Tafuta

Vatican News
Papa Francisko amekutana na viongozi wa Baraza kuu la Watendaji wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarnosc" afafanua maana ya "mshikamano. Papa Francisko amekutana na viongozi wa Baraza kuu la Watendaji wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarnosc" afafanua maana ya "mshikamano.  (Vatican Media)

Maana ya Mshikamano Kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa

Baba Mtakatifu Francisko anasema Changamoto kubwa kwa wakati huu ni ile ya kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu kati ya waja wake. Uwepo wa Mungu hufuatana na juhudi za dhati za mtu mmoja mmoja na za makundi ya watu kutafuta ari na maana katika maisha yao. Mwenyezi Mungu hukaa miongoni mwao, akihamasisha mshikamano, udugu, ustawi, ukweli na haki. Mshikamano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 4 Desemba 2019 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Baraza Kuu la Watendaji wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarność" kama sehemu ya maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 40 tangu kuanzishwa kwake kunako mwaka 1980. Shirikisho hili limekuwa ni moto wa kuotea mbali katika mchakato wa kuleta mabadiliko ya kisiasa na kijamii ndani na nje ya Poland. Ni Shirikisho ambalo linajipambanua kwa kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wafanyakazi nchini Poland. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni ile ya kutambua uwepo wa Mwenyezi Mungu kati ya waja wake. Uwepo wa Mungu hufuatana na juhudi za dhati za mtu mmoja mmoja na za makundi ya watu kutafuta ari na maana katika maisha yao. Mwenyezi Mungu hukaa miongoni mwao, akihamasisha mshikamano, udugu, ustawi, ukweli na haki.

Takribani miaka 40 iliyopia, Mtakatifu Yohane Paulo II aliwahimiza watu wa Mungu nchini Poland kutambua uwepo endelevu wa Mungu na hivyo kumwomba nguvu ya Roho Mtakatifu, ili aweze kushuka na hivyo kupyaisha uso wa dunia. Mshikamano wa upendo na wale wote wanaotafuta haki zao msingi unaomwilishwa katika maeneo ya kazi, elimu, mafungamano ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimataifa ni kielelezo makini cha waamini kujiweka wazi mbele ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, neno “Mshikamano” limechakachuliwa kiasi cha kueleweka vibaya, lakini linataja kitu ambacho ni zaidi ya matendo machache ya ukarimu. Ikumbukwe kwamba, mshikamano kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mwitikio huria wanao utoa wale wanaotambua kwamba kazi ya kijamii ya mali na lengo lake la jumla la bidhaa ni mambo ya kiuhakika yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya mali binafsi.

Huu ni mwaliko wa kusimama kidete kulinda na kutetea watu ambao wamepokwa: utu, heshima na haki zao msingi. Hawa ndio wale wanaofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, bila ya kupata ujira wa haki unaokidhi mahitaji yao msingi kwa ajili ya kuzitegemeza familia zao au kupata huduma bora ya afya au mapumziko. Katika majadiliano kati ya Dola pamoja na jamii, Kanisa halina suluisho kwa kila suala maalum. Lakini kwa kushirikishana na wadau mbali mbali katika jamii linaweza kupata majibu msingi ili kutetea utu wa binadamu, ustawi na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anawakumbusha wajumbe hawa kwamba, kubadilisha miundo bila kujenga hoja na mitazamo mipya kutahakikisha tu kwamba mara moja au baadaye, miundo hiyo hiyo haitaweza kufua tena dafu na hata wakati mwingine kusababisha madhara makubwa zaidi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amewaombea karama na mapaji ya Roho Mtakatifu viwasaidie wao kama watendaji wakuu pamoja na wafanyakazi wote Vyama Huru vya Wafanyakazi nchini Poland "Solidarność", ili ari na mwamko huu uweze kupata chimbuko lake katika tunu msingi na kanuni za Injili yaani kuchukuliana mizigo na kuitimiza hiyo sheria ya Kristo. Na hatimaye, akawaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Mari Mama wa Mungu na Malkia wa Poland, ili waendelee kudumu katika utekelezaji wa shughuli na utume wao.

Papa: Poland

 

04 December 2019, 16:41