Tafuta

Mtakatifu Yohane Paulo II: Waraka wa Kitume "Evangnelium vitae" Yaani "Injili ya uhai" tarehe 25 Mei 2020 unaadhimisha miaka 25 tangu ulipochapishwa, tarehe 25 Machi 1995 Mtakatifu Yohane Paulo II: Waraka wa Kitume "Evangnelium vitae" Yaani "Injili ya uhai" tarehe 25 Mei 2020 unaadhimisha miaka 25 tangu ulipochapishwa, tarehe 25 Machi 1995 

JPII: Wosia wa Kitume: Evangelium vitae; Injili ya uhai, Miaka 25

Mama Kanisa tarehe 25 Machi 2020 anaadhimisha Kumbu kumbu ya miaka 25 tangu Mt. Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa kitume, Injili ya Uhai. Huu ni mwendelezo wa mafundisho ya kina kuhusu maisha ya mwanadamu yaliyotolewa na Mtakatifu Paulo VI, “Humanae vitae” na Wajibu wa Familia za Kikristo katika Ulimwengu mamboleo: “Familiaris consortio”. Injili ya uhai dhidi ya kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Mama Kanisa tarehe 25 Machi ya kila mwaka anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, mwanzo wa Fumbo la Umwilisho, ni Siku ya Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kuna uhusiano wa karibu kati ya Fumbo la Umwilisho na utume wa familia. Kadiri ya mpango wa Mungu, Yesu Kristo alizaliwa na kukulia katika familia ya binadamu iliyoundwa na Yosefu pamoja na Bikira Maria. Kanisa linapoadhimisha Siku ya Uhai, linapenda kukazia umuhimu wa: maisha, utu na heshima ya kila binadamu. Tangu mwanzo, Mwenyezi Mungu alipenda kuibariki familia na kuipatia dhamana ya kuendeleza kazi ya uumbaji; ili kweli iweze kuwa ni Jumuiya ya maisha na upendo katika moyo wa jamii. Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inajenga na kudumisha utamaduni wa uhai kwani huu ni urithi wa binadamu wote.

Ni mwaliko wa kusoma na kutafakari kwa mara nyingine tena, urithi mkubwa ulioachwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Injili ya Uhai, “Evangelium vitae” iliyochapishwa tarehe 25 Machi 1995 yaani miaka ishirini na mitano iliyopita. Huu ni ujumbe endelevu kwani Mama Kanisa anatambua na kuthamini haki, utu na heshima ya kila mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mkombozi, yaani tarehe 25 Machi, Kanisa sehemu mbali mbali za dunia linatafakari kuhusu Injili ya Uhai kwa sala na shuhuda mbali mbali. Kwa namna ya pekee Mama Kanisa tarehe 25 Machi 2020 anaadhimisha Kumbu kumbu ya miaka 25 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochapisha Waraka wa kitume, Injili ya Uhai.

Huu ni mwendelezo wa mafundisho ya kina kuhusu maisha ya mwanadamu yaliyotolewa na Mtakatifu Paulo VI, “Humanae vitae” pamoja na Wosia wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kuhusu: Wajibu wa Familia za Kikristo katika Ulimwengu mamboleo: “Familiaris consortio”. Waamini wanahamasishwa kusimama kidete kutangaza Injili ya Uhai, Injili ya Familia na kukataa katu katu kumezwa na utamaduni wa kifo. Waamini na watu wenye mapenzi mema wanahamasishwa kukumbatia kweli za Kiinjili na Kanuni maadili kama zilivyobainishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II: “Mng’ao wa ukweli” Veritatis splendor”. Nyaraka zote hizi za Mama Kanisa zinalenga kutetea na kuendeleza Injili ya Uhai kwa kuheshimu na kuthamini uhai, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai”. Kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; Utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha.

