Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na Shirikisho la ACEC katika maadhimisho ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na Shirikisho la ACEC katika maadhimisho ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake.  (ANSA)

Papa: ACEC Dumisheni: Umoja, Ubunifu na Mwelekeo mpana zaidi.

Wajumbe wa ACEC wanapaswa kujizatiti katika mchakato wa umoja na ushirikiano, kwa kukazia ushupavu, ubunifu sanjari na wanachama wake kuwa na mwelekeo mpana zaidi kwa kutambua kwamba, Sinema zilizochezwa mara baada ya Vita Kuu ya Dunia ni shule kwa ajili ya familia ya binadamu. Watengenezaji wa Sinema nchini Italia wanapaswa kulitambua na kuthamini mchango huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirikisho la Kikatoliki la Wamiliki wa Kumbi za Sinema “Associazione cattolica Esercenti Cinema-Sale della Comunità, ACEC” lilianishwa kunako mwaka 1949 na katika kipindi cha Mwaka 2019 linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 ya uwepo wake katika kusimamia na kuendesha kumbi za Sinema nchini Italia. Ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano, kuna haja kwa wajumbe wa ACEC kuhakikisha kwamba, wanakita sera na miakati yao katika mchakato wa umoja na ushirikiano, kwa kukazia ushupavu na ubunifu sanjari na wanachama wake kuwa na mwelekeo mpana zaidi kwa kutambua kwamba, Sinema zilizochezwa mara baada ya Vita Kuu ya Dunia ni shule makini kwa ajili ya familia ya binadamu. Watengenezaji wa Sinema nchini Italia wanapaswa kutambua na kuthamini mchango huu. Watoto wengine wamefundwa  mambo mazito kutokana na kuangalia Sinema hizi ili kukuza na kudumisha umoja na mafungamano ya kifamilia.

Kwa ufupi hayo yamezungumzwa na Baba Mtakatifu Francisko siku ya Jumamosi, tarehe 7 Desemba 2019 alipokutana na wajumbe wa Shirikisho la Kikatoliki la Wamiliki wa Kumbi za Sinema “Associazione cattolica Esercenti Cinema-Sale della Comunità, ACEC”. Katika mazungumzo yake, amewapatia changamoto tatu muhimu wanazopaswa kuzivalia njuga. Mosi, wahakikishe kwamba, wanajenga na kudumisha umoja na mshikamano. Watambue kwamba, Sinema ni chombo kinachowaunganisha watu na hivyo kujenga umoja na mafungamano ya kijamii. Ni mahali ambapo watu washirikishana matatizo, machungu na matumaini ya maisha. Sinema ni jukwaa linalo elimisha na kuwafunda watu kutokana na matukio mbali mbali yanayooneshwa kwenye Sinema. Sinema zilizotengenezwa mara baada ya Vita Kuu za Dunia ni shule muhimu sana kwa familia ya binadamu.

Kumbe, Shirikisho hili nalo linapaswa kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na mshikamano kama sehemu ya utambulisho wao wa imani na upendo kwa Mungu na jirani. Katika muktadha huu, wataweza kufahamiana vyema na jirani zao. Umoja kati yao pamoja na wadau wengine katika sekta ya mawasiliano ni muhimu sana. Baba Mtakatifu amekazia kipaji cha ubunifu katika sanaa ya utengenezaji wa Sinema kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ni changamoto kubwa kwa watengenezaji wa Sinema kwa wakati huu. Bila ubunifu Shirikisho lao litajikuta limepitwa na wakati na hivyo “kuegeshwa pembeni kama magari mabovu” au “kuhifadhiwa katika majumba ya makumbusho”. Kipaji cha ubinifu hakina budi kwenda sanjari na wongofu fungamani kwa kutumia kikamilifu utajiri na karama za kila mmoja wao. Ushupavu unaomwilishwa katika kipaji cha ugunduzi vitawasaidia kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu.

Baba Mtakatifu analitaka Shirikisho hili kuhakikisha kwamba, linakuwa na mwono na mwelekeo mpana zaidi kwa kusoma alama za nyakati ili kugusa hisia mbali mbali za binadamu. Hii ni chapa ya macho katika uhalisia wa maisha ya watu. Wawe na uwezo wa kuamsha dhamiri za watu ili kuangalia Sinema hizi kwa umakini mkubwa. Matokeo yake ni yanaweza kuwa ni ujenzi wa umoja na ukuaji wa kipaji cha ubunifu; mambo ambayo ni chachu ya mageuzi ya ndani. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanachama hawa kwa sababu wanaonesha vinasaba kwa kupenda na kushikamana na Kanisa. Wajitahidi kuishi vyema hisia na weledi wao Kikanisa, dawa mchunguti inayosaidia kuwadhibiti ili wasitumbukie katika tabia ya kujitafuta, jambo ambalo ni hatari sana kwa maisha.

Papa: Sinema

 

 

07 December 2019, 15:39