Tafuta

Vatican News
Tarehe 8 Desemba 2019, Kardinali Pietro Parolin amezindua Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Miaka 100 ya Madhabahu ya B. Maria wa Loreto. Tarehe 8 Desemba 2019, Kardinali Pietro Parolin amezindua Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Miaka 100 ya Madhabahu ya B. Maria wa Loreto.  (Vatican Media)

Jubilei ya Miaka 100 ya Madhabahu ya B. Maria wa Loreto: 2019-2020

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Miaka 100 ya Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto yamezinduliwa tarehe 8 Desemba 2019 na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kilele chake ni tarehe 10 Desemba 2020. Papa Benedikto XV alimtangaza Bikira Maria wa Loreto kuwa ni msimamizi wa marubani na wasafiri wanaotumia usafiri wa anga duniani, watamani kwenda mbinguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto yaliyoko nchini Italia, ni sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa familia ya Mungu! Watu wanataka kuona matendo kama kielelezo cha imani tendaji! Sala, toba na wongofu wa ndani pamoja na tafakari ya kina ya Neno la Mungu ni nyenzo muhimu sana katika uinjilishaji mpya, ili kuwawezesha waamini kugundua na kuonja uwepo fungamani wa Mungu katika historia, maisha na matukio mbali mbali wanayokumbana nayo katika safari ya maisha ya hapa duniani. Kwa njia hii, waamini watakuwa na ujasiri wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na jirani zao, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wanaohitaji msaada zaidi!Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Miaka 100 ya Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto yamezinduliwa tarehe 8 Desemba 2019 na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican na kilele chake ni tarehe 10 Desemba 2020.

Papa Benedikto XV alimtangaza Bikira Maria wa Loreto kuwa ni msimamizi wa marubani na wasafiri wanaotumia usafiri wa anga duniani, ili katika huduma yao, wawasaidie pia waamini kutamani kwenda mbinguni, ili kuungana na Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia. Kumbe, viwanja vya ndege ni mahali muafaka pia kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji kutokana na ukweli kwamba, kuna umati mkubwa wa watu wanaosafiri kwenda sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 11 Desemba 2019 amewakumbusha waamini kwamba, tarehe 10 Desemba 2019, Kanisa zima limeadhimisha Kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Loreto, nafasi adhimu ya kuendelea kulitafakari Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipotwaa mwili na kukaa kati ya watu wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuyaelekeza macho yao mbinguni. Hatimaye, amewaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Loreto, ili aweze kuwasaidia kwenda mbinguni.

Katika mahubiri ya kuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Miaka 100 ya Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto, Kardinali Pietro Parolin amegusia kuhusu Fumbo la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili amesema, Papa Pio IX kunako tarehe 8 Desemba mwaka 1854 katika Waraka wake wa Kitume “Ineffabilis Deus”, alitangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili. Haya ni mafundisho tanzu ya Kanisa, kielelezo cha mng’ao wa utukufu wa Bikira Maria! Tangu mwanzo wa kuumbwa kwa ulimwengu, Mwenyezi Mungu alipanga na kutekeleza mpango wake kwa Bikira Maria kama kiumbe aliyepewa upendeleo wa pekee kwa kujazwa neema na kufunikwa na upendo wake usiokuwa na kifani. Kumbe, Bikira Maria ni mwombezi kwa ajili ya wokovu wa watu.

Kanisa linakiri kwa dhati huduma hii ya Bikira Maria, ili kwa kutegemezwa na msaada wake wa daima, waamini waweze kuambatana zaidi na Kristo Yesu ambaye ni Mpatanishi na Mkombozi wa ulimwengu. Lengo la madhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Miaka 100 ya Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto ni kwa waamini kuchuchumilia na kuambata toba, wongofu na utakatifu wa maisha, kwa kuwa wakamilifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu. Utakatifu huu umwilishwe katika huduma kwa maskini kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria.

B. Maria wa Loreto: Jubilei

 

 

 

12 December 2019, 15:48