Tafuta

2020.01.15 Udienza Generale 2020.01.15 Udienza Generale 

Papa Francisko:hata katika mateso Kanisa halichoki kamwe kukarimu!

Katika kiini cha tafakari ya katekesi ya Papa Francisko tarehe 15 Januari 2020 amejikita kuzungumza juu ya hatua ya mwisho wa safari ya Mtakatifu Paulo kuwa ni Roma. Na ndiyo hitimisho la mzunguko wa Katekesi kuhusu mada ya Kitabu cha Matendo ya Mitume aliyoanza tangu tarehe 29 Mei 2019. Anafunga tafakari hii kwa kuonesha kuwa sura ya Kanisa ni kama nyumba iliyo wazi kwa mioyo inayotafuta.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Katika mwanzo wa tafakari ya Papa Francisko katika katekesi ya tarehe 15 Januari 2020 kwenye ukumbi wa Paulo VI Vatican amesema, tuhitimishe katekesi leo hii kuhusu Kitabu cha Matendo ya Mitume kwa hatua ya mwisho ya umisionari wa Mtakatifu Paulo huko Roma (Mdo 28,14). Safari ya Paulo ambayo ilikuwa ya kuhubiri Injili ni ya majaribu mengi pamoja na mapambano ya waamini. Pia ilikuwa na lengo la kuwafanya waamini hao waishi imani, waweze kuwa nafasi ya mpito kuelekea wokovu wa Mungu kwa njia ya Neno la imani, ambalo ni chachu hai ya historia, yenye uwezo wa kubadilisha hali halisi na kufungua njia nyingine mpya. Kufika kwa Paulo katika Moyo Falme ya Roma ndiyo unafunga simulizi ya kitabu cha Matendo ya Mitume na ambapo haifungwi kwa kifodini cha Paulo bali kwa wingi wa upanzi wa Neno. Mwisho wa simulizi ya Luka unaojikita katika safari ya Injili duniani, unajikita na kueleza kwa upya mwendo wa Neno la Mungu, Neno ambalo halifungiki na ambalo linataka kukimbia ili kuwatangazia wokovu watu wote.

Ndugu katika Kristo Roma walimsubiri kwa hamu Paulo

Mjini Roma Paulo alikutana, awali ya yote, na ndugu katika Kristo ambao walimkaribisha na yeye kuwaimarisha katika ujasiri (Rej Mdo 28,15)   Na katika vuguvugu la makaribisho hayo Papa Francisko amethibitisha kwamba linatufanya tufikirie jinsi walivyokuwa wanamsubiri na kwa hamu kufika kwake. Na baadaye walimruhusu kuishi peke yake chini ya ulinzi wa kijeshi (custodia militaris,) kwa maana ya kuwa na askari aliyekuwa anamlinda, na  kwa njia hiyo alikuwa na kifungo cha nje, Papa anabainisha. Licha ya kukaa katika hali yake ya kifungwa Paulo aliweza kukutana na mawakili wa kiyahudi ili kuwauliza kwa nini amelazimishwa kupelekwa kwa Kaisari na kuzungumza nao juu ya ufalme wa Mungu. Yeye alitafuta kuwashawishi juu ya mtazamo wa Yesu, kuanzia katika Maandiko na kuwaonyesha mwendelezo kati ya mambo mapya ya Kristo na matumaini ya Israeli (Rej 28.20). Paulo anajitambua kwa kina kuwa yeye ni myahudi na anajiona katika Injili anayohubiri, kwa maana ya tangazo la Kristo aliyekufa na kufufuka katika kutimiza ahadi aliyosema kwa watu wateule.

Paulo kwa siku nzima alitakanga Ufalme wa Mungu

Baada ya mkutano wa kwanza wa kawaida ambapo anakutana na Wayahudi walio tayari, unafuata mkutano mwingine maalumu ambao, kwa siku nzima Paulo alitangaza Ufalme wa Mungu na kutafuta jisni ya kuwafungulia wasikilizaji wake imani katika Yesu kuanzia na “Sheria ya Musa hadi kwa Manabii” (Mdo28,23).  Kutokana na kwamba siyo wote walioshawishika, Yeye anawaonya kwa kuwatangazia kwamba ugumu wa mioyo ya watu wa Mungu ni sababu ya hukumu (Rej Is 6,9-10), na kutangaza kuhusu upendo wa wokovu kwa mataifa ambayo kinyume wanajionesha umakini kwa Mungu na uwezo wa kusikiliza Neno la Injili katika maisha, (Mdo At 28,28).

Neno la Mungu halifungwi mnyororo kama Paulo

Papa Francisko ameongeza kusema; kwa maana hiyo simulizi la Luka linahitimishwa na huduma yake akionesha kuwa  siyo kifo cha Paulo, bali ni mwendelezo wa mahubiri yake katika Neno ambalo “halifungwi minyororo” (2Tm 2,9). Paulo hana uhuru wa kuzunguka, lakini ana uhuru wa kuzungumza kwa sababu Neno halijafungwa mnyororo, bali liko tayari kujipanda peke yake katika ujazo wa mikono ya Mtume. Paulo alikuwa akihuburi ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi ( Mdo 28,31), katika nyumba ambayo wanapenda kupokea mafundisho juu ya Ufalme wa Mungu na kumjua Kristo.

Mioyo iliyo wazi katika kutafuta ndiyo sura ya Kanisa pamoja na kuteswa kwake linaendelea kukarimu

Nyumba hii, iliyo wazi kwa wote katika mioyo inayotafuta, ndiyo sura ya Kanisa ambalo pamoja na kuteswa kwake, kama inavyoonekana kufungwa na mnyororo, halichoki kamwe kukarimu kwa moyo wa imana kila mwanaume na mwanamke ili kuwatangazia wao upendo  wa Baba ambaye amejifanya kuonekana katika Yesu. Papa Francisko kwa kuhitimisha safari hii ya tafakari ya Kitabu cha Matendo ya Mitume kwa kufuata mbio za Injili duniani, anamomba Roho Mtakatifu anawafanye waamini  wawe hai kila mmoja katika ule wito wa kuwa wainjilishaji hodari na wenye furaha. Bwana awawezeshe kama Paulo, kujibidisha katika Injili katika  nyumba zao na kuwafanya kuwa karamu ya kidugu mahali ambapo wanampokea Kristo aliye hai, na ambaye anakuja kukutana na kila mtu kwa kila wakati.

15 January 2020, 11:33