Tafuta

Papa Francisko asema, Kwaresima ni safari katika Jangwa la maisha ya kiroho kwa njia ya sala na kufunga; kwa tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Papa Francisko asema, Kwaresima ni safari katika Jangwa la maisha ya kiroho kwa njia ya sala na kufunga; kwa tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Papa: Kwaresima ni Safari katika Jangwa la Maisha ya Kiroho!

Jangwani ni mahali pa ukimya pasi na kelele isipokuwa upepo mwanana. Ni mahali pa mwamini kujitenga na malimwengu, ili kutoa nafasi ya kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili kuleta faraja katika sakafu ya moyo wa mwamini. Yesu katika Maandiko Matakatifu anazungumzia mara kwa mara kuhusu “Jangwa”. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Musa aliwapatia Amri Kumi kule Jangwani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima kinachodumu kwa muda wa Siku Arobaini, kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kiini cha Mwaka wa Liturujia na imani ya Kanisa. Hii ni hija ya kumfuasa Kristo, ambaye kabla ya kuanza utume wake hadharani, alijitenga kwa ajili ya kusali na kufunga; akajaribiwa Jangwani kwa muda wa Siku Arobaini. Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, Jumatano ya Majivu, 26 Februari 2020, amepembua kuhusu maana ya Jangwa la Maisha ya Kiroho, hata kwa wale wanaoishi mijini! Jangwani ni mahali pa kimya kikuu, pasi na kelele isipokuwa upepo mwanana. Ni mahali pa mwamini kujitenga na malimwengu, ili kutoa nafasi ya kusoma na kulitafakari Neno la Mungu, ili kuleta faraja katika sakafu ya moyo wa mwamini. Kristo Yesu katika Maandiko Matakatifu anazungumzia mara kwa mara kuhusu “Jangwa”. Mwenyezi Mungu kwa njia ya Musa aliwapatia Amri Kumi kule Jangwani.

Waisraeli walipokengeuka na kutopea dhambini kwa kukosa uaminifu kwa Mungu, akawaongoza Jangwani na kuwajibu kama ilivyokuwa wakati wa ujana wao. Jangwani ni mahali ambapo mwamini anaweza kujenga: upendo, mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu. Yesu alipendelea sana kujitenga na makundi ya watu na kwenda Jangwani ili apate kusali, mwaliko kwa waamini katika hija ya maisha yao kutafuta fursa za kujitenga na malimwengu ili wapate kusali katika hali ya utulivu na ukimya. Hii ni changamoto kubwa kwani si rahisi sana kukaa kimya kwani watu wamekwisha jenga mazoea ya kuzungumza na watu. Kwaresima ni muda muafaka wa kutengeneza mazingira kwa ajili ya kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Ni wakati wa kuzima luninga na kufungua Biblia Takatifu; ni muda muafaka wa kuondokana na simu za kiganjani na kuanza kutafakari Neno la Mungu!

Pengine, ni wakati muafaka wa kuzima kidogo radio ili kutafakari Habari Njema ya Wokovu. Ni muda wa kuondokana na majungu, kelele na mazungumzo yalisiyo na faida, ili kuunda mazingira ya kuzungumza mubashara na Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo raha ya Kipindi cha Kwaresima inayofumbatwa katika ujenzi wa ekolojia ya moyo, kwa kusafisha sakafu ya moyo ili iweze kuwa nyeupe pe! Kama tui la nazi! Ulimwengu mamboleo umesheheni watu wanaopenda kuzungumza matusi; kiasi kwamba, “wanaweza kuteremsha matusi kama cherehani”. Huu ni wakati wa kuondokana na matangazo ya biashara ambayo wakati mwingine yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Hali ya utulivu wa ndani na ukimya ni dawa mchunguti inayoweza kuponya maradhi haya kwa kumwachia Mwenyezi Mungu dhamiri yako nyofu ili aweze kuiboresha. Kristo Yesu anawataka waja wake kusikiliza kwa makini na kuzingatia mambo msingi. Ni muhimu sana kwa waamini kusali, ili kupyaisha nyoyo zao na hivyo kuwa ni chemchemi mpya ya uhai na wala si Jangwa la kifo.

Kwa kuzungumzana na Mwenyezi Mungu, anawakirimia waja wake maisha tele! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Jangwa ni mahali panapopatikana mambo msingi ya maisha, kwa kuangalia makandokando ya maisha na hivyo kutoa kipaumbele kwa mambo msingi pamoja na kubahatika kuona sura za majirani wanao wazunguka. Kristo Yesu anatoa mfano mzuri kwa wafuasi wake jinsi ya kufunga, ili kukazia mambo msingi katika maisha, kwa kutafuta na kuambata uzuri na uhalisia wa maisha. Jangwa ni mahali ya upweke chanya. Leo hii kuna watu wanaokabiliwa na upweke hasi, dalili za kifo! Hawa ni watu maskini, wazee na wale wote wanaosukumiza pembezoni mwa jamii! Hawa kimsingi ndio wale “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi”. Ni watu wanaotafuta ukimya wa misaada na majitoleo ya waamini wenzao. Hija ya maisha ya kiroho Jangwani ni hija ya upendo kwa maskini na wahitaji zaidi.

Safari ya Jangwani katika kipindi cha Kwaresima, anasema Baba Mtakatifu Francisko inasimikwa katika: Sala, kufunga, pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mwenyezi Mungu amewawekea waja wake ahadi ya kutenda mambo mapya kwa kufanya njia hata jangwani na mito ya maji nyikani! Hii ni njia inayotoka katika kifo na kuelekea katika uzima. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuanza safari ya kwenda Jangwani wakiwa wameambata na Kristo Yesu, ili kusherehekea Fumbo la Pasaka kwa kuonja nguvu ya upendo na huruma ya Mungu inayopyaisha maisha na kupanda Jangwa maua ya maisha mapya!

Papa: Kwaresima 2020
26 February 2020, 15:41