Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati ili kuweza kupambana na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati ili kuweza kupambana na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za dunia.  (AFP or licensors)

Virusi vya Corona, COVID-19: Papa: Umoja na Mshikamano!

Watu wajenge na kuimarisha ari na mwamko wa mshikamano. Hiki ni kipindi ambacho waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kukiishi kwa toba na wongofi wa ndani; kwa kusali na kufunga. Ni muda wa kumwilisha upendo, matumaini na unyenyekevu; kwa kuwashirikisha watu wote na wala asiwepo mtu anayebakizwa nyuma au kutengwa. Corona inatisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 yamewaliza, kuwatesa na kuwatikisa watu wote wa Mungu kila mmoja kwa uzito tofauti. Kumbe, mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, ni mchakato unaopaswa kutekelezwa kwa njia ya umoja na mshikamano wa dhati, ili watu wote waweze kuvuka salama kipindi hiki kigumu katika historia ya maisha ya mwanadamu. Watu wajenge na kuimarisha ari na mwamko wa mshikamano. Hiki ni kipindi ambacho waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kukiishi kwa toba na wongofi wa ndani; kwa kusali na kufunga. Ni muda wa kumwilisha upendo, matumaini na unyenyekevu; kwa kuwashirikisha watu wote na wala asiwepo mtu anayebakizwa nyuma au kutengwa.

Hii ni sehemu ya mahojiano kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Domenico Agasso, mwandishi wa Gazeti la “La Stampa” linalochapishwa na kusambazwa kila siku nchini Italia kuhusu changamoto zinazoendelea kujitokeza katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Hakuna mtu awaye yote anayeweza kujihakikishia usalama wa maisha yake dhidi ya ugonjwa huu hatari. Kipindi cha Kwaresima kinapambwa na kurutubishwa kwa maisha ya: Toba na wongofu wa ndani, Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Kufunga pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Katika shida na magumu ya maisha, waamini wajifunze kumkimbilia Kristo Yesu kama walivyofanya Mitume wa Yesu walipokuwa katika hatari ya kuzama kutokana na dhoruba kali. Sala inamwezesha mwamini kutambua na kukiri udhaifu wake wa kibinadamu.

Sala ni kilio cha maskini na wale wote wanaojisikia kuelemewa na majanga na hatari mbali mbali za maisha. Ni watu wanaojisikia kuwa wapweke kweli kweli. Katika hali na mazingira haya, waamini wanapaswa kutambua kwamba, kuna Mwenyezi Mungu ambaye daima anasikiliza na kujibu sala zao kwa wakati. Katika shida na mahangaiko yao, watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anaweza kuwainua na kuwaokoa waja wake. Katika shida na mahangaiko yao, anawapatia pia nguvu na ari ya kusonga mbele kwa imani na matumaini makubwa. Kristo Yesu anatambua fika udhaifu wa wanafunzi wake, kwani walipokuwa wanakaribia kuzama, akawaokoa.

Mtakatifu Petro Mtume alipokuwa anakaribia kuzama baharini, Kristo Yesu akamshika mkono na kumwokoa. Baba Mtakatifu anasema watu wote wanatambulikana kuwa ni binadamu kwa sababu wameumbwa kwa sura na mfamo wa Mungu. Kwa wakati huu wa mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19, watu wote wako kwenye Mtumbwi mmoja. Watu wanalia na kuomboleza kwa sababu wote wanateseka. Umoja, upendo, mshikamano na uwajibikaji pamoja na moyo wa sadaka ni muhimu sana. Ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 unaendelea kusababisha maafa makubwa. Kuna watu wanaofariki dunia wakiwa wameelemewa na upweke bila hata ya kuonja uwepo wa ndugu, jamaa na majirani zao. Wanashindwa hata kuagana na wapendwa wao.

Huu ni wakati wa watu wa Mungu kushikana mikono; kusikilizana na kusaidiana, ili kuweza kukabiliana na balaa hii ya Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna watu ambao ugonjwa huu umewaachia madonda makubwa kwa kuondokewa na ndugu, jamaa na marafiki zao bila ya kuagana. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza: madaktari, wauguzi pamoja na watu wa kujitolea wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa hospitalini. Hii ni changamoto inayopaswa kuwasaidia watu kutambua kwamba, binadamu wote wanaunda familia kubwa ya watu wa Mungu. Huu ni wakati wa kujenga na kudumisha umoja, ili kwa pamoja, waweze kuokolewa. Ni muda wa kujenga udugu wa kibinadamu, kwa kusonga mbele kwa matumaini. Yajayo yanapaswa kusimikwa katika: mizizi, kumbu kumbu hai, udugu na matumaini.

Papa: Mahojiano
21 March 2020, 16:15