Tafuta

Vatican News
Tukio la uchumi wa Francisko litaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 26-28-machi-2020-mpango-mkakati-utume-kanisa-vijana Tukio la uchumi wa Francisko litaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 26-28-machi-2020-mpango-mkakati-utume-kanisa-vijana  (ANSA)

Uchumi wa Francisko: Kutimua vumbi Machi 2020, mjini Assisi!

Kuna haja ya kuwa na mfumo ya uchumi unaolinda na kutunza mazingira; uchumi unaoenzi zawadi ya maisha; kwa kudumisha tunu msingi za maisha ya familia; usawa wa kijamii, utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi, pamoja na kuwahakikishia vijana haki zao msingi. Kwa bahati mbaya, ni watu wachache sana ambao wamesikiliza na kutambua matatizo ya uchumi mamboleo! Utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni tukio ambalo litawakusanya wachumi na wajasiriamali wachumi vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kuanzia tarehe 26- 28 Machi 2020 huko Assisi, nchini Italia. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, unaotekelezwa kwa namna ya pekee, na Baba Mtakatifu Francisko. Hii itakuwa ni nafasi kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kukutana na kuzungumza na vijana wanaojifunza uchumi unaotekelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu! Anataka kuzama zaidi katika uchumi unaohuisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika kifo. Uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu; uchumi unaojikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko katika barua ya mwaliko kwa wachumi na wajasiriamali vijana, anawataka kujikita katika mchakato wa kupyaisha mchakato wa uchumi duniani, kwa kujikita katika udugu kama alivyokazia Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kuuchagua mji wa Assisi kuwa ni kitovu cha amani na kwa sasa yeye anataka mji wa Assisi uwe ni jukwaa la mchakato wa mfumo mpya wa uchumi mpya duniani.

Mji wa Assisi ni mahali ambapo, Mtakatifu Francisko wa Assisi alipouvua utu wake wa kale na kumchagua Mwenyezi Mungu kuwa ni dira na mwongozo wake wa maisha; na hivyo kuwa maskini kati ya maskini na ndugu ya wote. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maamuzi haya machungu, yakaibua dira na mwelekeo mpya kuhusu mwono wa kiuchumi unaotoa matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu katika ujumla wake. Mwelekeo huu ni muhimu sana katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama anavyokazia Mtakatifu Francisko wa Assisi katika “Utenzi wake wa ndugu Jua”. Mazingira na maisha ya binadamu vinategemeana na kukamilishana, ili haki iweze kupatikana kwa ajili ya maskini pamoja na kupata majibu muafaka wa matatizo ya muundo wa uchumi kimataifa. Baba Mtakatifu anasema, kuna haja ya kuwa na mfumo ya uchumi unaolinda na kutunza mazingira; uchumi unaoenzi  zawadi ya maisha; kwa kudumisha tunu msingi za maisha ya familia; usawa wa kijamii, utu, heshima na haki msingi za wafanyakazi, pamoja na kuwahakikishia vijana haki zao msingi ili kuwa na maisha bora zaidi kwa siku za mbeleni.

Kwa bahati mbaya, ni watu wachache sana ambao wamesikiliza na kutambua matatizo ya uchumi mamboleo kiasi hata cha kuthubutu kuweka mifumo mipya ya uchumi ambayo ni matunda ya utamaduni wa umoja unaojikita katika udugu na usawa. Mtakatifu Francisko wa Assisi ni mfano bora wa kuigwa katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na ekolojia fungamani. Ni Mtakatifu Francisko aliyethubutu kufanya ukarabati mkubwa wa “Nyumba ya Mungu” iliyokuwa inaporomoka. Huu ni wajibu wa watu wote yaani: Kanisa jamii na kwa kila mtu binafsi. Utunzaji bora wa mazingira unahitaji uchumi makini na maendeleo fungamani yanayoweza kuponya madonda, na hivyo kuwahakikishia watu matumaini kwa siku za mbeleni. Ili kuweza kutekeleza kwa dhati changamoto hii, kuna haja kwa kila mtu kuanza kufikiri na kujikita katika kanuni maadili, Amri za Mungu na mafao ya wengi. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika vijana, wanaotamani maisha bora na yenye furaha, vijana ambao ni alama ya kinabii, ili waweze kuonesha dira ya uchumi ambao uko makini kwa binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, vijana wa kizazi kipya, kutoka katika undani wa maisha yao, wamesikiliza kilio cha Mama Dunia na watoto wake maskini, wanaohitaji msaada, unao wawajibisha na kamwe wasikimbie dhamana hii, bali wasimame kidete kujenga na kudumisha utamaduni wa ujasiri, tayari kuthubutu kuanza ujenzi wa jamii mpya. Kristo Mfufuka ndiyo nguzo yao na kwamba, vijana wanapaswa kuwa ni wadau wakuu katika mchakato wa mageuzi, ili kuwa na kesho iliyo bora zaidi. Vyuo vikuu, shughuli mbali mbali za biashara, makongamano na warsha ni mahali muafaka pa kujenga njia za uelewa mpya wa uchumi na maendeleo, ili kuweza kukabiliana na utamaduni wa kutupa, kwa kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti na hatimaye, kuwa na mtindo mpya wa maisha, ili watu wote katika umoja wao, waweze kufurahia udugu wa kiulimwengu. Mkutano wa Uchumi wa Francisko huko Assisi una pania kuragibisha “Agano la pamoja” kama sehemu ya mchakato wa mabadiliko ulimwenguni kwa kuwakumbatia na kuwaambata watu wote bila ya kujali tofauti za imani wala utaifa wao, bali watu ambao wanaongozwa na dhana ya udugu, kwa kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu anawaalika vijana kujenga ndoto ya ubinadamu mpya ili kujibu matarajio ya watu kadiri ya mpango wa Mungu. Katika mchakato huu, Mtakatifu Francisko wa Assisi, aliyejitahidi kumwilisha Injili katika maisha yake, alisaidia kuleta mabadiliko katika masuala ya kijamii na kiuchumi. Anatoa mawazo na programu katika utekelezi wa mazingira, amani na maskini ndiyo maana alimchagua kuwa ni Msimamizi katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu akiwa ameshikamana na vijana, atawahamasisha magwiji wa sera na mipango ya uchumi duniani kuunda mwelekeo mpya wa uchumi na anatumaini kwamba, wataitikia mwaliko huu. Lakini, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ana matumaini makubwa kwa vijana, wenye uwezo wa kuota ndoto, wanaojiandaa kwa msaada wa Mungu kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki na uzuri. Baba Mtakatifu anasema, anatarajia kuwepo yeye mwenyewe, kuwapokea na kuwakaribisha mjini Assisi kuanzia tarehe 26 -28 Machi 2020.

Uchumi wa Francisko 2020
28 December 2019, 16:48