Tafuta

Vatican News
Imani katika uwepo Yesu inakutana  na sisi na kuandamana nasi hata wakati bahari ikiwa na dhoruba Imani katika uwepo Yesu inakutana na sisi na kuandamana nasi hata wakati bahari ikiwa na dhoruba 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani!

Katika ujumbe wa Papa Francisko wa Siku ya 57 ya Kuombea Miito duniani,anafafanua maneno muhimu katika wito ya kwamba ni kutoa shukrani,kuwa na ujasiri,kuna ugumu na sifa.Katika ujumbe huu unaangaziwa na sura ya Injili ya Yesu anayetembea juu ya maji ya dhoruba na kwa amri yake upepo ulikoma.Yesu anatambua wasiwasi,ugumu,shida na ndiyo maana anasema jipe moyo ni mimi.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 57 ya Kuombea miito duniani itakayofikia kilele chake tarehe 3 Mei 2020  unafafanuliwa na ‘Maneno ya wito’ ambayo ni shukrani, ujasiri, ugumu na sifa. Katika ujumbe huo Papa Francisko ameanza kusema kwamba tarehe 4 Agosti mwaka uliopita katika kukumbuka mwaka wa 160 tangu kifo cha Mtakatifu wa Ars (yaani cha Mtakatifu Yohane Maria Vianey) nilipendelea kutoa barua kwa mapadre ambao kila siku wanajikita katika maisha yao kwa wito ambao Bwana amewaita katika huduma kwa watu wa Mungu. Katika fursa hiyo nilichagua maneno kama kiongozi: uchungu, shukrani, ujasiri na sifa ili kweza kushukuru makuhani na kuwatia moyo katika huduma yao ya kichungaji. Aidha Papa Francisko ameandika: Ninaamini kuwa maneno haya katika fursa ya Siku ya 57 ya Kuombea Miito duniani, yanaweza kuwa muafaka na kuwaelekeza Watu wote wa Mungu kwa kuongozwa na  kiini  cha kiinjili kinachosimulia uzoefu wa aina ya pekee waliyokumbana nao Yesu na Petro wakati wa usiku wa dhoruba kali katika ziwa la Tiberiade (Mt 14,22-33). Baada ya mikate mingi, iliyokuwa imewafurahisha umati wa watu, Yesu mara akawalazimisha wanafunzi wake wapande chomboni na kutangulia mbele yake kwenda ng'ambo, wakati yeye alipokuwa akiwaaga mkutano.

Mtumbwi wa maisha unakwenda taratibu 

Papa Francisko ananaendelea kufafanua katika ujumbe wake kuwa: Fursa ya kukatisha ziwa hili ni kama vile mwangwi kwa namna nyingine wa kuelezea safari ya maisha yetu. Mtumbwi wa maisha, kiukweli unakwenda taratibu ukiwa huku na wasiwasi daima wa kujaribu kutafuta fursa, utayari wa kukabiliana na hatari na fursa za bahari, lakini pia hata shauku za kutaka kuwa kama naodha wa kuweza hatimaye kuelekea njia iliyo sahihi. Lakini wakati mwingine  inawezekana kupotea, kupotezwa na mwanga hafifu wa kujidanganya, badala ya kufuata taa angavu, ambayo inakupeleka katika forodha ya uhakika, au kuchangamotishwa na pepo nyingine kinyume na matatizo, mashaka na hofu. Inatokea hivyo hata katika mioyo ya wafuasi ambao wameitwa kumfuata mwalimu wa Nazareth, wanapaswa kufanya maamuzi ya kupitia ng’ambo nyingine, kuchagua kwa ujasiri wa kuacha uhakika binafsi kwa kujikita katika kumfuasa Bwana.

Mchakato huo siyo wa amani, kwa maana unawadia usiku, wa upepo mkali unaovuma kuelekea mkondo kinyume, chombo kinaanza kuyumbishwa na mawimbi na hofu ya kutoweza, hata hali ya kuweza kuitikia wito inahatarishwa. Injili inatueleza kwamba katika mchakato wa safari hiyo isiyo rahisi, hatuko peke yetu! Bwana ni kama vile alilazimisha machweo katika moyo wa usiku, anatembea juu ya maji yaliyochafuka na kuwafikia wanafunzi; anamwalika Petro atembee ili kukutana naye juu ya mawimbi; anamwokoa anapomwona anaanza kuzama,  hatimaye wanapanda chomboni na kutuliza dhoruba hiyo.

