Tafuta

Vatican News
Siku ya Walemavu Duniani inaadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba: Utu, heshima na haki msingi za walemavu zinapaswa kuzingatiwa na kudumishwa. Siku ya Walemavu Duniani inaadhimishwa kila Mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba: Utu, heshima na haki msingi za walemavu zinapaswa kuzingatiwa na kudumishwa.  (Vatican Media)

Ujumbe wa Papa Francisko: Siku ya Walemavu Duniani kwa Mwaka 2019

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Walemavu Duniani kwa Mwaka 2019, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwaangalia walemavu kwa jicho la imani na kuwashirikisha upendo wa dhati na kwa kufanya hivi watambue kwamba, wanamshirikisha Kristo Yesu mwenyewe anayejitambulisha na ndugu zake walio wanyonge na maskini. UTU!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba inaadhimisha Siku ya Walemavu Duniani, kwa kukazia: utu, heshima na haki zao msingi. Walemavu wana thamani kubwa katika maisha ya kiimani, kwani wanashiriki katika mateso na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Utu na heshima yao vinapaswa kulindwa na kuheshimiwa. Walemavu kwa upande wao, wapokee hali yao ya maisha kwa imani na matumaini. Wasikilizwe katika shida na mahangaiko yao ya ndani; washirikishwe katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuwamegea ukarimu na kulinda haki zao msingi. Wapewe huduma za tiba; miundo mbinu iwawezeshe kuishi kwa ukamilifu zaidi, wakiendelea kusaidiwa na Familia zao; daima mafao yao kama binadamu yapewe kipaumbele cha kwanza. Mama Kanisa anapenda kuonesha ukaribu wake kwa walemavu, kwa kuwashirikisha mwanga wa imani, matumaini, mapendo na mshikamano wa kweli.

Walemavu ni watu wanaopaswa kupewa tiba, lakini zaidi waonjeshwe upendo, watambuliwe, waheshimiwe na kushirikishwa katika maisha ya jamii inayowazunguka. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Walemavu Duniani kwa Mwaka 2019, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwaangalia walemavu kwa jicho la imani na kuwashirikisha upendo wa dhati na kwa kufanya hivi watambue kwamba, wanamshirikisha Kristo Yesu mwenyewe anayejitambulisha na ndugu zake walio wanyonge na maskini. Kuna haja ya kuimarisha haki msingi za walemavu na ushiriki wao katika maisha ya kijamii ili kuondokana na unyanyapaa na hatimaye, kujenga utamaduni wa watu kukutana pamoja na kuwa na maisha bora zaidi. Baba Mtakatifu anasema, kumekuwepo na maendeleo makubwa kwenye tiba na huduma msingi za binadamu, lakini hata leo hii bado kuna watu wanabaguliwa kiasi cha kushindwa kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ili kuwa na ushiriki mkamilifu, kuna haja ya kusimama kidete kulinda na kudumisha haki za watu wenye ulemavu pamoja na familia zao, sanjari na kuhakikisha kwamba, jamii inajitahidi kujenga mazingira yenye utu wema, kwa kung’oa vizingiti vya maamuzi mbele, miundo mbinu hatarishi na mambo yote yanayopekenyua ubora wa maisha ya watu. Walemavu wanapaswa kusindikizwa katika hatua mbali mbali za maisha yao, kwa kutumia vyema maendeleo ya sayansi na teknolojia, lakini utu na heshima yao vikipewa kipaumbele cha kwanza. Walemavu washirikishwe kikamilifu katika maisha ya jamii inayowazunguka. Hii ni hija yenye ugumu na changamoto zake, lakini ni muhimu sana katika kufunda na kuelimisha dhamiri nyofu, ili kutambua utu na heshima ya kila binadamu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, walemavu wanaonekana kuwa kama ni “watu walioko kwenye kifungo cha ndani katika familia na jamii nyingi”.

Kundi hili linawajumuisha wazee na hasa kutokana na ulemavu wao, wanaonekana kuwa kama “mzigo mzito kwa jamii”, kiasi kwamba, wanaweza hata kutelekezwa na kupuuzwa katika masuala ya ajira. Kuna haja ya kuwajengea uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao ili hatimaye, waweze kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi. Walemavu watambuliwe na kuheshimiwa kwani hata katika ulemavu wao wanaweza kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii inatokana na ukweli kwamba, mchango wao hautegemei sana matumizi ya milango ya fahamu. Kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuthamini utu na heshima ya binadamu kwa kuondokana na tabia ya kuwagawa watu katika makundi, wale ambao wako kwenye Kundi A na “Akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, yaani watu wa Kundi B. Walemavu wapewe sauti, haki na usawa. Ni wakati wa kuongoka na kubadili tabia inayotaka kujenga matabaka kati ya watu, kiasi cha kuwa ni kikwazo kwa walemavu kuweza kushiriki katika shughuli za kawaida.

Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni anasema Baba Mtakatifu kumekuwepo na harakati za kutaka kuwashirikisha walevu katika medani mbali mbali za maisha, lakini juhudi hizi zinakumbana na maamuzi mbele, ukosefu wa fursa sawa ya elimu, ajira na ushiriki mkamilifu wa walemavu. Walemavu wanapaswa kutambuliwa uwepo, ushiriki na utambulisho wao katika jamii. Mwishoni mwa ujumbe wake kwa Siku ya Walemavu Duniani kwa Mwaka 2019, Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wale wote wanaojisadaka kwa ajili ya huduma kwa walemavu, kuendeleza huduma hii muhimu, kielelezo cha ustaarabu wa taifa husika. Anawaombea watu wote ili waweze kuhisi Uso wa Mungu katika maisha yao, ili kudumisha utu na tunu msingi za maisha ya watu.

Papa: Walemavu

 

 

03 December 2019, 16:14