Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amepitisha Sheria Mpya Namba CCCLI (351) inayoratibisha shughuli za Mahakama mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko amepitisha Sheria Mpya Namba CCCLI (351) inayoratibisha shughuli za Mahakama mjini Vatican.  (ANSA)

Papa Francisko apitisha Sheria Namba 351: Mahakama za Vatican

Baba Mtakatifu Francisko kwa kusoma alama za nyakati amepitisha Sheria Namba CCCLI, (351) inayoratibisha Shughuli za Mahakama mjini Vatican kwa kutoa uhuru zaidi kwa Majaji pamoja na kurahisisha utekelezaji wa shughuli za Mahakama mjini Vatican. Ni sheria inayotofautisha kazi za Majaji wanaochunguza tuhuma mbali mbali na wale wanaotoa hukumu ya haki. Uhuru na Taaluma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 16 Machi 2020 amepitisha Sheria Namba CCCLI, (351) inayoratibisha Shughuli za Mahakama mjini Vatican kwa kutoa uhuru zaidi kwa Majaji pamoja na kurahisisha utekelezaji wa shughuli za Mahakama mjini Vatican. Ni sheria inayotofautisha kazi za Majaji wanaochunguza tuhuma mbali mbali na wale wanaotoa hukumu ya haki. Kinachozingatiwa hapa ni uhuru wa Majaji ili kutekeleza vyema taaluma yao bila kuingiliwa na mtu! Sheria hii inafanya marekebisho ya Sheria Namba CXIX (119) ya tarehe 21 Novemba 1987, iliyopitishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II na kurekebishwa na Sheria namba LXVII (67) ya tarehe 24 Juni 2008.

Sheria mpya Namba CCCLI, (351) imepitishwa ili kukidhi mahitaji ya nyakati hizi sanjari na kusoma alama za nyakati zinazohitaji ufanisi zaidi na imegawanyika katika Ibara 31. Sheria hii inatoa fursa kwa Mahakama na Majaji mbali mbali wanaoteuliwa moja kwa moja na Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa uhuru zaidi. Majaji watakaoteuliwa ni wale wanaofundisha vyuo vikuu, wenye uzoefu na sifa nyingine zinazohitajika. Watafanya kazi zao kwa muda wa miaka mitatu na kwamba, watapaswa kuteuliwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mahakama zimeongezewa kitengo kimoja. Sheria hii mpya ni sehemu ya marekebisho ya masuala ya fedha na uchumi mintarafu Sheria na Mikataba ya Kimataifa. Sheria hii pia inafafanua pamoja na mambo mengine haki ya Sheria za Kanisa zinazotekelezwa na Vatican, kama kigezo na rejea katika kufanya tafsiri ya Sheria.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, usimamizi wa rasilimali za dunia ni sehemu ya utekelezaji wa haki inayomwajibisha mtu binafsi, kwa kutambua kwamba, hii ni dhamana inayotekelezwa kwa ukarimu na wale wote waliokabidhiwa madaraka. Kumbe, kuna umuhimu kwa Mahakama na Taasisi zake kuhakikisha kwamba, zinatekeleza Sheria kwa haraka pamoja na kuzingatia ufanisi wake. Mabadiliko haya yanalenga kuisaidia Vatican kutekeleza dhamana na utume wake wa uinjilishaji ulimwenguni. Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo yamesaidia kuanzisha mchakato wa marekebisho ya Taasisi mbali mbali zilizoko mjini Vatican, ambazo nyingi ni zile zilizoanzishwa kunako mwaka 1929, daima Kanisa linataka kusoma alama za nyakati. Sheria hii mpya anasema Baba Mtakatifu inapania pamoja na mambo mengine: kufanya marekebisho makubwa katika mfumo wa Mahakama mjini Vatican ili kuziboresha zaidi kwa kuongeza tija na ufanisi. Baba Mtakatifu ameamua pia kwamba, Mwaka wa Mahakama za Vatican utakua unaanza tarehe Mosi, Januari ya kila mwaka.

Papa: Sheria Mpya

 

17 March 2020, 14:34