Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko: Urbi et Orbi kwa Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2019: Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko: Urbi et Orbi kwa Sherehe za Noeli kwa Mwaka 2019: Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa. 

Papa Francisko: Ujumbe wa Urbi et Orbi:2019: Yesu Mwanga wa Mataifa!

Papa Francisko amewakumbuka wananchi wanaoishi Mashariki mwa DRC, ambao wameathirika kwa madhara ya vita na kinzani ya kijamii; ni watu ambao wameteseka sana kwa maafa asilia pamoja na milipuko ya magonjwa. Mwanga angavu wa Kristo Yesu, uwe ni faraja kwa wale wote wanaoteseka kutokana na imani yao, husasan wamisionari na waamini ambao wametekwa nyara!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Nabii Isaya anasema, watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu! Katika tumbo la Kanisa, amezaliwa tena Mwana wa Mungu, aliyefanyika mtu. Jina lake ni Yesu maana yake Mungu anaokoa. Mwenyezi Mungu, Baba wa milele, upendo wake hauna mipaka na kwa jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, si kwa ajili ya kuuhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Mwenyezi Mungu amemtoa Mwanawe wa pekee kwa huruma kubwa, kwa ajili ya watu wote na kwa daima. Mwana wa Mungu amezaliwa katika hali ya giza nene, akawa kama mshumaa unaowaka gizani katika ubaridi wa usiku wa manane! Baba Mtakatifu Francisko katika salam zake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, “Urbi et Orbi” kwa Noeli ya Mwaka 2019 anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumwangalia na kumtafakari Mtoto Yesu aliyezaliwa na Bikira Maria, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.

Hili ni Neno ambalo limekuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya Abrahamu kuelekea kwenye nchi ya ahadi na bado inaendelea kuwa na mvuto na mashiko kwa wale wote wanaojiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Hili ni Neno ambayo limewaongoza Wayahudi katika safari ya ukombozi kutoka utumwani Misri na linaendelea kuwaita wale wote wanaoendelea kugandamizwa katika kongwa la utumwa mamboleo, ili hatimaye, waweze kuokolewa na kutoka katika magereza haya ya utumwa! Hili ni Neno angavu ambalo limetwaa mwili na kufanyika kuwa ni Mwana wa mtu, Kristo Yesu, mwanga wa mataifa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ndiyo maana Nabii Isaya anasema, watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu. Ni kweli kabisa katika sakafu ya moyo wa mwanadamu kuna giza nene, lakini mwanga angavu wa Kristo Yesu ni mkubwa zaidi. Kuna giza katika mahusiano na mafungamano ya watu binafsi, katika familia na jamii katika ujumla wake, lakini mwanga angavu wa Kristo Yesu ni mkubwa zaidi.

Kuna giza katika kinzani na mipasuko ya kiuchumi, kijiografia na kiekolojia, lakini mwanga angavu wa Kristo Yesu bado unag’ara zaidi. Ni matamanio ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kristo Yesu, awe ni mwanga angavu wa watoto wengi wanaoteseka kutokana na vita na kinzani huko Mashariki ya kati na katika sehemu mbali mbali za dunia. Mwanga wa Kristo Yesu, uwe ni faraja kwa watu wa Mungu huko Siria, nchi ambayo bado inateseka kwa chuki na uhasama; mambo ambayo yamesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao kwa takribani miaka kumi sasa. Mwanga angavu wa Kristo usute dhamiri za watu wote wenye mapenzi mema. Uwasaidie viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kufanya kazi ili hatimaye, waweze kupata suluhu itakayo wahakikishia wananchi wa Siria usalama, amani na utulivu kwa kuwaondolea mateso na mahangaiko yao. Mwanga wa Kristo Yesu, uwe ni nguzo na msaada kwa wananchi wa Lebanon, ili hatimaye, waweze kutoka salama katika hali tete ya kisiasa, na hatimaye, waweze kugundua tena wito wao kwa kutambua kwamba, wao ni wajumbe wa uhuru, utulivu na maridhiano.

