Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wazazi na walezi kujikita katika malezi na makuzi ya watoto wao kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wazazi na walezi kujikita katika malezi na makuzi ya watoto wao kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko!  (Vatican Media)

Papa Francisko: Furaha ya upendo ndani ya familia! Malezi na makuzi ya watoto!

Wazazi wanapaswa kuwa ni walezi na warithishaji wa imani, maadili na utu wema kwa watoto wao, lakini utume huu sasa unafanywa na baadhi ya taasisi pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Makanisa mahalia yanapaswa kuwaandaa wanasheria watakaosaidia kuunda Mahakama za Kanisa Kikanda pamoja na kushughulikia kesi mbali mbali kwa haraka bila kucheleweshwa sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alifanya hija ya 30 ya kitume kimataifa  huko Romania iliyoongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja” ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kufuata nyayo za mashuhuda wa imani, waliomimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Baba Mtakatifu alikwenda nchini Romania kama hujaji na ndugu yao katika Kristo ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano unaokita mizizi yake katika amana na utajiri wa imani nchini Romania! Hija ya Baba Mtakatifu nchini Romania kuanzia tarehe 31 Mei hadi tarehe 2 Juni 2019, ilikita ujumbe wake katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene, changamoto ya kuvumbua tena tunu msingi za maisha ya kiroho, katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili familia ya Mungu nchini Romania iweze kwenda kwa pamoja! Hili lilikuwa ni tukio la kihistoria tangu Kanisa lilipotengana kunako mwaka 1054 na huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Wakati wa hija hii ya kitume Baba Mtakatifu alipata fursa ya kukutana na kuzungumza na Wayesuit wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Romania pamoja na kujibu maswali kadhaa kutoka kwa Wayesuit.

Nchini Romania, Wayesuit wamejikita katika sekta ya elimu na utamaduni; mafungo na maongozi ya kiroho; utume kwa vijana pamoja na huduma katika Parokia mbali mbali nchini Romania. Wayesuit wako pia mstari wa mbele katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, changamoto kubwa inayopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Wayesuit katika mazungumzo haya wamesema, licha ya watu wengi kuthamini mchango unaotolewa na Wayesuit katika maisha na utume wa Kanisa, lakini pia wamekuwa wakipokea shutuma nzito, kiasi cha kuwakatisha tamaa na kuona kana kwamba, yote wanayofanya ni ubatili mtupu! Katika changamoto na hali kama hizi, Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa uvumilivu na udumifu, kwa kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati. Huu ni muda muafaka wa kukaa na kutafakari; kusikiliza kwa uvumilivu na kujadiliana katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Nyakati kama hizi ni muda uliokubalika kwa ajili ya kusali na kumwachia Mwenyezi Mungu ili aweze kuzungumza kutoka katika undani wa maisha yao, ili kwa mwanga wa Neno na mang’amuzi yao ya ndani, waweze kuendelea na hija ya huduma kwa watu wa Mungu. Katika nyakati za shida na karaha katika maisha, ni muda wa kujenga ukaribu na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Ibada ya Kuabudu pamoja na maadhimisho mbali mbali ya Sakramenti za huruma ya Mungu kwa waja wake. Waangalie pale walipoteleza na kuanguka, tayari kuomba neema na baraka za kusimama tena na kusonga mbele, huku wakijitahidi kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu kwa njia ya sadaka na majitoleo yao katika huduma makini. Wakati mwingine, busara inadai kukaa kimya, lakini pale ambapo kuna ukweli unaoweza kusimama na uongo kujitenga, basi majadiliano katika ukweli na uwazi yanaweza kuanzishwa. Angalisho hapa ni kuwa makini, majadiliano haya si kwa ajili ya kujibu mashambulizi, kwani hayatasaidia, bali ni kufafanua na kuweka mambo katika uhalisia wake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ushauri huu ameufafanua kwa kina na mapana katika Kitabu chake kijulikanacho kama “Lettere della Tribolazione” yaani “Nyaraka katika mateso”. Hiki ni kitabu kinachofafanua nyakati za mateso na mahangaiko kwa Shirika la Wayesuit duniani. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha Wayesuit kuhusu umuhimi wa kuiga mfano wa Kristo Yesu, wanapokabiliwa na shutuma pamoja na mashtaka mbali mbali hata pengine yale ambayo hayana ukweli ndani mwake! Kristo Yesu mbele ya shutuma na mashitaka kutoka kwa Mafarisayo, Masadukayo na Waandishi wa sheria, alibaki kimya, kiasi hata cha kuwashangaza watesi wake. Wakati wa madhulumu na nyanyaso, jambo la msingi ni kukuza na kudumisha ushuhuda wa maisha; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa maisha ya sala inayomwilishwa katika Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni katika wema na unyoofu wa moyo, mwamini anaweza kukumbatia Fumbo la Msalaba katika maisha yake.

