Tafuta

Vatican News
Papa Francisko tarehe 19 Machi 2020 ameadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria kwa kuwaombea wafunga gerezani wanaotishiwa na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 Papa Francisko tarehe 19 Machi 2020 ameadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu Mume wake Bikira Maria kwa kuwaombea wafunga gerezani wanaotishiwa na maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 

Virusi vya Corona, COVID-19: Papa Francisko awaombea wafungwa!

Papa Francisko aadhimisha kumbu kumbu ya miaka saba tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kwa kutolea nia ya Misa kwa ajili ya wafungwa na kuwaomba kushiriki kwa hamu Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hiki ni kipindi kigumu sana katika historia na maisha ya wafungwa gerezani kutokana na wasi wasi wa mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vimekuwa ni tishio!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi, anaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria. Sherehe hii inapata chimbuko lake katika Maandiko Matakatifu. Mtakatifu Yosefu ni Baba mlishi wa Kristo Yesu aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu; ni wakili mwaminifu na mwenye busara ambaye Mwenyezi Mungu alimweka kuwa ni msimamizi wa Familia Takatifu ya Nazareti. Mtakatifu Yosefu amekuwa ni mtu wa mwisho kupokea maagizo ya Mwenyezi Mungu katika hali ya unyenyekevu akiwa kwenye ndoto. Mt. 1:20-24. Ni mtu mwamini na mwenye haki. Mt. 1:19. Mtakatifu Yosefu anatoka katika ukoo wa kifalme, kumbe, ni kiungo imara cha ukoo wa kifalme kwa Yesu.

Mtakatifu Yosefu alikabidhiwa dhamana ya kuiongoza, kuilinda na kuitunza Familia Takatifu ya Nazareti kwa kukimbilia Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu na Bikira Maria mamaye na hatimaye, akawarejesha tena mjini Nazareti kama ilivyokuwa kwa Waisraeli kutoka utumwani Misri. (Rej. Kut. 37:50; 22-26; Mt. 2:13-21. Papa Pio wa IX akamtangaza Mtakatifu Yosefu kuwa Msimamizi wa Kanisa zima. Naye Mtakatifu Yohane XXIII wakati wa Maandalizi ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akamteuwa kuwa mlinzi wa Mtaguso na kuandika jina lake katika Kanuni ya Misale ya Kirumi. Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 19 Machi 2013 akasimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, akitoa kipaumbele cha kwanza kwa: Maskini, Amani na Mazingira. Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kujitanabaisha kama “Baba wa huruma ya Mungu” katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, miaka saba tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, ametolea nia ya Misa kwa ajili ya wafungwa na kuwaomba kushiriki kwa hamu Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hiki ni kipindi kigumu sana katika historia na maisha ya wafungwa gerezani kutokana na wasi wasi wa mlipuko wa Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vinaendelea kusababisha taharuki kubwa sehemu mbali mbali za dunia. Wafungwa wana wasi wasi kuhusu hatima ya maisha yao kwa siku za usoni kutokana na ugonjwa huu. Wakiwa huko gerezani, bado wanayaelekeza pia mawazo yao kwenye familia, ndugu na jamaa zao. Baba Mtakatifu anasema, kuna wasi wasi mkubwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 kupiga hodi gerezani na hapo, itakuwa kweli “ni patashika nguo kuchanika”. Matukio yote haya yanawafanya wafungwa kuwa na wasi wasi kuhusu uhakika wa usalama na maisha yao.

Baba Mtakatifu amezama zaidi katika Liturujia ya Neno la Mungu, Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria. Amesema, Mtakatifu Yosefu alikuwa ni mtu mwenye haki, aliyejitahidi kuishi kadiri ya imani yake na Mama Kanisa anatambua na kuthamini mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa. Mtakatifu Yosefu alizamisha maisha yake katika imani, matumaini na mapendo, kiasi cha kuona yale yasioweza kuonekana kwa macho ya kibinadamu pamoja na kugusa yale yasiyoweza kugusika. Yosefu mtu wa haki, alipewa dhamana ya kumfundisha maisha na kazi, Kristo Yesu, Mungu kweli na mtu kweli. Alibahatika kuzungumza na Mwenyezi Mungu katika ndoto, kiasi cha kuzama hadi kwenye kilindi cha Fumbo la Umwilisho.

Katika hali ya ukimya na unyenyekevu mkuu, akaendelea kurutubisha Fumbo hili katika dhamana ya maisha na utume wake kwa umakini mkubwa kama sehemu ya taaluma yake. Hii ndiyo chemchemi ya utakatifu wa maisha ya Yosefu, Baba mlishi wa Yesu, anayeendelea kulitafakarisha Kanisa katika maisha na utume wake. Baba Mtakatifu anawauliza watu wa Mungu ikiwa kama wanayo ile jeuri ya kuingia na kuzama katika Fumbo la maisha ya Mungu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Yosefu? Kanisa halina budi kujenga na kudumisha uwezo wa kuingia na kuzama katika Mafumbo ya Mungu kwa njia ya sala, ili kuweza kumwabudu Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia neema na baraka ya kuweza kuzama katika Mafumbo ya maisha ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuhitimisha Ibada ya Misa Takatifu, amewaalika waamini wote waliokuwa wanafuatilia Ibada ya Misa Takatifu kwa njia ya Televisheni pamoja na mitandao mbali mbali ya kijamii, kujiunga naye ili kuweza kushiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kuonesha ile kiu ya kiroho. Makanisa Jimbo kuu la Roma yamefunguliwa na kuachwa wazi kwa ajili ya waamini wanaotaka kukimbilia huruma ya Mungu kwa sala, lakini hakuna maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa umati wa waamini.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya toba ya kweli ili kupata wongofu wa ndani. Watambue uwepo endelevu wa Kristo katika maisha yao na kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya upendo wake usiokuwa na kifani. Waamini wamwalike Kristo Yesu, ili aweze kuwatembelea katika shida na mahangaiko yao, ili siku ile itakapowezekana, wawe tayari kumpokea. Upendo wa Kristo upyaishe maisha yao, ili uweze kuwaangazia katika maisha na hata katika kifo, kwa sababu wana mwamini na kumpenda Kristo Yesu. 

Papa: Mtakatifu Yosefu

 

 

 

19 March 2020, 14:11