Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko analipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kwa kuendesha Kampeni ya Udugu na Mshikamano wakati wa Kwaresima kwa Kipindi cha Miaka 57 Baba Mtakatifu Francisko analipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kwa kuendesha Kampeni ya Udugu na Mshikamano wakati wa Kwaresima kwa Kipindi cha Miaka 57 

Kampeni ya mshikamano na udugu nchini Brazil kwa mwaka 2020

Mwanadamu hakuumbwa kwa ajili ya kifo, bali awe na uzima na utimilifu wa maisha. Baba Mtakatifu Francisko analipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil ambalo kwa muda wa miaka 57 iliyopita limeendesha Kampeni ya udugu na mshikamano katika kipindi cha Kwaresima. Imekuwa ni nafasi ya kumwilisha wongofu wa ndani katika udugu kwa ndugu zao. Udugu na Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, katika maadhimisho ya Jumatano ya Majivu, tarehe 26 Februari 2020 limezindua Kampeni ya 57 Udugu na mshikamano kwa kukazia tunu msingi za maisha ya binadamu yanayopaswa kulindwa, kuendelezwa na kudumishwa, kwa sababu maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kutunzwa daima! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil katika kipindi hiki cha Kampeni ya Udugu na Mshikamano, anawakumbusha kwamba, Kwaresima ni kipindi muafaka cha kusali zaidi, kufunga na kumwongokea Mwenyezi Mungu kama sehemu ya mchakato wa kujiandaa kuadhimisha vyema Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! Kwa muda wa siku arobaini, Mama Kanisa anatoa fursa kwa watoto wake kutafakari kwa kina maana ya maisha, kwa kutambua kwamba, ni kwa njia ya Kristo Yesu peke yake, mwanadamu anaweza kupata jibu la Fumbo la mateso na kifo.

Mwanadamu hakuumbwa kwa ajili ya kifo, bali awe na uzima na utimilifu wa maisha. Baba Mtakatifu analipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil ambalo kwa muda wa miaka 57 iliyopita limeendesha Kampeni ya udugu na mshikamano katika kipindi cha Kwaresima. Imekuwa ni nafasi ya kumwilisha wongofu wa ndani katika udugu kwa ndugu zao. Kampeni ya Mwaka 2020 inawawajibisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujizatiti zaidi kulinda na kudumisha maisha kwa sababu maisha ni dhamana na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kutunzwa. Changamoto hii ni kubwa hasa katika ulimwengu mamboleo unaogubikwa na ongezeko kubwa la mahangaiko ya binadamu kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Hali hizi zimemfanya Mama Dunia na wale waliotengwa kulia wakiomba zichukuliwe njia nyingine mbadala. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa halina budi kujielekeza ili liwe ni Kanisa la Msamaria mwema.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kuna haja ya kuvuka tabia ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kwa kufuata mfano bora wa Msamaria mwema, unaowachangamotisha waamini kukiishi vyema Kipindi cha Kwaresima. Mambo msingi ya kuzingatia ni: kuangalia, kuhurumia na kuhudumia. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu anasikiliza kilio, cha wale wanaoteseka na kuomboleza, waamini nao wanapaswa kufungua akili na nyoyo zao kwa ndugu zao wanaohitaji: kulishwa, kuvishwa, kukaribishwa na kutembelewa.

Kwaresima ni kipindi muafaka cha kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mwenyezi Mungu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutubu na kumwongokea; kwa kuwa na huruma pamoja na kwa kuguswa na mateso ya watu wanaosumbuka bila ya kupata msaada wanaouhitaji. Baba Mtakatifu anawaombea watu wa Mungu nchini Brazil, ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo katika Kipindi hiki cha Kampeni ya Udugu na mshikamano, awawezeshe kujizatiti zaidi katika kulinda tunu msingi za maisha kama zawadi na dhamana inayopaswa kudumishwa! Mtakatifu Dulce dos Pobres, aliyetangazwa mwezi Oktoba 2019, awe ni mfano bora wa kuigwa katika kuguswa na mahangaiko ya jirani zao.

Kampeni ya Udugu Brazil 2020

 

26 February 2020, 14:57