Tafuta

Vatican News
Papa Francisko anasema, upendo kwa maskini unapyaisha imani na maisha ya kiroho! Papa Francisko anasema, upendo kwa maskini unapyaisha imani na maisha ya kiroho!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Upendo kwa maskini unapyaisha imani na maisha ya kiroho!

Kwa kufuata nyayo za watangulizi wao, Wanachama wa Chama Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hata wao wanashiriki katika utume wa kimisionari unaotekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wake wa mapambano ya ulinzi wa utu, heshima sanjari na maendeleo yake: kiroho na kimwili, bila kujali asili na hali yake ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 24 Fdebruari 2020 amekutana na kuzungumza na wanachama wa Chama Cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: "Pro Petri Sede", wakati huu wanapofanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, wajumbe hawa wanaongozwa na upendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro. Kwa kulizunguka kaburi la Mtakatifu Petro aliyeyamimina maisha yake kama kielelezo cha upendo kwa Mwalimu na Mwokozi wake, hata wao wanatekeleza tendo la imani linalopyaisha maisha yao ya kiroho.

Hii ni fursa ya kuweza kuwasilisha mchango wao wa fedha na maisha ya kiroho ili kuchangia shughuli mbali mbali za kijamii na maisha ya kiroho mintarafu maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na shughuli mbali mbali zinazotekelezwa na Mama Kanisa. Kwa kufuata nyayo za watangulizi wao, hata wao wanashiriki katika utume wa kimisionari unaotekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mchakato wake wa mapambano ya ulinzi wa utu, heshima sanjari na maendeleo yake: kiroho na kimwili, bila kujali asili na hali yake ya kijamii. Katika ulimwengu mamboleo ambamo watu wengi wanatafuta kupata ufanisi, heshima na hata wakati mwingine madaraka, maskini na watu wadogo wanajikuta wakibezwa na hata kusukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, watu wanataka kupata yote kwa mara moja na kwamba, wale wanaobaki nyuma, wanawakera wale wanaotaka kwenda kwa kasi kubwa. Ni katika muktadha huu, “wazee, watoto, walemavu wanaonekana kana kwamba, si mali kitu! Kanisa linataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kwa kujiaminisha kwa watu wenye mapenzi mema na wale wanao ongozwa na Injili, ili kuwapelekea na kuwaonjesha watu wote amani na furaha ya Kristo Mfufuka! Kwa njia ya mchango wao wa hali na mali, kwa hakika wanakuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu inayowakirimia watu wengi ladha ya maisha.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa kwake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, katika kukabiliana na changamoto mamboleo zinazomsibu mwanadamu na mazingira yake. Kuna kilio cha watu wanaoteseka kutokana na vita, kwa kukosa makazi bora, umaskini pamoja na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Kuna haja ya kusimama kidete ili kusitisha kabisa tabia ya unyonyaji wanayofanyiwa maskini na wanyonge ndani ya jamii. Umefika wakati wa kuondokana na vita, kinzani na nyanyaso mbali mbali zinazopelekea makundi makubwa ya watu kuikimbia nchi na makazi yao.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote, kwa kujizatiti katika wongofu wa kiekojia. Maisha ya wanachama wa Chama Cha Mtakatifu Petro kwa ajili ya kusaidia utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni ushuhuda wa maisha ya Kikristo unaofumbatwa katika moyo wa ukarimu kwa kwa kuwajali wengine. Huu ni mwaliko wa kufyekelea mbali ubinafsi na uchoyo, tabia ya kutowajali na kuguswa na mahangaiko ya jirani; hali inayohatarisha amani kati ya watu wa Mataifa pamoja na mazingira.

Baba Mtakatifu anawataka wanachama hawa kujizatiti kikamilifu na kujikita zaidi katika imani ili waweze kuwa kweli ni miale ya moto wa matumaini kwa watu wa nyakati hizi. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro Mtume, wanachama hawa wanapaswa kuwa na ujasiri na uthubutu wa kuwashirikisha wengine upendo wa Kristo Yesu uliofunuliwa kwao. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wanachama wote pamoja na familia zao chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria pamoja na watakatifu kutoka katika nchi zao. Na hatimaye, akawapatia baraka zake za kitume!

Papa: Pro Petri Sede

 

26 February 2020, 14:17