Tafuta

Vatican News
Siku kuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na shahidi: mfano bora wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo ya Kiinjili. Siku kuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na shahidi: mfano bora wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya matendo ya Kiinjili.  (AFP or licensors)

Siku kuu Mtakatifu Stefano: Huduma ya upendo wa Kiinjili na udugu!

Stefano, Shahidi kijana na mhudumu wa Injili alikua amejaa Roho Mtakatifu, akafanikiwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu ambaye alitimiza ahadi yake kwa wafuasi wake, kwa kumpatia nguvu ya Roho Mtakatifu ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo. Stefano alijitahidi kumuiga Mwalimu wake aliyejiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni pamoja na kuwasamehe watesi wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Stefano Shemasi ni shuhuda wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni kati ya Mashemasi saba waliochaguliwa na Mitume wa Yesu kwa ajili ya huduma kwa Jumuiya ya Wakristo wa kwanza. Utume ambao aliutekeleza kwa muda mfupi sana ikilinganishwa na matumaini ya Mitume wa Yesu. Mtakatifu Stefano alikuwa ni mwema, mwenye kujawa na Roho, na hekima. Alitenda maajabu na ishara, kisha akafungwa. Akabahatika kuwa ni shuhuda wa Yesu pamoja na kupewa neema ya kutafakari utukufu wa Kristo Mfufuka, kiasi hata cha kutangaza Umungu wake. Kabla ya kifo chake, akajiaminisha kwa huruma na upendo wa Kristo Yesu. Katika mateso makali akathubutu kuwasamehe watesi wake, mbele ya Kristo Yesu ili asiwahesabie dhambi hii, akiisha kusema haya akalala! Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 26 Desemba 2019 amesema, Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Stefano Shahidi.

Liturujia ya Neno la Mungu inajikita zaidi katika hatua ya mwisho mwisho wa maisha ya Mtakatifu Stefano, alipokamatwa na kupelekwa mbele ya baraza na huko akafunguliwa mashitaka ya uongo juu ya kufuru kwa mahali patakatifu na juu ya torati. Katika muktadha wa Sherehe ya Noeli, kwa baadhi ya watu Siku kuu ya Mtakatifu Stefano, Shahidi inaweza kuonekana kuwa hapa si mahali pake. Lakini mwamini akizama zaidi, atagundua kwamba, hapa ni kiini cha maana ya kweli ya Sherehe ya Noeli. Hapa ni mahali ambapo mauaji ya kikatili yanashindwa na upendo; Injili ya uhai inapeta zaidi kuliko utamaduni wa kifo na kwamba, huu ni ushuhuda wa hali ya juu kabisa unaomwezesha Mtakatifu Stefano kumtafakari Kristo Mfufuka na hatimaye, kuwa na ujasiri wa kuweza kuwasamehe watesi wake. Stefano, Shahidi kijana na mhudumu wa Injili alikua amejaa Roho Mtakatifu, akafanikiwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu ambaye alitimiza ahadi yake kwa wafuasi wake, kwa kumpatia nguvu ya Roho Mtakatifu ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Mtakatifu Stefano, Shemasi na Shahidi amejitahidi sana kumuiga Mwalimu wake, Kristo Yesu kwani alipokuwa kufani, alijiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni pamoja na kuwasamehe watesi wake! Stefano Shahidi naye alipokuwa anakaribia kufa aliomba akisema, “Bwana Yesu pokea roho yangu”. Sala hii ni sawa na ile sala ya Yesu alipokuwa kufani alisema, “Baba mikononi mwako naiweka roho yangu”. Waamini wanapaswa kujifunza kwamba, utukufu wa mbinguni unaodumu milele yote unafumbata kwa namna ya pekee upendo na sadaka ya mtu binafsi na wala si kwa utajiri na utawala wa nguvu za kibinadamu. Kuna haja kwa waamini kuwa na subira pamoja na kuyaelekeza macho yao mbinguni ili kumtazama Kristo Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yao, ili kuwa tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililoko ndani yao, kwa njia ya changamoto na majaribu ya maisha ya kila siku.

Kwa Wakristo mbingu haiko mbali sana kiasi cha kutenganishwa na dunia. Kristo Yesu aliyekuwa mbinguni ameshuka na kuja hapa duniani. Kumbe, kwa njia ya Roho Mtakatifu waamini hata katika ubinadamu wao wanaweza kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, ambaye anawawezesha kuwa wanyenyekevu, wajasiri, wapole, watu wa amani na wenye nguvu! Stefano Shemasi na Shahidi ni mfano bora wa kuigwa katika kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya udugu wa kibinadamu na matendo ya upendo wa Kiinjili. Ushuhuda wake, ulihitimishwa kwa kifodini, chemchemi ya upyaisho wa Jumuiya mbali mbali za Kikristo. Hizi ni Jumuiya zinazopaswa kuendelea kujipyaisha katika ari na mwamko wa kuwa ni za kimisionari, ili kuinjilisha kwa kuwaendelea watu ambao wamesukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; mahali ambako kuna kiu kubwa ya matumaini na wokovu. Baba Mtakatifu anazitaka Jumuiya za Kikristo zitoe kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu na wala zisijitafute zenyewe, bali ziwe ni alama na ushuhuda wa utukufu wa Mungu unaopewa kipaumbele cha kwanza, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, hususan maskini na wahitaji zaidi.

Siku kuu ya Mtakatifu Stefano Shemasi na Shahidi ni changamoto na mwaliko wa kuwakumbuka mashuhuda wa imani wa jana na leo, kwa kuonesha umoja na mshikamano pamoja nao. Waamini wawe na ujasiri wa kuwaomba ili wawaombee neema ili hata wao waweze kuishi na hatimaye kuaga dunia wakiwa wanatangaza Jina la Yesu midomoni na nyoyoni mwao. Bikira Maria, Mama wa Mkombozi, awasaidie kuishi vyema kipindi hiki cha Noeli kwa kumtazama Kristo Yesu, ili siku moja, waweze kufanana naye!

Papa: Stefano Shahidi
26 December 2019, 16:01