Tafuta

Vatican News
Rais Sergio Mattarella wa Italia anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia! Rais Sergio Mattarella wa Italia anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Kumbukizi la Miaka 7 ya Maisha na Utume wake!

Rais Sergio Mattarella, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, tarehe 19 Machi 2020 amemtumia Baba Mtakatifu ujumbe wa matashi mema, akimtakia heri na baraka katika maisha na utume wake. Anampongeza Baba Mtakatifu kwa kuendelea kujipambanua katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; upendo na mshikamano wa dhati kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2013 alianza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, sanjari na Maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Baba mlishi wa Mtoto Yesu. Kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko pia ni Askofu wa Jimbo la Roma, Kanisa ambalo ni kielelezo cha upendo na mshikamano na Makanisa mengine yote yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko na utamadunisho; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Anapenda kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa.

Ni katika muktadha wa kumbukizi la Miaka Saba, tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki, Rais Sergio Mattarella, kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, tarehe 19 Machi 2020 amemtumia Baba Mtakatifu ujumbe wa matashi mema, akimtakia heri na baraka katika maisha na utume wake. Anampongeza Baba Mtakatifu kwa kuendelea kujipambanua katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; upendo na mshikamano wa dhati kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji; pamoja na kuendelea kukazia utandawazi unaojali na kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu badala ya watu kutumbukia katika utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani zao.

Kumbukizi la Miaka Saba tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki imekuja wakati ambapo Italia pamoja nchi mbali mbali duniani zinapambana dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Serikali ya Italia inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuguswa na kuonesha uwepo wake wa karibu kwa mahangaiko ya watu wa Mungu ndani na nje ya Italia. Kwa hakika, katika kipindi hiki kigumu, Baba Mtakatifu amekuwa ni mwanga angavu wa utume na dhamana ya kichungaji, kwa kuwa ni shuhuda amini wa Injili pamoja na kuwahamasisha watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kuendelea kushirikiana na kushikamana ili kupambana na changamoto mamboleo zinazoendelea kumwandama mwanadamu. Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; yote haya ni mambo yanayoweza kuwasaidia watu wa Mungu kupambana na changamoto mbali mbali na hivyo kuendeleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu!

Kumbukizi 7 YRS
20 March 2020, 14:57