Tafuta

Vatican News
Papa Francisko asikitishwa na hali tete inavyoendelea kushika kasi nchini Iraq kiasi cha kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao! Papa Francisko asikitishwa na hali tete inavyoendelea kushika kasi nchini Iraq kiasi cha kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao!  (AFP or licensors)

Papa Francisko asikitishwa na hali ya kisiasa nchini Iraq: Kipigo kwa waandamanaji!

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya tafakari yake ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na hali tete inavyojitokeza nchini Iraq. Waandamanaji nchini Iraq, wameshambuliwa na vikosi vya ulinzi na usalama kiasi cha kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu anawaombea watu wa Mungu nchini Iraq amani, utulivu na maridhiano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 1 Desemba 2019 kwa ajili ya familia ya Mungu kutoka DRC amegusia kuhusu maana ya kipindi cha Majilio yaani Mwanzo wa Mwaka Mpya wa Kanisa. Hapa Kanisa linangojea ujio wa Pili wa Kristo Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu, changamoto na mwaliko wa kuendelea kujikita katika matumaini, huku wakiwa wanasindikizwa na mafundisho ya Nabii Isaya. Majilio ni hija ya matumaini kumwendea Kristo Yesu, ili aweze kuzima kiu ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati. Majilio ni kipindi cha kumpokea Kristo Yesu anayekuja kama mjumbe wa amani anayewaonesha watu njia ya Mungu. Majilio ni kipindi cha kukesha na kusali; kwa kuwa na moyo wazi na huru unaojielekeza zaidi katika huduma kwa Mungu na jirani. Ni changamoto na mwaliko wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya umoja na udugu wa kibinadamu yanayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Ujio wa Kristo Yesu, uamshe tena na tena mshangao wa matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu, kwa kumpatia kipaumbele cha kwanza katika maisha. Kukesha ni mchakato unaomwezesha mwamini kuwa makini kusikiliza na kujibu kilio na mahitaji msingi ya binadamu, kama kielelezo cha ushuhuda wa uwepo wa Mungu kati ya waja wake. Baba Mtakatifu mara baada ya tafakari yake ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na hali tete inavyojitokeza nchini Iraq. Waandamanaji nchini Iraq, wameshambuliwa na vikosi vya ulinzi na usalama kiasi cha kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu anawaombea watu wa Mungu nchini Iraq amani na utulivu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amelipongeza Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kuanzisha Kitengo cha Ushauri wa Vijana Kimataifa, kinachoundwa na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hili ni jibu makini la mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyoadhimishwa kunako mwaka 2018.

Dhamana na wajibu wa Kitengo hiki ni kusaidia kuona vipaumbele vya shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana wa kizazi kipya pamoja na tema mbali mbali zinazohusu maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana.

Papa: Iraq

 

01 December 2019, 15:26