Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu alishinda vishwishi Jangwani kwa nguvu ya Neno la Mungu pamoja na kujiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni! Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu alishinda vishwishi Jangwani kwa nguvu ya Neno la Mungu pamoja na kujiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni!  (ANSA)

Papa: Yesu alishinda Vishawishi Jangwani kwa Neno la Mungu!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kumtoa “mkuku” Ibilisi au kumjibu kwa kutumia Maandiko Matakatifu na kamwe wasijaribu kujadiliana na Ibisili, Shetani, atawavuruga na kuwagalagaza! Hata leo hii Ibilisi bado anaendelea kujiingiza na kujichanganya katika maisha ya watu, ili kwa njia ya sauti yake, aweze kulaza dhamiri nyofu, ili hatimaye, waweze kujilegeza na hatimaye kutenda dhambi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima inasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu, hali amejaa Roho Mtakatifu, alirudi kutoka mto Yordani akaongozwa na Roho kwa muda wa siku arobaini nyikani, akijaribiwa na Ibilisi. Yesu alikuwa anajiandaa kuanza utume wake wa maisha ya hadhara wa kutangaza na kushuhudia ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kama ilivyokuwa kwa Musa na Eliya katika Agano la Kale. Kristo Yesu anakiingia Kipindi cha Kwaresima kwa kufunga. Baada ya kuhitimisha kipindi hiki cha Mfungo, alihisi njaa na hii ikawa ni nafasi ya Ibilisi, Shetani kumjaribu mara tatu ili kumtumbukiza Yesu matatani. Kishawishi cha kwanza kinakita uzito wake katika baa la njaa! Ibilisi akamshawishi Yesu kugeuza jiwe liwe mkate! Yesu akamkata kauli kwa kumwambia, “Imeandikwa ya kwamba mtu hataishi kwa mkate tu bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

Kristo Yesu alikuwa anarejea kwa Mtumishi wa Mungu, Musa aliyewakumbusha Waisraeli waliokuwa safarini Jangwani kwamba, maisha yao yote yalitegemea sana Neno la Mungu. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 1 Machi 2020. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kishawishi cha pili, Ibilisi anajaribu kunukuu hata vifungu vya Maandiko Matakatifu. Lengo ni kutaka kupima imani katika nguvu ya Mungu, kwa kumwagizia Malaika zake wamlinde asije akajikwaa! Hata katika kishawishi hiki, Kristo Yesu anasimama kidete kwa kusema, “Imenenwa, Usimjaribu Bwana Mungu”. Yesu tangu mwanzo wa maisha na utume wake, alijiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kishawishi cha tatu kilikita mizizi yake katika miliki, enzi na fahari zake! Ibilisi alitambua kwamba, hatima ya utawala wake, imefikia ukingoni, kumbe, kishawishi hiki kinapania kuvuruga utimilifu wa kazi ya ukombozi, kwa kumpatia Umasiha wa kisiasa! Alitaka kumtumbukiza Yesu katika utukufu na fahari ya mambo ya dunia Lakini, Kristo Yesu, akajibu kwamba, “Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, Umwabudu yeye peke yake”. Yesu huku akiendelea kuwa mwaminifu kwa kujiaminisha mbele ya Baba yake wa mbinguni, Malaika wakaja na kumtumikia! Baba Mtakatifu anakaza kusema, fundisho kuu hapa ni kwamba, kamwe waamini wasithubutu kujadiliana na Ibilisi, Shetani, ndiyo maana Kristo Yesu alijibu kwa kutumia Maandiko Matakatifu.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kumtoa “mkuku” Ibilisi au kumjibu kwa kutumia Maandiko Matakatifu na kamwe wasijaribu kujadiliana na Ibisili, Shetani, kwani atawavuruga na kuwagalagaza! Hata leo hii Ibilisi bado anaendelea kujiingiza na kujichanganya katika maisha ya watu, ili kwa njia ya sauti yake, aweze kulaza dhamiri nyofu, ili waweze kujilegeza na hatimaye, kukubali kujaribiwa kwa kutenda dhambi na kuanza kufuata njia ya mkato kinyume kabisa cha mapenzi ya Mungu, kwa kujidanganya kwamba, mbele ya Mungu kuna msamaha! Kumbe, huu ulikuwa ni wakati wa kuponda maisha hadi kieleweke! Kwa bahati mbaya yote haya ni mambo ya kufikirika, kwani baadaye, watu wanagundua kwamba wamekwenda mbali na kinyume cha Mwenyezi Mungu! Na hapa ni kilio na kusaga meno, kwani hapo ndipo mtu anapojikuta hana tena ulinzi na hivyo kuanza kukabiliana na matatizo makubwa katika maisha yake.

Mwishoni mwa tafakari yake, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amewaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyethubutu kumkanyaga Ibilisi kichwani, ili kamwe wasikubali kuwa chini ya utumwa wa Ibilis, Shetani. Kipindi cha Kwaresima iwe ni fursa ya kupambana na vishawishi, ili hatimaye, kuibuka kidedea kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu!

Papa: Vishawishi Jangwani
01 March 2020, 10:17