Baba Mtakatifu akijibu kuhusu Injili ya faraja anaendelea kufafanua kwamba, haya ni matokeo ya uchunguzi wa dhamiri nyofu mbele ya Mwenyezi Mungu. Faraja kubwa anayoweza kupata mwamini katika shida na mahangaiko yake, inabubujika kutoka katika sala ambamo Mwenyezi Mungu anawafariji waja wake, kwa kuwakirimia imani na matumaini. Faraja inapatikana kutoka kwa watu wa Mungu wanaowahudumia, kwani hawa ndio wale wanao onja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya huduma inayotolewa na Mapadre wake. Baba Mtakatifu anawaalika Wayesuit kuwathamini na kuwasilikiza watu wa Mungu kwani hata wao wana “Sensum fidei”, inayosaidia kurekebisha mapungufu ya kibinadamu na kuwaonesha dira na njia ya kufuata katika maisha. Wawasikilize wazee na vijana yale wanayotamani kutoka katika undani wa nyoyo zao. Kuna maelfu ya waamini na watu wenye mapenzi mema, wanaojisadaka kwa ajili ya kuwambea Mapadre wao, lakini pia katika “msafara wa Mamba, Kenge hakosekani” kumbe, kuna waamini wengine wanaojitahidi kulishambulia Kanisa na viongozi wake.

Hili ni jambo la kawaida katika maisha. Umoja, mshikamano na upendo kwa watu wa Mungu, utawawezesha viongozi wa Kanisa kutambua yale mema wanayofanya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu pamoja na kasoro wanazopaswa kuzivalia njuga katika maisha yao, ili kuzirekebisha kwani kukosa na kukoseana ni mtindo wa maisha; kusamehe na kusahau ni mwanzo wa utakatifu. Mapadre wajenge utamaduni na Ibada ya kukimbilia katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika maisha yao, ili aweze kuwafariji na kuwaombea kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, kwani Bikira Maria ni Mama wa Mungu na Kanisa. Ibada ya Rozari Takatifu muhtasari wa historia nzima ya ukombozi ni sala maalum kwa watu wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini lakini zaidi Mapadre kukukuza na kudumisha Ibada ya Rozari Takatifu. Mapadre wajitahidi kukutana na watu wa Mungu katika uhalisia wa maisha yao, katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, katika raha na shida! Ni katika uhalisia wa maisha ya watu, Mapadre wanaweza kuonja ikiwa kama wanapendwa kweli kutoka undani wa maisha ya watu, au wanachukiwa na kwamba, wamegeuka kuwa ni kero isiyoweza kuvumiliwa tena! Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho hata kidogo!

Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”, ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo. Unatoa mwelekeo wa Kristo Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Ni wosia unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Baba Mtakatifu anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao wa ndoa na familia. Wayesuit wamemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Injili ya ndoa na familia nchini Romania inakabiliwa na changamoto pevu kutokana na uwepo mkubwa wa wingi wa tamaduni, mila, desturi na mapokeo ya watu kutoka sehemu mbali mbali za Bara la Ulaya.

Hii ni changamoto ambayo Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwahi kuigusia. Lakini, ikumbukwe kwamba, kulega lega kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ni kielelezo cha uhaba wa imani, matumaini na mapendo thabiti. Kuna wakati ndoa inageuka kuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia. Katika muktadha kama huu, mchakato wa kutengua ndoa kama hii unaweza kufanywa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wamejadili changamoto hii kwa kina na mapana na matokeo yake ni Waraka wa wa Kitume“Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia”. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hata leo hii, bado mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi kuhusu masuala tete ya ndoa na familia yanaendelea kuwagawa waamini. Sinodi za Maaskofu kuhusu familia zilizoadhimishwa kunako mwaka 2014 na Mwaka 2015 zilibainisha changamoto za kisiasa, kijiografia na kitamaduni mintarafu utandawazi, mambo yanayolitaka Kanisa kuwa karibu sana na waamini kama Msamaria mwema; Mama mwenye huruma na mapendo, anayefundisha, anayeganga na kutaka kuponya madonda yanayowaandama watoto wake katika uhalisia wa maisha!