Hata leo hii bado kuna damu ya watu wasiokuwa na hatia inaendelea kumlilia Mwenyezi Mungu. Haya ndiyo mauaji ya kimbari na vita. Kuna sera za utoaji na uzuiaji mimba; kifo laini pamoja na uzalishaji kwa njia ya chupa. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamepelekea hata mauaji ya watoto wenye ulemavu kuanzia tumboni mwa mama zao. Yote haya ni matokeo ya uhuru unaoshindwa kutambua: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, kuna haja kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kutambua uwepo wa Mungu na kuzingatia kanuni maadili na utu wema, kwa kuimarisha matumaini pamoja na maboresho katika huduma ya tiba ya mwanadamu. Jitihada hizi hazina budi kwenda sanjari na mchakato wa kupinga adhabu ya kifo na kwamba, umefika wakati wa kuachana na dhana ya “vita halali na ya haki”, ili kujenga na kudumisha kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, pamoja na kupambana dhidi ya mauaji ya kimbari.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Kristo Yesu ni chemchemi ya utimilifu wa maisha, mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai, kwa sababu maisha ni tunu adhimu inayofumbatwa katika maadili na maisha ya kiroho. Ikumbukwe kwamba, utukufu wa Mungu unang’aa katika sura ya mwanadamu kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa utimilifu wa upendo wake ambao ni zawadi ya maisha ya uzima wa milele. Hii ni changamoto kwa waamini kudumisha upendo kwa Injili ya uhai, kwa kuwajibika barabara kulinda na kudumisha maisha. Utu, heshima na haki msingi za watoto ambao hawajazaliwa zinapaswa kulindwa na wote. Maisha yana thamani hata katika mateso, magonjwa na uzee kama yanavyofafanuliwa katika Amri za Mungu. Huu ni mwaliko wa kuendelea kuwa waaminifu katika Sheria na Injili ya uhai. Kristo Yesu, kwa mateso, kifo na ufufuko wake ameonesha kilele cha ufunuo wa Injili ya uhai. Msalabani, Kristo Yesu alionesha ukuu na utukufu wake, chemchemi ya maisha mapya na mwaliko kwa Wakristo kusimama kidete kulinda Injili ya uhai.

Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Usiue kwa sababu maisha ya mwanadamu ni matakatifu na yasioharibika na kwamba, Mwenyezi Mungu ni chanzo na utimilifu wa maisha ya binadamu. Kanisa linalaani vitendo vyote vya utoaji mimba, kifo laini au watu kujinyonga kwa sababu hii ni dhambi dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huruma na upendo ni urithi na amana ya ubinadamu. Mwanadamu anapaswa kuheshimu Sheria na Amri za Mungu, kanuni maadili na utu wema. Upendo kwa Mungu na jirani, usaidie kulinda na kudumisha Injili ya uhai. Mtakatifu Yohane Paulo II analihamasisha Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni mpya wa maisha kwa kulinda na kutetea Injili ya uhai; kwa kutangaza na kuadhimisha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma, ili kuenzi: ukuu na utakatifu wa maisha. Injili ya uhai iwe ni sehemu ya maisha ya sala ya kila siku, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa pamoja na Liturujia ya Mwaka wa Kanisa. Huu ni mchakato wa ushuhuda wa imani tendaji unaozingatia mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kwa kutambua kwamba, familia ni tabernakulo ya Injili ya uhai; kwa kuwalinda na kuwahudumia watu wanaoteseka kwa uzee na magonjwa ya muda mrefu.

Huduma shufaa itolewe kwa kuzingatia maboresho katika huduma ya afya. Injili ya uhai ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na mtu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Wanasiasa wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.  Familia, Kanisa dogo la nyumbani linahamasishwa kuwa ni madhabahu ya Injili ya uhai, ambamo zawadi ya maisha inapokelewa na kutolewa. Familia iwe ni mahali pa kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya mwanadamu kwa njia ya mshikamano na kutembea kama watoto wa mwanga. Lengo ni kuondokana na utamaduni wa kifo kwa kukumbatia na kuambata utamaduni wa uhai. Kila mtu pamoja na taasisi mbali mbali anayo dhamana ambayo anapaswa kuiendeleza, kama shuhuda wa Injili ya uhai na chachu ya mabadiliko ya kweli ndani ya jamii. Amani ya kweli inalinda na kuendeleza Injili ya uhai.

JPII: Evangelium vitae

 

24 March 2020, 11:39