Tafuta

Vatican News
Wosia wa Kitume wa Papa Francisko "Evangelii gaudium" yaani "Furaha ya Injili" ni dira na mwongozo wa shughuli za kichungaji kwa sasa na kwa siku za mbeleni. Wosia wa Kitume wa Papa Francisko "Evangelii gaudium" yaani "Furaha ya Injili" ni dira na mwongozo wa shughuli za kichungaji kwa sasa na kwa siku za mbeleni.  (ANSA)

Wosia wa Kitume: Evangelii gaudium: Furaha ya Injili! Dira na Mwongozo wa Kichungaji

Huu ni ushuhuda wa furaha na upendo unaobubujika baada ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha na hivyo, hii inakuwa ni fursa ya kufanya mabadiliko makubwa katika maisha. Jambo la msingi hapa ni ushuhuda wenye mvuto kama chachu ya uinjilishaji ilivyoshuhudiwa na watu kama Maria Magdalena, baada ya kukutana mubashara na Kristo Mfufuka, siku ile ya kwanza ya juma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” uliochapishwa tarehe 24 Novemba 2013, unatoa kipaumbele cha kwanza kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu. Katika mwono huu, Kristo Yesu ni kiini cha Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya Uinjilishaji Mpya. Wosia huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa siku za mbeleni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi. Wosia huu wa kitume unachota utajiri wake kutoka katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza Imani ya Kikristo.

Baba Mtakatifu Francisko, akayasoma na kuyafanyia tafakari ya kina na hatimaye kuyaweka kuwa ni sehemu ya ujumbe wake kwa Familia ya Mungu wakati huu inapojielekeza katika hija ya Uinjilishaji Mpya, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ndiye kiini cha Uinjilishaji na ndiye Mwinjilishaji Mkuu. Wakristo wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi, iliyoanzishwa na Yesu mwenyewe katika mazingira na tamaduni mpya za uinjilishaji. Mwono huu wa kimisionari ni mwaliko kwa Makanisa mahalia kuangalia changamoto na fursa zilizopo mintarafu tamaduni na hali halisi ya nchi husika. Baba Mtakatifu anatoa kigezo kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu na kwa kila mdau wa uinjilishaji, ili kwa pamoja kuwa na mbinu mkakati shirikishi katika mchakato mzima wa uinjilishaji pasi na kujitenga kama kisiwa!

Wosia unabainisha nguzo kuu saba za uinjilishaji zinazopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mwono wa uinjilishaji Mpya: Mageuzi ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, Kanisa kimsingi ni la kimissionari; vishawishi vya wainjilishaji, Kanisa kama Familia ya Mungu inayotumwa kuinjilisha; Umuhimu wa mahubiri na matayarisho yake; ushiriki wa kijamii wa maskini katika maisha na utume wa Kanisa; amani na majadiliano ya kijamii na kiini cha kazi ya uinjilishaji inayofanywa na Mama Kanisa. Yote haya yanakita mizizi yake katika huruma na upendo mfunuliwa wa Mungu unaogusa moyo wa kila mtu kwa kukutana na Kristo Yesu, chemchemi ya furaha inayomsukuma mwamini kushirikisha upendo huu kwa wengine. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko alikutana na kuzungumza na washiriki wa mkutano wa kimataifa kuhusu umuhimu wa kumwilisha Wosia wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” katika maisha na utume wa Kanisa.

Mkutano huu uliandaliwa Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya kwa kuwashirikisha wawakilishi kutoka katika nchi 62 duniani. Mkutano huu umefanya tathmini ya Wosia wa Kitume “Furaha ya Injili” miaka sita na jinsi ambavyo unaendelea kumwilishwa katika maisha na utume wa Makanisa mahalia. Wosia huu unawahamasisha waamini kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili, kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa kwanza wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu katika hotuba yake alikazia umuhimu wa Kanisa kuwa huru na malimwengu, tayari kutoka kifu mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa ulimwengu mamboleo. Huu ni ushuhuda wa furaha na upendo unaobubujika baada ya kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha na hivyo, hii inakuwa ni fursa ya kufanya mabadiliko makubwa katika maisha.

Jambo la msingi hapa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kama chachu ya uinjilishaji ilivyoshuhudiwa na watu kama Mtakatifu Maria Magdalena, baada ya kukutana mubashara na Kristo Mfufuka, siku ile ya kwanza ya juma. Mtakatifu Maria Magdalena akawa ni mwinjilishaji wa kwanza kwa Mitume wa Yesu, akishuhudia ile furaha ya kukutana na Kristo Mfufuka, chemchemi ya upendo usiokuwa na mipaka. Upendo huu ukafyekelea mbali hofu na mashaka yaliyotanda wakati wa mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Huu ni mwaliko wa kuishi na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha, ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, tabia ya ulaji wa kupindukia na ubaguzi na utengano usiokuwa na tija. Kuna watu wanaotafuta maana ya maisha, mateso na mahangaiko ya mwanadamu, usaliti pamoja na upweke hasi unaotishia usalama wa maisha yao. Baba Mtakatifu anasema, hawa ni watu wanaopaswa kushikwa mkono na kuanza kutembea bega kwa bega, ili hatimaye, kuwa ni wandani wa safari.

Mchakato wa uinjilishaji unafumbatwa katika umoja, mshikamano na mafungamano katika misingi ya ukweli, uwazi na upendo, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Katika muktadha huu, hakuna maadui, bali wote wanakuwa ni wandani wa safari. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kukosa na kukoseana ni sehemu ya ubinadamu. Kumbe, wainjilishaji wawe ni watu wanaomtafuta Mungu kwa kushirikiana na wengine ili kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. Udhaifu na mapungufu ya kibinadamu yasiwe ni kikwazo cha kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, bali kielelezo cha neema na huruma ya Mungu inayotenda kazi ndani mwao. Kuna wakati ambapo Mwenyezi Mungu anatumia hata vyombo dhaifu kufikishia watu ujumbe wake. Mungu ni upendo unaoshirikishwa na kuwaambata watu wote. Huu ni wakati wa kila mwamini kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, waamini wanahitaji Kanisa ambalo liko huru, lisilomezwa na malimwengu kwa kutafuta rasilimali fedha na utajiri kwa udi na uvumba. Kanisa lioneshe na kushuhudia ufukara wake kama chachu ya uinjilishaji. Mfano wa mashuhuda, waungamana imani na watakatifu wa Kanisa la mwanzo uwe ni kikolezo cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Waamini wawe na matumaini na kamwe wasikubali kubebeshwa huzuni na masikitiko nyoyoni mwao. Waamini wawe na ujasiri wa kumkimbilia Roho Mtakatifu ili awasaidie kupata ari na nguvu mpya ya kumtangaza Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ushuhuda wa upendo iwe ni sumaku ya kuwavuta watu kumwendea Kristo Yesu. Waamini wajifunze kujivika ufukara, tayari kujisadaka kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji mpya!

Papa: Furaha ya Injili
04 December 2019, 17:26