Kuna matatizo na changamoto za kanuni maadili na utu wema; uwepo wa utamaduni wa kifo na mwelekeo tenge wa tendo la ndoa unaogeuzwa kuwa ni fursa ya kukidhi tamaa za mwili badala ya kuwa kweli ni kielelezo cha utimilifu wa upendo kati ya bwana na bibi. Dhamana na utume wa familia katika nchi nyingi duniani, haupewi msukumo unaostahili na matokeo yake, familia imekuwa kama “mpira wa danadana”. Elimu makini kwa watoto ni dhamana ambayo kwa sasa inaondolewa kutoka kwa wazazi na walezi na matokeo yake ni mwelekeo tenge wa usawa wa kijinsia unaotaka kufuta tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Kimsingi, wazazi wanapaswa kuwa ni walezi na warithishaji wa imani, maadili na utu wema kwa watoto wao, lakini utume huu sasa unafanywa na baadhi ya taasisi pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa  Makanisa mahalia kuwaandaa wanasheria watakaosaidia kuunda Mahakama za Kanisa Kikanda pamoja na kushughulikia kesi mbali mbali kwa haraka bila kucheleweshwa sana!

Majadiliano ya Kiekumene miongoni mwa wakristo, yanapata chimbuko lake kutoka katika asili ya utume wa Kanisa lenyewe. Ni mchakato unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha katika imani. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”, anasema kwamba, majadiliano ya kiekumene si sehemu ya mchakato wa shughuli za kidiplomasia au jambo la kulazimishana, bali ni changamoto ya kufanya toba na wongofu wa ndani, ili Wakristo kwa pamoja, waweze kushikamana katika kutangaza Furaha ya Injili ili ushuhuda wao uweze kuwa na mvuto pamoja na mashiko. Huu ndio mwendelezo wa Mafundisho wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Hati za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu: Kanisa, Majadiliano ya Kiekumene na Makanisa ya Mashariki ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, katika mchakato wa ujenzi wa Umoja wa Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hakuna sababu msingi kwa waamini wa Kanisa la Kiorthodox kuhamia katika Kanisa Katoliki; Makanisa haya mawili yanategemeana na kukamilishana katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene.

Baba Mtakatifu amegusia pia kuhusu ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kukuza na kudumisha ubinafsi na choyo, kiasi cha watu kujifikiri na kujitafuta wenyewe, na hivyo kushindwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao. Hiki ni kielelezo cha upagani mamboleo. Kuna wakimbizi na wahamiaji wanaokufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania; wanaoteseka kwa njaa na kiu ya kutisha kwenye Jangwa la Sahara; kuna watu wanaokufa kwa baa la njaa na utapiamlo, lakini kuna watu wanaokula na kusaza, kiasi hata cha kufanya kufuru; matukio ya majanga na maafa sehemu mbali mbali za dunia, yanaanza kuzoeleka na kuwa si tena sehemu ya habari inayovuta hisia za huruma, upendo na mshikamano na watu kama hawa! Hizi ni dalili za upagani mamboleo. Huu ni mwaliko hata kwa Mama Kanisa kufungua macho yake na kuangalia kile kinachotendeka katika uhalisia wa maisha ya watu! Hiki ni kielelezo cha watu kumezwa sana na malimwengu. Jamii inayoshindwa kufurahi pale palipo na furaha; kulia na kuhuzunika na watu wake wanapokumbana na majonzi, tambua kwamba, hapa kuna jambo ambalo si sawa sawa katika akili na nyoyo za watu!

Watu wanapaswa kujenga umoja na udugu; kushikamana na kusaidiana katika hali mbali mbali za maisha, ili kudumisha udugu wa kibinadamu, kamwe kifo hakiwezi kuzoeleka, kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anasema,  Shirika la Wayesuit linaundwa na watu kutoka katika mataifa, makabila, mila na desturi mbali mbali. Tofauti hizi msingi ni amana na utajiri  katika maisha na utume wa Kanisa na kamwe isiwe ni sababu ya kuwagawa na kuwanyanyasa watu. Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, wanayo dhamana na wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kanisa liwe ni sauti ya kinabii kwa wale wasiokuwa na sauti katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni. Maendeleo endelevu na fungamani yanatoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu  Francisko alivyohitimisha mazungumzo yake ya maswali na majibu alipokutana na kuzungumza na Wayesuit wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Romania.

Papa: Wayesuit
28 December 2019, 16:21