Neno la kwanza ni shukrani

Papa Francisko ameeanza kufafanua kwa kuandikia: Neno la kwanza la wito kwa maana hiyo ni shukrani. Kupiga kasia kuelekea  njia sahihi siyo kazi iliyokabidhiwa katika juhudi zetu tu na wala haitegemei njia tunazochagua kuchukua tu. Utimilifu wa sisi wenyewe na mipango yetu ya maisha siyo matokeo ya kihesabu kwa kile ambacho tunaamua ndani (ya umimi binafsi): kinyume chake, awali ya yote ni jambo la wito ambao unatoka kwa aliye juu. Ni Bwana ambaye anatuelekeza ng’ambo ya kwenda na kwamba kabla ya hayo anatupatia ujasiri wa kupanda juu ya mtumbwi. Ni Yeye ambaye wakati anatuita, yeye anakuwa ndiye naodha wa kutusindikiza , kutuonyesha mwelekeo, na kutuzuia kwamba sisi tusije kukwana na  kugonga miamba ya kukosa maamuzi na kutufanya tuweze hata kutembea juu ya maji yaliyochafuka. Kila wito unazaliwa na mtazamo wa upendo ambao Bwana alikuja kukutana nasi labda ni wakati ambamo mtumbwi wetu ulikuwa hatari ya dhoruba.  Zaidi ya kuwa uchaguzi wetu, ni jibu la wito wa bure wa Mungu ( Rej. Barua kwa makuhani, tarehe 4 Agosti 2019): Kwa maana hiyo tutaweza kujigundua na kuukumbatia ikiwa moyo wetu utafikia kutoa shukrani na utatambua kupokea hatua za Mungu katika maisha yetu.

Neno la pili: Jipeni moyo

Wakati wanafunzi walipomwona Yesu akiwakaribia huku akitembea kwa miguu  juu ya maji, mwanzoni walifikiria ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Lakini mara Yesu akawahakikisha usalama kwa maneno ambayo daima yatusindikize katika maisha na katika safari yetu ya wito  yaani “Jipeni moyo ni mimi; msiogope! Mt 14, 27). (kiukweli ndiyo neno la pili ninalitaka kuwakabidhi; jipeni moyo!). Hii ina maana kwamba mara nyingi hofu inatuzuia kutembea, kukua, kuchagua njia ambayo Bwana anachagua kwa ajili yetu, ni vivuli ambavyo vinatikisa mioyo yetu. Tunapoitwa kuvuka  ng’ambo zetu zenye uhakika ili kukumbatia maisha fulani kama vile ya ndoa, daraja la ukuhani, maisha ya kitawa, hali ya kwanza mara nyingi inayojitokeza ni kama kivuli na kutoamini. Ni kufikiria kuwa hiyo siyo wito wangu; je hii ni njia sahihi kweli?, Bwana  kweli anaomba hilo kwangu?

Bwana anajua kuwa wito una ugumu wake

Papa ameongeza kusema kuwa hivyo hivyo yanaongezeka mawazo hayo, ya kutafuta sababu,  kupima kwa kuhesabu mambo ambayo yanatupotezea mwamko, yanatuchanganya na kutuacha tumegandamana ng’ambo kabla ya kuanza safari. Tunaamini tumepoteza mwanga, hatuna uwezo na kwa urahisi wa kufikiria, ni kuona vivuli vya kufukuza. Hata hivyo Bwana anajua kuwa uchaguzi msingi wa maisha kama vile wa ndoa au wa wakfu kwa namna ya pekee katika huduma, unahitaji ujasiri! Yeye anajua maswali, mashaka na matatizo yanayotikisa mitumbwi ya mioyo yetu na kwa maana hiyo anatuhakikishia “jipeni moyo, msiogope, mimi niko nanyi".  Imani katika uwepo wake ni ambayo inakuja kukutana na sisi na kuandamana nasi, hata wakati bahari ina dhoruba, inatuweka kuwa huru dhidi ya ulegevu ambao nilipata nafasi ya kuufafanua kama kwamba ni “huzuni usiyo na utamu”, (Rej. barua ya makuhani tarehe 4 Agosti 2019)  yaani kukata tamaa ya ndani ambayo inazui na haikuruhusu kuonja uzuri wa wito.

