Tafuta

Papa Francisko anasema, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni Kitovu cha Kipindi cha Majilio. Papa Francisko anasema, Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni Kitovu cha Kipindi cha Majilio. 

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili: Kiini cha Majilio

Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni kielelezo cha matukio muhimu yaliyojiri katika maisha na utume wa Bikira Maria hata kabla ya Kristo Yesu kuzaliwa. Tangu kutungwa kwake mimba, Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, kielelezo cha upendo wa Mungu unaotakatifuza na hivyo kumkinga Bikira Maria na kila doa la dhambi ya asili ambayo binadamu wote wameirithi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kipindi cha Majilio ni nafasi kwa waamini kulitafakari kwa namna ya pekee, Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu alipozaliwa kwa mara ya kwanza katika historia na maisha ya mwanadamu. Hiki ni kipindi cha subira, imani na matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Majilio ni kipindi kinachomwandaa mwamini kuadhimisha vyema Fumbo la Umwilisho. Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu ni chemchemi ya matumaini, imani na furaha; tema muhimu sana wakati huu na kwamba, Bikira Maria anayo nafasi ya pekee katika maadhimisho ya Kipindi cha Majilio. Tarehe 8 Desemba 2019, Kanisa limeadhimisha Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kiini cha Kipindi cha Majilio. Maadhimisho haya ni kielelezo cha matukio muhimu sana yaliyojiri katika maisha na utume wa Bikira Maria, aliyekingiwa dhambi ya asili hata kabla ya Kristo Yesu kuzaliwa. Tangu kutungwa kwake mimba, Bikira Maria alikingiwa dhambi ya asili, kielelezo cha upendo wa Mungu unaotakatifuza na hivyo kumkinga na kila doa la dhambi ya asili ambayo binadamu wote wameirithi.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 8 Desemba 2019. Malaika Gabrieli alimwamkia Bikira Maria kwa kusema, “Salam uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe”. Tangu mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, Mwenyezi Mungu alipanga na kutekeleza mpango wake kwa Bikira Maria kama kiumbe aliyepewa upendeleo wa pekee kwa kujazwa neema na kufunikwa na upendo wake usiokuwa na kifani. Lakini, ili kumwezesha Mwenyezi Mungu kutekeleza mpango huu, kuna haja kwa mwamini kujitoa bila ya kujibakiza kama alivyofanya Bikira Maria. Akasikiliza kwa makini Neno la Mungu na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu na kumpokea katika maisha yake bila masharti. Ni kwa njia ya Bikira Maria, Neno wa Mungu alifanyika Mwili na kukaa kati ya watu wake. Yote haya yamewezekana kutokana na Bikira Maria kukubali na kuitikia mpango wa Mungu katika maisha yake kwa kusema, “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema”.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria hakumwekea Mwenyezi Mungu vizingiti, bali akawa tayari kujiaminisha na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu atekeleze wajibu wake. Akajisadaka bila ya kujibakiza kwa historia na maisha yake kwa ajili ya Mungu ili kwamba Neno na mapenzi ya Mungu yaweze kutendeka. Ni kutokana na muktadha huu, Bikira Maria akatekeleza kwa dhati kabisa mpango wa Mungu katika maisha yake, akawa ni “mzuri” na “mtakatifu” bila ya kujipendelea. Bikira Maria ni kielelezo cha kazi kubwa ya uumbaji inayojidhihirisha katika unyenyekevu, udogo na ufukara. Bikira Maria ni kioo cha uzuri wa Mungu na ni utimilifu wa upendo, neema na majitoleo binafsi. Bikira Maria anajitambulisha kuwa ni mjakazi wa Bwana, kielelezo cha huduma na majitoleo kwa wenye shida na mahangaiko mbali mbali. Bikira Maria amekuwa kweli ni chombo na shuhuda wa huduma makini kwa jirani kama ilivyojionesha kwa kumtembelea binamu yake Elizabeti baada ya kupashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu. Uwajibikaji mbele ya Mwenyezi Mungu unamwilishwa kwa kuwajibika pia mbele ya jirani, katika hali ya unyenyekevu na upendo usiokuwa na makuu.

Baba Mtakatifu anasema, upendo na matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni mambo yanayomwilishwa katika undani wa mwamini na wala hayahitaji “kufanyiwa matangazo”. Waamini katika Jumuiya zao mbali mbali wanaitwa na kuhamasishwa kufuata mfano bora wa Bikira Maria kwa kutenda yote hayo bila makelele wala kutaka kuonekana mbele ya watu. Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, iwasaidie waamini kuitika “Ndiyo” kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni “Ndiyo” inayo mwabudu Mwenyezi Mungu katika uhalisia huduma na matendo ya upendo kwa Mungu na jirani. Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili ni siku ambayo Chama cha Vijana Wakatoliki nchini Italia, wanarudia tena ahadi zao. Hii iwe ni fursa ya kujizatiti katika hija ya majiundo makini, huduma na shuhuda zenye mvuto na mashiko kwa watu wa Mungu.

Papa: Imakulata
08 December 2019, 16:30