Tafuta

Vatican News
Siku ya Kuombea Amani Duniani ilianzishwa na Mtakatifu Paulo VI tarehe Mosi, Januari 1968. Siku ya Kuombea Amani Duniani ilianzishwa na Mtakatifu Paulo VI tarehe Mosi, Januari 1968.  

Siku ya Kuombea Amani Duniani 2020: Amani ni safari ya matumaini

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 53 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu: Amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia. Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maagamizi: Vunjilieni mbali hofu na vitisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Kuombea Amani Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu  Paulo VI, tarehe Mosi, Januari 1968. Takribani miaka 53 iliyopita. Mtakatifu Paulo VI alituma ujumbe wa amani kwa familia ya Mungu duniani kwa kuonesha kuwa, amani ni chachu ya maendeleo ya watu na kwamba, kinzani, misigano na utaifa usiokuwa na mashiko, ni mambo yanayotishia amani duniani. Kumbe, vita, migogoro na kinzani mbali mbali zinaweza kupatiwa ufumbuzi kwa kujikita katika: sheria, haki, usawa, upendo; ukweli na uhuru; tunu ambazo zinaonesha umuhimu wa pekee hata katika ulimwengu mamboleo. Mtakatifu Paulo VI anasema, amani ni jina jipya la maendeleo fungamani. Hivyo basi, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu utu na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Waamini na watu wote pamoja na watu wenye mapenzi mema, wanapaswa kutangaza na kushuhudia Injili ya Amani Duniani kwa kuzingatia utu wa binadamu na haki zake msingi!

Mtakatifu Yohane XXXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anakaza kusema, amani ya kweli inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 53 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu: Amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia. Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maagamizi, kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali mawazo ya vitisho na hofu. Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anapembua kwa kina na mapana amani, kama safari ya matumaini inayokabiliana na vizingiti pamoja na majaribu. Amani ni safari ya ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza unaosimikwa katika kumbu kumbu, mshikamano na udugu wa kibinadamu. Amani ni safari ya upatanisho katika umoja wa kidugu. Amani ni safari ya wongofu wa kiekolojia na kwamba, watu wataweza kupata yale yote wanayotumainia.

Dr.  Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika hotuba yake elekezi wakati wa kuwasilisha ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya kuombea amani duniani kwa Mwaka 2020, amekazia kwamba, tangu kuanzishwa kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kunako mwaka 1968, binadamu daima amekuwa na kiu ya amani kutoka katika undani wa maisha yake. Mtakatifu Paulo VI akatoa ujumbe wa amani wakati ambapo dunia ilikuwa imegubikwa na Vita Baridi pamoja na hofu ya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Kwa upande wake Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anasema, Kanisa linapoadhimisha Sherehe ya Noeli, ujumbe unaosikika kutoka kwa Malaika mbinguni ni amani duniani na wachungaji waliokuwa kondeni wakaondoka kwa haraka kwenda mjini Bethlehemu. Amani ni safari ya matumaini: Majadiliano, Upatanisho na Wongofu wa kiekolojia.

Amani na utulivu wa Jumuiya ya Kimataifa, hauwezi kamwe kujengeka katika msingi wa vitisho na hofu ya maagamizi, kumbe, kuna haja ya kuvunjilia mbali mawazo ya vitisho na hofu. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani anataja vikwazo na vizingiti vya safari ya amani duniani ambavyo kwa ufupi kabisa ni vita, kinzani na mipasuko mbali mbali duniani pamoja na ukosefu wa haki jamii. Wakati huo huo, Monsinyo Bruno Marie Duffè,  Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya binadamu amekazia kuhusu amani kama safari ya wongofu wa kiekolojia, kwa kuwa na matumizi bora ya rasilimali za dunia badala ya kutumia utajiri wa dunia kwa vita na vitendo vya uvunjifu wa haki kiasi cha kushindwa kulinda na kuendeleza kazi ya uumbaji. Uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka vinapelekea watu kushindwa kuthamini jumuiya asilia, kutunza mazingira nyumba ya wote pamoja na kulinda mafao ya wengi.

Maafa makubwa yaliyosababishwa na mashambulizi ya silaha za atomiki kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki yawe ni fundisho kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimiana na kuthaminiana sanjari na kuelekeza rasilimali za dunia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Naye Prof. Gabriella Gambino Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, amesisitiza kwamba, Mama Kanisa ameendelea kuwa ni chombo na shuhuda wa matumaini sehemu mbali mbali za dunia kwa kuwarithisha watu wa Mungu tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kwa njia ya huduma mbali mbali za kijamii, hususani: elimu, afya na ustawi wa kijamii. Tangu mwanzo Kanisa linatambua kwamba, familia ni shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Ni mahali pa kujifunza kupenda na kupendwa, kusamehe na kusahau. Ni kutokana na muktadha huu, familia inapashwa kuwa ni chemchemi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Lakini kwa sasa familia inakumbana na changamoto mbali mbali kiasi hata cha kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake msingi katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, demokrasia, ustawi na maendeleo ya wengi. Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya ujenzi wa amani duniani. Upweke hasi ni chanzo cha hofu na wasi wasi unaopelekea hali ya kudhaniana vibaya, kinzani, misigano na hatimaye, vita. Familia ya Kikristo mintarafu vinasaba vya maisha yake, inapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa amani, uhuru unaowajibisha pamoja na ukweli. Kuna haja kwa familia kuwafunda vijana wa kizazi kipya umuhimu wa kuthamini michezo, wongofu wa kiekolojia; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana na kujadiliana na wengine katika ukweli na uwazi. Vijana wawe na ujasiri wa kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii, kwa kuguswa na furaha pamoja na mahangaiko ya jirani zao.

Vijana wawe mstari mbele kuwatetea maskini na wanyonge katika jamii pamoja na kuwa na matumizi bora ya njia za mawasiliano ya jamii. Bila kuzingatia mambo haya, vijana wengi watajikuta wametumbukia katika anasa kupita kiasi, kwa kuzama katika ombwe na ulimwengu wa kufikirika, ukatili wa kimtandao mambo yanayopelekea vijana wengi kukengeuka na kutopea katika maadili na utu wema. Familia iwe ni kitovu cha ujenzi wa mahusiano bora kwa kuaminiana na kuthaminiana; kwa kujisadaka na kujitosa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

[ Audio Embed Siku ya Amani Duniani 2020]  

23 December 2019, 11:05