Tafuta

Vatican News
Papa Francisko, Jumatatu tarehe 9 Desemba 2019 amekutana na wanachama wa asasi za kiraia "A Chance in Life" Papa Francisko, Jumatatu tarehe 9 Desemba 2019 amekutana na wanachama wa asasi za kiraia "A Chance in Life"  (Vatican Media)

Papa Francisko: Zingatieni ekolojia fungamani, utu na heshima ya binadamu!

Kwa kuendelea kuwa waaminifu katika karama ya muasisi wa asasi hii, wamejitahidi kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa elimu. Juhudi hizi zinachota utajiri na amana yake kutoka katika Waraka wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Lengo ni kukazia ekolojia fungamani na utu wa mtu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Asasi ya kiraia ya “A Chance in Life” ilianzishwa kunako mwaka 2010 ili kujenga daraja kati ya asasi za huduma ya kijamii zilizokuwa zinatekeleza nyajibu zake nchini Urussi, hasa katika masuala ya kijamii pamoja na kuunga mkono jitihada za watoto kupata elimu makini. Asasi hii imekuwa ikijihusisha pia kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia matatibu ya watoto wenye uhitaji mkubwa zaidi na imekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya huduma kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi katika masuala ya elimu ili hata wao waweze kuona furaha ya Injili hata katika shida na mahangaiko yao. Wajumbe wa Asasi ya “A Chance in Life”, Jumatatu, tarehe 9 Desemba 2019 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Wazo la kuanzishwa kwa asasi hii lilitolewa na Monsinyo John Patrick Carroll-Abbing na leo hii, imekuwa ni chombo cha faraja kwa watoto wengi kutoka Italia, Bolivia, Columbia, Guatemala na Perù, ili kutoa nafasi ya kuweza kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha ya kila mtoto.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa ukarimu hasa kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, kwa kuwasaidia kurejea tena katika jamii, huku wakiongoza na kanuni ya vijana wenyewe kujitawala na kujiongozwa. Kwa kuendelea kuwa waaminifu katika karama ya muasisi wa asasi hii, wamejitahidi kusoma alama za nyakati na kujibu changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa elimu. Juhudi hizi zinachota utajiri na amana yake kutoka katika Waraka wake wa kitume “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Lengo ni kukazia ekolojia fungamani inayopania ustawi na maendeleo ya kila mtu pamoja na dunia inayowazunguka.

Baba Mtakatifu anawapongeza wajumbe wa asasi hii kwa kuhakikisha kwamba, wanawajengea uwezo vijana wa kizazi kipya kama raia kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo, utu, heshima na haki msingi za binadamu zikipewa kipaumbele cha kwanza. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanahitajika ili kuweza kufikia malengo haya. Ikiwa kama wamehamasika vya kutosha wanaweza kufikia malengo yao kwani hawa ni vijana waliozaliwa na kukulia kwenye mazingira ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba,  msaada wao katika ngazi ya kitaifa unahitajika san ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru kwa mchango wao wa kutoa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mapendo, awakirimie nguvu na ujasiri wa kusonga mbele katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Papa: Chance to life

 

09 December 2019, 15:00