Tafuta

Papa Francisko: Sagari ya Injili Duniani: Ushuhuda wa Mtakatifu Paulo kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu! Papa Francisko: Sagari ya Injili Duniani: Ushuhuda wa Mtakatifu Paulo kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu! 

Safari ya Injili Ulimwenguni: Ushuhuda wa Mtakatifu Paulo!

ushuhuda wa Mtume Paulo ulijikita katika uinjilishaji kwa kuanzisha Jumuiya za Kikristo pamoja kuendeleza utume wa umisionari miongoni mwa watu wa Mataifa, kiasi hata cha kuwa tayari kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Akashutumiwa kwa mashitaka ya uongo, lakini akasimama imara.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Mzunguko wa Katekesi kuhusu Safari ya Injili Ulimwenguni mintarafu Kitabu cha Matendo ya Mitume ni fursa ya kuendelea kupembua: mchango wa Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Mwanzo na uwepo wa nguvu tendaji ya Roho Mtakatifu, uliozindua mchakato mzima wa uinjilishaji unaoendelea kutekelezwa na Mama Kanisa hata katika ulimwengu mamboleo kwa kukazia ushuhuda kama kielelezo cha imani tendaji. Mtume Paulo alipokuwa mbele ya Mfalme Festo alijitetea kwa hekima na busara kiasi hata cha kumstaajabisha Mfalme Festo ambaye alimkemea kwa ukali, lakini akamjibu kwamba, alikuwa ananena maneno ya kweli na ya akili kamili. Aliyasema kwa ujasiri kwa kutambua kwamba, hata Mfalme alikuwa ana waamini Manabii. Lakini Mfalme Agripa alimjibu kwa kejeli akisema, “Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo”.

Mtume Paulo hakuonekana na hatia ya kustahili kifo, lakini kwa sababu alikuwa amekata rufani kwa Kaisaria, ilibidi apelekwe Roma. Kwa ujasiri na hekima kubwa, Mtume Paulo akatangaza na kushuhudia kuhusu: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu! (Rej. Mdo: 9:15-16). Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 11 Desemba 2019 amekiri kwamba, ushuhuda wa Mtume Paulo ulijikita katika uinjilishaji kwa kuanzisha Jumuiya za Kikristo pamoja kuendeleza utume wa umisionari miongoni mwa watu wa Mataifa, kiasi hata cha kuwa tayari kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Mtume Paulo alipopanda na hatimaye kuwasili mjini Yerusalemu, “hali ya hewa” ikachafuka sana, akakutana na upinzani mkubwa, huku akishutumiwa kuwafundisha watu kinyume cha Torati na Hekalu Takatifu. Paulo akapewa nafasi ya kujitetea mbele ya Baraza kuu la Wayahudi.

Mwinjili Luka anasimulia mashtaka dhidi ya Mtakatifu Paulo, akiyaoanisha na mashitaka ambayo Wayahudi walitoa dhidi ya Kristo Yesu. Wanamwona hana hatia, lakini bado anahukumiwa kufa kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu mwenyewe. Hapa kwa hakika mateso ya Paulo Mtume yanakuwa ni Ishara ya Injili hai. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kabla ya Katekesi yake, amekutana na kuzungumza na watu wa familia ya Mungu kutoka Ukraine ambao wamefika mjini Roma kumshukuru Mungu kwa kumbu kumbu ya miaka 30 tangu walipotoka mafichoni na kuanza kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu. Ni waamini ambao walisimama kidete kuhakikisha kwamba, wanatangaza na kushuhudia imani yao bila ya kuogopa kifo, kilichokuwa kinawakodolea macho!

Hata leo hii kuna Wakristo wengi wanaoendelea kudhulumiwa na kuuwawa Barani Ulaya na sehemu mbali mbali za dunia kwa sababu ya imani yao. Wakati mwingine, wanasukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Lakini, ikumbukwe kwamba, kifodini “Martyrium” ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake na kwamba, damu ya wafiadini imekuwa daima ni chemchemi ya kukua na kukomaa kwa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Mama Kanisa anatumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Amani, Upendo na Mshikamano. Mtakatifu Paulo, Mtume ni shuhuda amini wa Kristo Yesu na Kanisa, kiasi hata cha kuthubutu kutoa ushuhuda wa historia ya kuongoka kwake. Kristo Yesu alipenda kumwongoa Paulo, ili aweze kuwa ni Mtume wa Mataifa ili aweze kuwafumbua macho, kuielekea nuru kwa kuachana na dhambi na kumwelekea Mungu ili wapate msamaha wa dhambi zao na urithi miongoni mwao watakaotakaswa na imani inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.

Paulo Mtume, akawafafanulia imani ya Manabii na Musa na kwamba, sasa yeye anayatamka kwa ujasiri ya kwamba, Kristo hana budi kuteswa, kufa na kufufuka kwa wafu ili kuwatangazia watu wake na watu wa Mataifa habari ya Nuru! Huu ni ushuhuda unaozama na kutikisa kabisa sakafu ya moyo wa Mfalme Agripa kiasi hata cha kutaka kumwongoa kuelekea Ukristo. Hatima ya maisha ya Mtakatifu Paulo ikawekwa mikononi mwa Warumi. Akapelekwa Roma akiwa amefungwa, alama ya uaminifu wake kwa Injili na kwa Kristo Mfufuka. Minyororo hii ni kielelezo kinachomdhalilisha mtu, lakini upendo wake mkuu kwa Kristo Yesu anaiangalia minyororo hii kwa jicho la imani, upendo na matumaini. Huu ni ushuhuda wa udumifu wa imani hata katika mateso na madhulumu, kwa kuwa na uwezo wa kuyaangalia yote haya kwa jicho la imani. Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko amewasihi waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba Mtakatifu Paulo, Mtume ili aweze kuwaombea wawe na ujasiri wa kupyaisha imani na kuendelea kuwa mashuhuda amini wa wito wa kikristo, mitume na wamisionari hadi dakika ya mwisho.

Papa: Ushuhuda wa Imani.
11 December 2019, 16:47