Baba Mtakatifu anasema, Mwanga wa Kristo Yesu uwaangazie watu wa Mungu katika Nchi Takatifu, mahali alikozaliwa Mkombozi wa binadamu; mahali ambapo hata katika mateso na mahangaiko yao, wanaendelea kutumaini siku ya amani, usalama, ustawi na maendeleo. Mwanga wa Kristo Yesu, uwe ni faraja kwa watu wa Mungu nchini Iraq wanaokabiliana kwa sasa na machafuko ya kijamii bila kusahau wananchi wa Yemen wanaopitia kipindi kigumu cha mateso na mahangaiko makuu. Mtoto Yesu kutoka Bethlehemu awe ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu Barani Amerika, ambako kuna baadhi ya nchi ambazo kwa sasa zinapitia kipindi kigumu cha machafuko ya kisiasa na kijamii. Mtoto Yesu awe ni faraja kwa watu wa Mungu nchini Venezuela wanaoteseka kutokana na kinzani za kisiasa na kijamii, ili hata katika muktadha huu, kamwe wasikose kupata msaada wanaouhitaji. Mtoto Yesu awalinde na kuwabariki wale wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya haki na upatanisho, wawe na ujasiri wa kuweza kuvuka vikwazo mbali mbali pamoja na mifumo ya umaskini inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Mtoto Yesu awe ni mwanga angavu kwa wananchi wa Ukraine, wanaoendelea kutumainia suluhu itakayowawezesha kupata amani ya kudumu. Mtoto Yesu aliyezaliwa, awe ni mwanga angavu kwa watu wa Mungu Barani Afrika ambako kutokana na hali za kisiasa na kijamii, watu wengi wanalazimika kuzikimbia na kuzihama nchi zao, kiasi cha kuwakosesha watu makazi na familia. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka wananchi wanaoishi Mashariki mwa DRC, ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa na madhara ya vita na kinzani ya kijamii; ni watu ambao wameathirika vibaya na maafa asilia pamoja na milipuko ya magonjwa. Mwanga angavu wa Kristo Yesu, uwe ni faraja kwa wale wote wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao, husasan wamisionari na waamini ambao wametekwa nyara na hawajulikani mahali waliko. Kristo Yesu awe ni kimbilio la watu wanaoshambuliwa kutokana na misimamo mikali ya kidini sanjari na vitendo vya kigaidi hasa huko Burkina faso, mali, Niger na Nigeria.

Mwana wa Mungu aliyeshuka kutoka mbinguni awe ni mlinzi na msimamizi wa wale wanaoteseka kutokana na ukosefu wa haki msingi za binadamu; watu wanaolazimika kuzikimbia nchi na familia, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao kwa kutembea jangwani na kusafiri majini na matokeo yake, “wamezama na kupotelea huko kama risasi ndani ya maji”. Mwana wa Mungu awe ni mtetezi wa wale wote wanaokabiliana na nyanyaso mbali mbali; watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo na huko wanawekwa vizuizini na kukabiliwa na mateso makali. Hawa ni watu ambao wanazuiliwa kupata hifadhi mahali ambako palionekana kuwa ni chemchemi ya matumaini na maisha bora, lakini matokeo yake wanakutana na “kuta za chuma cha pua” pamoja na watu kuwageuzia kisogo! Emmanueli, yaani Mungu pamoja nasi, awe ni mwanga angavu wa binadamu aliyejeruhiwa kutokana na ubinafsi, ili kwa toba na wongofu wa ndani, watu waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu; furaha na matumaini kwa watoto sehemu mbali mbali za dunia, hasa zaidi wale waliotelekezwa na wanaokumbana na nyanyaso mbali mbali katika maisha yao. Kwa njia ya waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wasaidie kuwavika nguo walio uchi; kuwapa chakula kwa wenye njaa, na kutoa huduma bora ya afya kwa wagonjwa.

Wawe karibu zaidi na wazee, wakimbizi, wahamiaji na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Sherehe ya Noeli iwe ni chemchemi ya wema na mwanga angavu ili kufukuzia mbali giza linalouandama ulimwengu.

Papa: Urbi et Orbi

 

 

25 December 2019, 16:25