Bwana anatuita kwa sababu anataka tuwe kama Petro

Akiendelea kufafanua anasema: Katika barua kwa makuhani, nimezungumzia hata uchungu, lakini hapa ninataka kutafsiri kinyume cha neno na kuelezea juu ya ugumu. Kila wito unapelekea kuwa na jitihada. Bwana anatuita kwa sababu anataka tuwe kama Petro, mwenye uwezo wa kutembea juu ya maji, yaani hiyo ni kuchukua maisha yetu katika  mkono yetu na  kujikita katika huduma ya Injili, kwa njia halisi za kila siku ambazo Yeye anatuonyesha hasa katika aina tofauti za miito ya kilei, kikuhani na maisha ya kitawa. Lakini sisi tunafanana na mitume. Tuna shauku na ari, japokuwa wakati mwingine tumekumbwa na udhaifu na hofu. Ikiwa tunaacha tukumbwe na mawazo ya uwajibikaji ambayo yanatusibiri, katika maisha ya ndoa, au ya huduma ya kikuhani, au katika  shida zitakazo tokea, basi mara moja yatatuondolea ule mtazamo wa Yesu na kama Petro tutakuwa na hatari ya kuzama. Kinyume chake, licha ya udhaifu wetu na umaskini, imani inaturuhusu kutembea na kukutana na Bwana mfufuka na kushinda hata dhoruba. Yeye kwa hakika anatusubiri hasa ikiwa ni uchovu au hofu inayo hatarisha kuzama, anatupatia ari ya lazima kwa ajili ya kuuishi wito wetu kwa furaha na shauku.

Dhoruba na mitikiso inaweza kukaribia makuhani,watawa na wanandoa

Papa Francisko katika ujumbe wake bado amesitiza kuwa: Hatimaye Yesu alipopanda katika mtumbwi, upepo na mawimbi vilitulia. Ni sura nzuri ambayo Bwana anatenda katika maisha yetu na katika wasiwasi wa historia, hasa tunapokuwa na dhoruba. Yeye anaamlisha upepo mkali utulie  na nguvu za ubaya, hofu, kunyong’onyea hakuna nguvu tena juu yetu. Katika kufafanua uhalisi wa wito maalum ambao tumeitwa kuuishi, dhoruba hizi zinaweza kutukaribia. Ninafikiria wale ambao wanajukumu muhimu katika jamii, kwa maana hiyo wanandoa ambao ninapendelea kuwaita kama “wajasiri” na hasa wale ambao pia wanakumbatia maisha ya kitawa na makuhani. Ninatambua ugumu wetu, upweke ambao mara nyingine unakuwa mzito katika moyo, na hatari ya mazoea ambayo kwa taratibu yanazima moto unaowaka wa wito, mzigo wa kutokuwa na uhakika, dukuduku za nyakati zetu,  hofu za wakati ujao. Jipeni moyo, umsiogope!  Yesu yuko karibu nasi hasa tukiwa tunamtambua kuwa ni Bwana mmoja wa maisha yetu. Yeye utushika kwa mkono wake na kutunyakua ili atuokoe.

Sifa:kuimba wimbo wa sifa kama Bikira Maria 

Papa Franciko kwa kuhitimisha ujumbe wake anasisitiza tena kwamba: Hata hivyo licha ya kuwa katikati ya mawimbi, maisha yetu yanafunguliwa kwa sifa. Ndiyo neno la mwisho kuhusu wito ambalo ninataka uwe mwaliko wa kukuza tabia ya ndani ya Mtakatifu  Maria. Yeye akiwa na shukurani kwa mtazamo wa Mungu ambaye alitulia juu yake, alijikabidhi kwa imani, hofu na dukuku, alikumbatia kwa ujasiri wito wake. Yeye alifanya maisha yake  ya milele kuwa kama wimbo wa sifa kwa Bwana! Wapendwa hasa katika siku hii,  lakini pia katika matendo ya kawaida ya kichungaji katika jumuiya zetu, ninapendelea kwamba Kanisa litembee katika mchakato wa safari hiyo ya huduma ya miito, kwa kufungua mikono yake wake katika moyo wa kila mwaamini ili kila mtu aweze kugundua kwa shukrani wito ambao Mungu anawalekeza, kuwa na ujasiri wa kusema “NDIYO”. Kushinda ule ugumu wa imani katika Kristo na hatimaye, kuweza kujitoa maisha binafsi kama wimbo wa sifa kwa Mungu, kwa ndugu na kwa ajili ya ulimwengu mzima. Bikira Maria atusindikize na kutuombea. Amehitimisha Papa Ujumbe wake wa Siku ya 57 ya Kuombea  Miito Duniani.

UJUMBE WA PAPA-WITO
24 March 2020, 12:35