Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko asema Ukanda wa Bahari ya Mediterrania unayo nafasi kubwa katika utangazaji wa Injili pamoja na kurithisha imani inayopyaishwa kwa katekesi, sakramenti na Neno. Baba Mtakatifu Francisko asema Ukanda wa Bahari ya Mediterrania unayo nafasi kubwa katika utangazaji wa Injili pamoja na kurithisha imani inayopyaishwa kwa katekesi, sakramenti na Neno. 

Hotuba ya Papa Francisko kwa Maaskofu Ukanda wa Mediterrania

Ukanda wa Bahari ya Mediterrania una mchango mkubwa katika ustawi, maendeleo na tamaduni za watu; utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu na urithishaji wa imani, madhara ya vita na umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani. Maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kusaidia mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu ili kupambana na umaskini duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 23 Februari 2020 akiwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, Kusini mwa Italia, amekutaka na Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi zinazozunguka Bahari ya Mediterrania. Amepokea taarifa ya mkutano wa siku nne kuanzia tarehe 19-23 Februari 2020; mkutano uliopembua kwa kina na mapana kuhusu changamoto ya kutangaza na kushuhudia imani ya Kikristo, mahusiano ya waamini wa dini mbali mbali na jamii katika ujumla wake; umuhimu wa waamini kuwa ni vyombo na wajenzi wa amani. Baada ya kukutana na Maaskofu hawa, Baba Mtakatifu alikwenda kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika uwanja wa Vittorio Emanuele na hatimaye kusali pamoja nao Sala ya Malaika wa Bwana.

Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwa Maaskofu wanaoizunguka Bahari ya Mediterrania amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa Bahari ya Mediterrania katika ustawi, maendeleo na tamaduni za watu; utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu na urithishaji wa imani, madhara ya vita na umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani. Maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kusaidia mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu ili kupambana na umaskini duniani. Kuna haja ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine ili kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mediterrania ni uwanja wa watu kukutana, kujadiliana pamoja na kuitamadunisha imani.

Baba Mtakatifu amewapongeza Maaskofu kwa juhudi walizozifanya hadi kufanikisha mkutano huu ambao pamoja na mambo mengine, umewawezesha Maaskofu kuanzisha mchakato wa kujadiliana na kusikilizana ili hatimaye, kujenga utamaduni wa amani katika Ukanda wa Bahari ya Mediterrania. Uwepo wake ni ushuhuda wa udugu, umoja na urika wa Maaskofu. Jimbo kuu la Bari ni kitovu cha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kujenga na kudumisha umoja, ujirani na udugu. Utangazaji wa habari Njema ya Wokovu, urithishaji wa imani pamoja na mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa katika Ukanda wa Mediterrania. Ni kwa njia hii, watu kutoka katika mataifa na tamaduni mbali mbali wanaweza kujisikia kuwa ni wamoja na hivyo kutumia rasilimali na uzuri wa eneo hili kwa ajili ya ustawi wa wengi.

Ukanda wa Mediterrania unayo nafasi kubwa katika masuala ya kijamii, kisiasa, kidini na kiuchumi. Lakini kwa bahati mbaya ni Ukanda ambao pia umeacha kurasa chungu katika maisha ya watu kutokana na: vita, kinzani, ukosefu wa haki na usawa na matokeo yake ni kucharuka kwa kinzani za kiuchumi, kisiasa na kidini. Katika muktadha huu, Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha umoja na amani, kama ushuhuda unaobubujika kutoka katika misingi ya amana ya imani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Amana ya Imani: “Fidei Depositum” inapyaishwa kwa njia ya Katekesi makini, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa, uundaji wa dhamiri nyofu, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na Ibada mbali mbali za Kanisa. Amana hii inajidhihirisha hata katika usanii na kazi za sanaa; utajiri ambao unapaswa kulindwa ili kukirithishwa kwa kizazi kijacho. Kumbe, utangazaji na urithishaji wa imani unalenga kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lakini vita, kinzani na migawanyiko imekuwa ni jambo la kawaida katika Ukanda wa Mediterrania.

Biashara haramu ya silaha inayochochea vita na kinzani mbali mbali za kijamii, kisiasa na kidini ni vitendo vinavyopokonya rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kuhudumia familia, kuboresha huduma za afya, elimu, ustawi na maendeleo ya wengi. Vita imesababisha maafa makubwa ya watu na mali zao; uharibifu wa miundo mbinu; vimeharibu mahusiano na mafungamano ya watu kijamii na kiuchumi kutokana na uchu wa mali, utajiri wa haraka haraka na mafao binafsi. Kamwe watu wasikubali vita kuwa ni jambo la kawaida, wasimame kidete kujenga na kudumisha utamaduni wa amani ili kuondokana na chuki na tabia ya kutaka kulipizana kisasi. Kanisa na watu wa Mungu katika ujumla wake, wanapaswa kuwajibika katika mchakato wa ujenzi wa amani duniani.

Kipaumbele cha kwanza kiwe ni mahitaji msingi ya binadamu; kwa kukazia haki, usawa, utu na heshima ya binadamu sanjari na kuondokana na umaskini. Kanisa lichangie utamaduni wa upendo, maboresho ya elimu na malezi. Lisimame kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasaidie kuchangia mapambano dhidi ya umaskini kwa kujenga mshikamano wa upendo. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani ni changamoto changamani inayotumiwa na baadhi ya wanasiasa kutishia usalama wa raia na mali zao, kuchochea vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kiimani na kiitikadi. Jamii inapaswa kujenga mazingira yatakayodumisha usawa kwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi sanjari na kulinda uhuru wa kidini. Dhuluma na nyanyaso za kidini zimeacha madonda makubwa katika nyoyo za watu. Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kulindwa na kutetewa na kamwe wasiwe ni wahanga wa biashara ya binadamu na utumwa mamboleo.

Baba Mtakatifu anasema changamoto ya ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji inapaswa kufanyiwa kazi, ili kuwapokea na kuwakirimia watu hawa wanaoweza pia kusaidia kuchangia ukuaji wa uchumi mahalia. Wakimbizi na wahamiaji wawezeshwe kuunganika na familia zao. Ukanda wa Mediterrania ni mahali pa watu kukutana, kujadiliana sanjari ya kutamadunisha imani. Dhamana na wito huu, usiharibiwe na uchoyo pamoja na ubinafsi unaofanywa kwa kisingizio cha utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko! Vijana wapewe nafasi ya kuwa ni vyombo vya matumaini kwa siku za usoni. Kanisa liendeleze majadiliano ya kidini na kiekumene kwa kujenga utamaduni wa kusikilizana kidugu; kwa kudumisha upendo na ukarimu. Waamini wa dini mbali mbali waondokane na misimamo mikali ya kidini inayohatarisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na matokeo yake ni kumong’onyoka kwa kanuni maadili, utu wema na mafungamano ya kibinadamu. Majadiliano ya kidini na kiekumene ni chachu ya haki na amani.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani, upendo, umoja na mshikamano wa kidugu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, haya ni kati ya mambo msingi ambayo amependa kuwashirikisha kama sehemu ya mchango wa kutangaza na kurithisha imani kwa furaha na katika uhuru kamili kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Habari Njema ya Wokovu iwe ni chemchemi ya matumaini, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu; upatanisho na amani Ukanda wa Mediterrania.

Papa: Hotuba Maaskofu Ukanda wa Mediterrania

 

23 February 2020, 15:09