Tafuta

Vatican News
Ujumbe wa Kwaresima 2020: Kauli mbiu: "Twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: Mpatanishwe na Mungu" 2 Kor. 5:20 Ujumbe wa Kwaresima 2020: Kauli mbiu: "Twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: Mpatanishwe na Mungu" 2 Kor. 5:20 

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Kwaresima 2020: Upatanisho, Toba na Matendo ya huruma!

Ujumbe wa Papa Francisko katika Kipindi cha Kwaresima 2020 unaongozwa na kauli mbiu “Twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: Mpatanishwe na Mungu.” 2 Kor. 5:20. Anasema, Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ndicho kiini cha toba na wongofu wa ndani, unaowawezesha waamini kumgusa Kristo Yesu kwa njia ya imani, wale wote wanaoteseka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwaresima ni muda uliokubaliwa wa kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, kiini cha maisha ya mkristo mmoja mmoja na Jumuiya ya Wakristo katika ujumla wake. Kwaresima ni kipindi cha kufanya rejea ya Fumbo la Pasaka: kwa akili na moyo wa dhati, ili kuweza kukua na kukomaa kwa kuchota nguvu yake ya kiroho, ili hatimaye, kujibu kwa uhuru na ukarimu. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu “Twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: Mpatanishwe na Mungu.” 2 Kor. 5:20. Anasema, Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ndicho kiini cha toba na wongofu wa ndani, unaowawezesha waamini kumgusa Kristo Yesu kwa njia ya imani, wale wote wanaoteseka.

Baba Mtakatifu anawahamasisha waamini kufanya toba ya kweli kwa njia ya sala, ili kumwongokea Mungu na kuwa tayari kutenda mapenzi yake katika maisha yao. Ni kipindi cha kuingia katika undani wa jangwa la utupu wa maisha, tayari kuanza majadiliano ya kina, kwa kuwapenda jirani lakini zaidi kwa kuwapenda adui zao pamoja na kua na matumizi sahihi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Utajiri na amana ya Fumbo la Pasaka ni tunu shirikishi katika ujenzi wa amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kusimama na kujizatiti katika utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha uchumi shirikishi unaofumbatwa katika kanuni ya upendo!

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Monsinyo Bruno Marie Duffè, Katibu mkuu wa Baraza pamoja na DR. Mariella Enoc Rais wa Baraza la Uongozi wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuongozwa na Vatican, Jumatatu, tarehe 24 Februari 2020 wamewasilisha Ujumbe wa Baba Mtakatifu Franciko kwa Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2020 kwa vyombo vya habari mjini Vatican. Katika hotuba yake elekezi, Kardinali Turkson amekazia umuhimu wa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Hiki ni kipindi ambacho pia Mwenyezi Mungu anawarudia watu wake waliokengeuka na kutopea katika dhambi! Hiki ndicho kiini cha sala.

Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo, ufufuko na kupaa kwake mbinguni, Kristo Yesu ameshiriki ubinadamu unao waunganisha watu na Mwenyezi Mungu. Mpatanishwe na Mungu ni tema inayoongoza ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2020 maana yake ni wongofu na mwaliko kwa binadamu kumrudia tena Mungu wake. Hiki ni kipindi muafaka ya kujiandaa kuadhimisha Fumbo la Pasaka kama sehemu ya mchakato wa kuendeleza maadhimisho haya katika akili na nyoyo za waamini, ili kukua zaidi kiroho kwa njia ya nguvu iliyoko ndani mwao. Huu ni mwaliko wa kujibu wito huu kwa uhuru mkamilifu unaochota nguvu zake katika fumbo la kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Waamini wawe wepesi kukubali na kupokea upendo wa Mungu ambao umefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, ili kujenga mahusiano wazi na majadiliano yenye tija na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani kwa njia ya Sala, matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kwa kujenga na kudumisha moyo wa uvumilivu na utayari wa kusamehe na kusahau!

Kardinali Turkson anasema, jambo hili ni muhimu sana. Upweke hasi kutokana na kiwango kidogo cha watoto wanaozaliwa, mahusiano tenge pamoja na hamu ya watu kutaka kujitegemea na kuwa huru zaidi, ni mambo yanayowakumbusha watu wa Mungu kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Mahusiano na mafungamano haya yanajionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya kifamilia, jumuiya na jamii katika ujumla wake. Utu na haki sawa zinawasukuma kujikita kutafuta mafao ya wengi kwa kutambua kwamba, wao ni binadamu. Watu wanatekeleza dhamana na wajibu huu kwa kuongozwa na mshikamano pamoja na kanuni ya auni. Lengo ni kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anasema, maskini, wagonjwa, wanyonge, pamoja na watu wasiokuwa na makazi maalum, wanapaswa kumegewa Injili ya matumaini na mapendo katika hija ya maisha yao. Kwaresima ni muda muafaka wa kutoka katika lindi la dhambi linalopekenya utu na heshima yao kwa kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, kwa kuishi chini ya ulinzi wa mbawa zake. Nguvu ya Fumbo la Pasaka inaganga na kuwaponya watu na jamii katika ujumla wake. Mahusiano na mafungamano yaliponywa na kutakaswa kwa nguvu ya Fumbo la Pasaka yanatoa maana halisi ya maisha!

