Tafuta

Papa Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, ameungana na Maaskofu wa Italia kuombea umoja, amani na mshikamano wa kitaifa. Papa Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, ameungana na Maaskofu wa Italia kuombea umoja, amani na mshikamano wa kitaifa. 

Virusi vya Corona, COVID-19: Papa Francisko: Sala kwa Mt. Yosefu

Papa Francisko tarehe 19 Machi 2020 ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kwa ajili ya kusali ili kuombea Umoja wa Kitaifa nchini Italia katika kipindi hiki kigumu cha mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hili ni tukio ambalo limeungwa mkono na watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliomsindikiza Papa kusali Rozari Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, majira ya usiku, tarehe 19 Machi 2020 ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kwa ajili ya kusali ili kuombea Umoja wa Kitaifa nchini Italia katika kipindi hiki kigumu cha mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hili ni tukio ambalo limeungwa mkono na watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliomsindikiza Baba Mtakatifu kwa kusali Rozari Takatifu, Matendo ya Mwanga. Hiki ni kielelezo cha nguvu ya sala, wakati huu ambapo jitihada za mwanadamu kupata ufumbuzi wa haraka na wa kudumu zinaonekana kusua sua sana wakati ambapo maelfu ya watu wanaendelea kupoteza maisha yao. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video anasema, anapenda kuungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ili kuenzi maneno, matumaini na imani yao.

Ibada ya Rozari takatifu ni muhtasari wa Injili, unaowasaidia waamini kwa njia ya Bikira Maria, kumfahamu zaidi Yesu Kristo, Mkombozi wa dunia. Ni Biblia Takatifu kwa watu wa kawaida, mahali ambapo waamini wanaweza kumfahamu Kristo Yesu kwa njia ya Bikira Maria. Kusali Rozari ni kufanya tafakari ya kina kuhusu Mafumbo ya maisha na utume wa Yesu, kwa kutumia akili ya imani na unyenyekevu wa moyo. Kimsingi Rozari Takatifu ni muhtasari wa ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni sala inayowaongoza waamini kwenye furaha na maisha ya uzima wa milele. Kwa hakika anasema Baba Mtakatifu watu wa Mungu wanahitaji faraja na kujisikia kwamba, wamezungukwa na huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka.

Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha mshikamano na mafungamano ya kijamii na jirani zao; kwa kujikita katika Injili ya upendo, huruma, uvumilivu na msamaha. Kuta zinazowatenganisha, zisiwe ni kikwazo, bali watumie fursa hii kukuza na kudumisha moyo wa ukarimu na uwepo wa huduma kwa ajili ya jirani zao. Baba Mtakatifu anasema, Sala ya Rozari Takatifu, ambayo imewashirikisha watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ilikuwa ni kwa ajili ya kuomba ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yosefu, Mlinzi mwaminifu wa Familia Takatifu ya Nazareti. Mtakatifu Yosefu katika maisha na utume wake, aliguswa na kipeo cha ukosefu wa fursa ya ajira; alikuwa na wasi wasi na yale ya mbeleni; lakini akaonesha ujasiri na kusimama kidete kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake.

Baba Mtakatifu amemwomba Mtakatifu Yosefu kuilinda Italia na watu wake. Awaangazie viongozi wanaosimamia ustawi na mafao ya wengi, ili watambue umuhimu wa kuwahudumia watu waliowekwa chini ya ulinzi na tunza yao. Amewaombea akili na maarifa wanasayansi na wale wote ambao wamezama kutafuta njia sahihi ya maboresho ya afya ya ndugu zao. Mtakatifu Yosefu awatie shime wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya jirani, maskini na wagonjwa. Hawa ni watu wanaojitolea kila siku, wafanyakazi katika sekta ya afya ambao wako mstari wa mbele katika kuwahudumia wagonjwa, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao. Amemwomba Mtakatifu Yosefu alibariki Kanisa: Awabariki watumishi wake, ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa mwanga na mapenzi yake.

Mtakatifu Yosefu azisindikize familia katika hali ya ukimya; asaidie kujenga na kuimarisha amani na utulivu kati ya watoto na wazazi wao; hasa kwa watoto wadogo zaidi. Awalinde wazee dhidi ya upweke hasi unaoweza kuwatumbukiza katika ugonjwa wa sonona na hali ya kukata tamaa. Amemwomba Mtakatifu Yosefu kuwafariji wanyonge, kuwatia shime waliokata tamaa na hatimaye, kuwaombea maskini. Mtakatifu Yosefu kwa kuungana na Bikira Maria, wamwombe Mwenyezi Mungu ili aweze kuukomboa ulimwengu dhidi ya magonjwa ya milipuko!

Papa: Sala Italia

 

20 March 2020, 15:26