Tafuta

Vatican News
Papa Francisko, Askofu mkuu Justin Welby pamoja na Mchungaji John Chalmers wamewaandikia ujumbe wa noeli na matashi mema viongozi wa Serikali ya Sudan ya Kusini. Papa Francisko, Askofu mkuu Justin Welby pamoja na Mchungaji John Chalmers wamewaandikia ujumbe wa noeli na matashi mema viongozi wa Serikali ya Sudan ya Kusini.  (PETERLOUIS)

Ujumbe wa Noeli kwa viongozi wa Kisiasa nchini Sudan ya Kusini

Baba Mtakatifu pamoja na viongozi wenzake, wanapenda kumtolea sala na maombi yao Kristo Yesu, ili awasaidie kuendelea kujizatiti katika upatanisho na udugu. Wanawaombea wananchi wa Sudan ya Kusini, heri, baraka na neema tele. Kristo Yesu, Mfalme wa amani, awaangazie na kuongoza hatua zao katika njia ya wema na ukweli, ili siku moja waweze kutembelea Sudan ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sherehe ya Noeli ni ukumbusho endelevu wa Fumbo la Umwilisho, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni muda muafaka kwa watu wote kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; ukomavu wa imani na mshikamano wa upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe za Noeli, Baba Mtakatifu Francisko akiwa ameungana na Askofu mkuu Justin Welby wa Jimbo kuu la Canterbury ambaye pia ni kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikani pamoja na Mchungaji John Chalmers, ambaye aliwahi kuwa Mchungaji mkuu wa Kanisa la Presibiterian huko nchini Scotland, wanapenda kutoa salam na matashi mema ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2019 pamoja na Mwaka Mpya 2020 kwa viongozi wa kisiasa nchini Sudan ya Kusini.

Viongozi hawa wa kiroho wanawatakia wananchi wa Sudan ya Kusini amani na ustawi na kwamba wako pamoja nao katika kipindi hiki cha mpito, kuelekea katika mchakato wa uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama sehemu ya utekelezaji wa Makubaliano ya Amani. Baba Mtakatifu pamoja na viongozi wenzake, wanapenda kumtolea sala na maombi yao Kristo Yesu, ili awasaidie kuendelea kujizatiti katika mchakato wa upatanisho na udugu. Wanawaombea watu wa Mungu nchini Sudan ya Kusini, heri, baraka na neema tele. Kristo Yesu, Mfalme wa amani, awaangazie na kuongoza hatua zao katika njia ya wema na ukweli, ili hatimaye waweze kuzima ile kiu ya kutaka kutembelea Sudan ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko na Askofu mkuu Justin Welby wameonesha nia ya kutembelea Sudan ya Kusini kwa pamoja, Mwenyezi Mungu akiweka mkono wake, mwaka 2020, ingawa tarehe rasmi bado haijapangwa.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa nchini Sudan ya Kusini, ilipaswa kuundwa tarehe 12 Novemba 2019, kadiri ya makubaliano yaliyofikiwa mwezi Septemba 2019, baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo na shinikizo kutoka Umoja wa Mataifa, Marekani na nchi za kikanda.

Wanasiasa Sudan ya Kusini
25 December 2019, 15:36