Monsinyo Bruno Marie Duffè, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, anasema, toba na wongofu wa ndani ni kiini cha Kipindi cha Kwaresima kama kielelezo cha hija ya imani kama ilivyokuwa kwa Abrahamu Baba wa imani; na kwa Waisraeli chini ya uongozi wa Musa. Waisraeli katika safari ya Jangwani kwa muda wa miaka 40 wakajenga matumaini; wakaanguka na kutopea katika dhambi na hali ya kukata tamaa na hatimaye, kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo hija iliyotekelezwa na Kristo Yesu katika maisha na utume wake na utimilifu wake ni katika Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko kutoka kwa wafu. Lengo la Kristo Yesu ni kumkirimia mwanadamu utimilifu wa maisha na furaha ya kweli na upendo usiokuwa na kifani. Ni kutokana na huruma na upendo wake, Kristo Yesu aliyamimina maisha yake!

Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020, anawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwangalia na kumtambua Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni mwaliko wa kugundua tena na tena: upendo, huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, kielelezo cha maisha mapya katika mwanga angavu wa Fumbo la Ufufuko. Mwaliko wa toba na wongofu wa ndani ni mwaliko maalum katika kipindi hiki cha Kwaresima. Wongofu wa ndani ni msamaha unaokita mizizi yake katika maisha ya ndani. Ni fursa ya maisha mapya katika ukweli na msamaha. Kwaresima ni kipindi cha neema kinachowaondoa waamini kutoka katika utupu na kuwaelekeza kwa Kristo Yesu, mshindi dhidi ya dhambi na kifo; chemchemi ya maisha mapya na furaha shirikishi. Kwaresima ni kipindi cha Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Funga na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu katika mwanga huu wa Kipindi cha Kwaresima anawaalika vijana kuanza mchakato wa ujenzi wa mfumo mpya wa uchumi duniani kwa kukutana mjini Assisi nchini Italia kuanzia tarehe 24-28 Machi 2020.

Hivi karibuni, Baba Mtakatifu amezindua mpango mkakati wa mwaka 2020, tukio la kimataifa litakaloadhimishwa hapo tarehe 14 Mei 2020, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya mfumo wa elimu kimataifa”. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti, kwa kujikita katika elimu fungamanishi inayowataka vijana kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa! Zote hizi ni jitihada za kutaka kumwilisha mang’amuzi haya katika mwanga wa Pasaka. Mang’amuzi haya yanapata chimbuko lake katika Heri za Mlimani, muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu, kwa ajili ya huduma kwa binadamu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria anayeendelea kusali na kuwasindikiza watoto wake, dhamana na utume aliokabidhiwa na Kristo Yesu pale chini ya Msalaba, ili wote waweze kumwendea Kristo Yesu, Mfufuka!

Kwa upande wake, DR. Mariella Enoc Rais wa Baraza la Uongozi wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuongozwa na Vatican, anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya imani inayomwilishwa katika matendo. Huduma katika sekta ya afya iwasaidie waamini kuwa na ufahamu wa kina kuhusu tiba, taaluma na maendeleo ya sayansi yanayoongoza maboresho ya tiba ya mwanadamu. Kanuni maadili, utu, heshima na haki msingi za wagonjwa ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa na wahudumu katika sekta ya afya. Wahudumu wa sekta ya afya wanao wajibu wa kimaadili kuhakikisha kwamba, wanatoa huduma na tiba muafaka kwa wagonjwa. Hiki ni kielelezo na utajiri wa kwanza wanaopaswa kuwashirikisha wagonjwa na familia zao.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia katika tiba ya mwanadamu ni tunu inayopaswa kuwashirikisha wengine kama ambavyo Hospitali ya Bambino Gesu inavyoshirikiana kwa karibu sana na wadau kutoka katika nchi mbali mbali kwa ajili ya elimu na tiba katika nchi ya Siria, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Tanzania, India na Cambodia. Upendo wa ufahamu unasaidia kujenga amani. Huduma kwa wagonjwa ni kielelezo cha upendo wa Kanisa kwa watu wa Mungu. Kwa njia ya majiundo makini ya wafanyakazi katika sekta ya afya na huduma kwa watoto, Hospitali ya Bambino Gesù inatekeleza dhamana na wajibu unaokita mizizi yake katika ujenzi wa diplomasia ya huruma ya Mungu. Ni kwa njia ya diplomasia hii, leo hii watoto kutoka sehemu mbali mbali za dunia wameweza kupata huduma na tiba inayotolewa na Hospitali ya Bambino Gesù, ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na utandawazi wa mshikamano na upendo duniani!

Ujumbe wa Kwaresima 2020

 

24 February 2020, 14:38