwenye barabara ya “Del Corso” kama kielelezo cha hija ya kiroho na kwenda kusali kwenye Kanisa kuu la “San Marcello” lililoko kwenye barabara ya “Del Corso”. Ndani ya Kanisa hili kunahifadhiwa Msalaba wa Miujiza uliotumika kwa maandamano makubwa ya toba na wongofu wa ndani kunako mwaka 1522 ili kuomba huruma ya Mungu kutokana na maambukizi makubwa yaliyokuwa yamesababishwa na mlipuko wa ugonjwa wa Tauni mjini Roma.

Baba Mtakatifu katika sala zake, alimwomba Mwenyezi Mungu awaangalie watu wake kwa macho ya huruma na upendo, ili hatimaye, aweze kusitisha ugonjwa huu unaoendelea kusababisha maafa makubwa sehemu mbali mbali za dunia. Katika mahojiano maalum na Gazeti “La Repubblica” linalo chapishwa na kusambazwa nchini Italia, Baba Mtakatifu amefafanua kwamba, amemwomba Mwenyezi Mungu katika sala yake ili kwa mkono wake wenye nguvu na maajabu, aweze kusitisha ugonjwa huu wa hatari. Katika kipindi hiki kigumu cha myumbo na mtikisiko wa maisha katika ujumla wake, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati katika mambo ya kawaida kati ya wanafamilia, ndugu na majirani. Haya ndiyo mambo msingi yanayokumbatia amana na utajiri wa maisha ya watu wengi.

Huu ni muda anasema Baba Mtakatifu wa kugundua tena ile fadhila ya ujirani mwema. Ni muda wa kujenga na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana, ili kugundua, kuonja na hatimaye, kutimiza mahitaji msingi ya wanafamilia na jirani katika ujumla wao. Watu waonje shida, magumu na matamanio halali ya wanafamilia na jirani zao, tayari kuyamwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hiki ni kipindi ambacho watu wengi wameshikwa na huzuni na simanzi mioyoni mwao, kiasi cha kujikatia tamaa ya maisha! Kristo Yesu, awe ni chemchemi ya faraja na matumaini kwa wale wote wanaoteseka na kuhangaika sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anaendelea kuwashukuru na kuwapongeza wafanyakazi katika sekta ya afya, watu wanaojitolea bila ya kujibakiza pamoja na familia zilizoguswa na kutikiswa kutokana na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hawa ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, mfano bora wa kuigwa katika huduma ya upendo. Baba Mtakatifu anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa karibu zaidi na wale ambao wamewapoteza ndugu, jamaa na marafiki zao kutokana na ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Imani, faraja na matumaini ni changamoto inayopaswa kushuhudiwa na watu wote kadiri inavyowezekana. Mwishoni mwa mahojiano haya, Baba Mtakatifu anawataka waamini, watu wote wenye mapenzi mema na hata wale wasioamini kuwa na matumaini kwani wote hawa ni watoto wanaopendwa na Mwenyezi Mungu. Hata wale ambao bado wanatembea katika ombwe na giza la kutomjua Mungu, kwa sasa wanaweza kuona mwanga na njia ya kufuata; kwa kuonesha upendo wa dhati kwa watoto, wanafamilia, ndugu na jamaa!

Papa: Mahojiano

 

 

18 March 2020, 15:07